Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, hiki ni kitabu cha nane ambacho tunakutumia mwaka huu 2015 katika utaratibu wetu wa wewe msomaji kutumiwa kitabu kimoja kila mwezi.
Swali ni je unasoma vitabu hivi au tunavituma tu kukamilisha utaratibu? Kama havisomwi ni bora tukaitumia nafasi hii ya kila mwezi kutoa makala nyingine nzuri kwa maisha yetu sote. Na kama unavisoma tafadhali niandikie email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz na nishirikishe chochote ambacho unaendelea kupata kwenye vitabu hivi.

 
Mwezi huu wa nane tunashirikishana kitabu kinaitwa EAT MOVE SLEEP nafikiri kwa kiswahili inaeleweka vizuri kabisa kwamba kitabu hiki kitakuwa kinahusiana na nini. Kitabu kinahusiana na kula, kufanya mazoezi na kulala. Unajua vitu hivyo vitatu vinajenga nini? Vinajenga afya yako. Na unajua afya yako inajenga nini? Inajenga maisha yako. Hivyo kama unataka uwe na maisha bora unahitaji kuanzia wapi? Anzia kwenye afya yako.
SOMA; Afya Yako Ni Kitu Muhimu Sana.
Hakuna kitu muhimu kwako kuzidi afya yako, HAKUNA, hata ungekuwa na fedha nyingi kiasi gani, kama afya yako ni mbovu maisha yako yataishia kuwa mabovu.
Katika semina za kuweka malengo ambazo huwa nafundisha kila mwanzoni mwa mwaka, nimekuwa nasisitiza sana kwamba katika malengo yako usiache kuweka malengo ya kiafya. Ni muhimu sana kwa sababu bila afya imara huwezi kufikia mafanikio mengine.
Wengi wetu tunakazana sana kufikia mafanikio na kusahau afya zetu, inafika wakati unazo fedha nyingi ila afya yako ni ya hovyo, hata fedha huwezi kuzifurahia. Kwa mfano umesahau afya yako na kukazana kutafuta fedha, halafu wakati umezipata ukaambiwa una kisukari au una presha, ni dhahiri kwa kuwa na magonjwa haya huwezi kuishi kama unavyotaka kuishi. Japo una fedha za kuamua uishije, afya yako itakuletea vikwazo vingi.
Ni kutokana na umuhimu huu wa afya yako nimeona ni vizuri kukushirikisha kitabu kinachoelezea kuhusu afya yako.
Kitabu EAT MOVE SLEEP ni kitabu ambacho kinaongelea mambo haya matatu muhimu sana kwa afya yako. Hivi unajua kwamba vitu hivi vitatu ndio msingi mkuu wa afya yako?
Msingi wa kwanza unakula nini?
Huu ni muhimu sana kwa sababu kwa dunia tunayoishi sasa, tunakula sumu nyingi sana. Kwa nje utaona ni vyakula vizuri na vitamu, ila vikifika ndani ya mwili vinakuwa sumu sana. Vinachochea kansa, vinaleta magonjwa ya kisukari na presha na pia vinasababisha uzito wa mwili unaongezeka.
Katika kitabu hiki mwandishi amechambua sana kuhusu vyakula tunavyokula, vipi ni sumu kwetu na vipi ni vizuri kwetu kula. Usuthubutu kuacha kusoma kitabu hiki, miaka kumi ijayo utashukuru sana kukijua kitabu hiki leo, kama utafanyia kazi. Au utajitia sana kwa sababu ulipata nafasi ya kujifunza lakini hukuitumia.
SOMA; Tabia Tano(5) Za Wafanyakazi Ambao Ni Sumu Kwenye Eneo La Kazi Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
Msingi wa pili unafanya mazoezi kiasi gani?
Kitu kikubwa na cha tofauti nilichojifunza kwenye kitabu hiki ni kwamba kumbe ule muda wa kufanya mazoezi nusu saa au saa moja kwa siku tunajidanganya. Muda huu hautoshi kabisa kwa wewe kuwa na afya bora. Hata kama unafanya mazoezi magumu kiasi gani kwa saa moja, kama masaa mengine yote ya siku unakuwa umekaa ni kazi bure.
Mwandishi ametoa njia nyingi sana unazoweza kutumia kufanya mazoezi na ukawa na afya bora. Pia mwandishi amezungumzia sigara mpya ambayo watu wengi tunaivuta kwa sasa. Sigara hiyo ni kukaa. Kukaa kunaua watu wengi kuliko madawa yoyote ya kulevya.
Wengi wetu tunafanya kazi zetu tukiwa tumekaa siku nzima, tukitoka kazini tunaenda kukaa tena kupumzika na baadae tunaingia kitandani kulala. Hii ni sumu kubwa sana kwa afya yako. Mwandishi ametoa njia nyingi unazoweza kuhakikisha mwili wako unapata mazoezi ya kutosha hata kama kazi zako ni za kukaa siku nzima.
Nasisitiza tena, usiache kusoma kitabu hiki tafadhali, na yale utakayojifunza yafanyie kazi.
Msingi wa tatu ni unalala?
Kwa kifupi ni kwamba watu wengi hatulali kwa muda unaotosha, na hata huo muda ambao hatulali hakuna jambo la msingi tunalofanya. Mwandishi amegusia jinsi ambavyo wengi wetu tunafikiri tunaongeza uzalishaji kwa kupunguza muda wa kulala, kumbe ndio tunapunguza zaidi uzalishaji wetu. Na hata kulala sio muda unaokuwa kitandani, bali ubora wa usingizi wako ni muhimu pia.
Kwa kifupi niseme kama uko makini na maisha yako, kama unataka kweli kuwa na mafanikio makubwa na ya kudumu kwenye maisha yako, basi soma kitabu hiki. Au usikisome na endelea kuishi maisha ambayo yatakupoteza. Uzuri ni kwamba maisha ni yako na uchaguzi ni wako.
Kupata kitabu hiki, EAT MOVE SLEEP, bonyeza hayo maandishi ya kitabu na utakipakua.
Soma kitabu hiki, utapata maarifa ya kuboresha maisha yako, na hiko ndio kitu muhimu sana kwako.
Nakutakia kila la kheri kwenye usomaji wa kitabu hiki na vingine ambavyo tumekutumia.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.
TUPO PAMOJA.