Kitabu 100 WAYS TO MOTIVATE OTHERS ni kitabu kinachokupa maarifa ya kuweza kuwahamasisha wengine ili kuweza kua na kufabya zaidi.
Kumbuka kwamba mafanikio yako kwenye kazi na hata maisha yanategemea ni jinsi gani unaweza kuwahamasisha wengine ili waweze kutimiza majukumu yao.
Hapa kuna mambo 20 nitakayokushirikisha kutoka kwenye kitabu hiki.
1. Kama wewe ni kiongozi wa kazi au una watu wanaofanya kazi chini yako, ni muhimu sana uweze kuwahamasisha. Watu wana uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yao lakini kama watakosa mtu wa kuwaonesha hilo ni vigumu kufanyia kazi.
Popote ulipo, hakikisha unaweza kuwahamasisha wanaokuzunguka ili waweze kufanya zaidi ya wanavyofanyq sasa.
2. Hatua ya kwanza kabisa ya kuwahamasisha wengine ni wewe mwenyewe kuwa umehamasika. Hamasa inaambukizwa, kama huna hamasa huwezi kuwahamasisha wengine. Kama unajiona uko chini ma hata wanaokuzunguka watakuwa chini. Unapokuwa na hamasa na kile unachofanya ni rahisi wanaokuzunguka na wao kuwa na hamasa.
Unakuwaje na hamasa?
1. Penda kile unachofanya.
2. Jua kwa nini unafanya unachofanya.
3. Jifunze zaidi kuhusiana na unachofanya.
4. Mara zote menda hatua ya ziada.
3. Huwezi kuwadhibiti watu. Huwezi kuwalazimisha watu wawe na hamasa. Unachoweza kufanya ni kuwafanya watu wajihamasishe wenyewe.
Wewe unachofanya ni kuwaonesha watu kwamba wanaweza kufanya zaidi ya wanavyofanya sasa. Wanaweza kupata zaidi ya wanachopata sasa. Na wenyewe wachukue hatua ya kufikia kile ambacho wameshaamini wanaweza kufikia.
Hivyo badala ya kulazimisha watu wafanye kitu fulani, waoneshe ni jinsi gani itakuwa bora kwao kufanya kitu hiko.
4. Nidhamu binafsi sio kitu ambacho mtu anakuwa nacho au hana. Yaani sio kwamba kuna watu wana nidhamu binafsi na wengine hawana. Kila mmoja wetu ana nidhamu binafsi. Ila sasa tunaamua kuitumia au kutokuitumia.
Unapokuwa na kitu kinachokupa shauku kufanya unatumia vizuri nidhamu yako binafsi. Unapokuwa unafanya kitu ambacho hakikupi hamasa unaacha kutumia nidhamu binafsi yako.
Hatua ya kwanza muhimu ya kuwahamasisha watu ni kuwaonesha kwamba wana nidhamu binafsi na ni maamuzi yao kuitumia au la.
5. Chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo kwenye maeneo ya kazi kwa sasa ni watu kuwa na mawazo mengi, hofu nyingi, mipango mingi, majukumu mengi, vyote kwa wakati mmoja kwenye akili yako.
Akili yako haiwezi kubeba mzigo wote huu kwa wakati mmoja. Boresha maisha yako kwa kuweka jambo moja kwenye akili yako na kuliufanyia kazi mpaka likamilike, kisha nenda kwenye jambo jingine.
6. Watu wanafanya kazi kwa hamasa pale ambapo wanakuwa na mrejesho(feedback). Hakikisha watu wote ambao wanafanya kazi chini yako unawapa mrejesho, kipi wanafanya vizuri na kipi cha kurekebisha.
Watu wakikosa mrejesho kutoka kwako wanatengeneza mrejesho wao wenyewe. Na mara nyingi mrejesho wanaojitengenezea ni wa hofu. Kuona kwamba kile wanachofanya hakitoshelezi au hakikubaliki.
Hata kwenye familia pia, toa mrejesho kila mara.
7. Kila taasisi, kila biashara ni lazima ijiandae kuacha kile wanachofanya sasa kama kweli wanataka kudumu.
Huwezi kuendelea kufanya hiko unachofanya sasa kwa miaka mingi ijayo na ukaendelea kuwa sokoni. Ushindani utakuondoa. Ni lazima uende na mabadiliko yanayotokea. Wahamasishe watu wako kuboresha zaidi kazi zao kila siku ili kutokutolewa sokoni kwa kuachwa nyuma na mabadiliko.
8. Mabadiliko yoyote yanapitia hatua hizi nne. Ni muhimu sana kuzijua na kuwasaidia walioko chini yako ili wasikate tamaa.
Hatua ya kwanza; KUKATAA..
Haya mabadiliko hayatafanya kazi, haya mabadiliko tunakosea.
Hatua ya pili; KUPUUZA.
Sitajihusisha na mabadiliko haya, wacha tuone….
Hatua ya tatu; KUCHUNGUZA.
Nawezaje kuyatumia mabadikiko haya…
Hatua ya nne; KUKUBALI.
Nimekubali mabadiliko haya na nitayafanyia kazi.
Hakikisha unawapeleka vizuri watu wako kwenye maeneo hayo manne unapokuwa na mabadiliko.
9. Watu wanahamasika pale ambapo wanakuwa na mawazo ya hamasa. Mawazo ndio yanaleta kila kitu.
Kama watu wanawaza mawazo ya kukata tamaa ni vigumu sana kuhamasika. Wafanye watu wawe na mawazo kwamba inawezekana na itakuwa rahisi kwao kuhamasika.
10. Mara zote sema ukweli. Watu wanahamasika zaidi kama wanafanya kazi na mtu ambaye anasema ukweli hata kama unauma. Usijidanganye kuwa muongo ili kuwafurahisha watu kwa muda mfupi. Baadae wataujua ukweli na hawatakuheshimu tena na hawatahamasika tena kufanya kazi na wewe.
11. Wasimamizi wengi wa maeneo ya kazi ni watu wa kuzima moto. Wao huangalia ni tatizo gani limeibuka na hukimbilia kulitatua. Kwa mtizamo huu hujikuta wakiona moto kila mahali.
Kama kweli unataka kuwahamasisha wengine, ona matatizo kabla hayajatokea na yatafutie ufumbuzi. Ukiwa mtu wa kuzima moto kila siku utaishia kuona moto kila mahali.
12. Popote ambapo unaweka mawazo yako kwa muda mrefu panakua.
Kama unatumia muda mwingi kufikiria matatizo basi matatizi hayo yatakuwa makubwa zaidi.
Kama utatumia muda mwingi kufikiria mafanikio basi utaona mafanikio zaidi.
Wasaidie watu wanaokuzunguka wawaze zaidi yale majibu mazuri mnayotala kupata.
13. Kuwa makini sana unapoajiri watu wa kukusaidia na mara zote hakikisha unaajiri watu wanaotaka mafanikio, watu ambao wapo tayari kupiga hatua. Ukiajiri watu ambao wameshakata tamaa na maisha yao, huwezi kuwahamasisha hata ungefanya nini.
Chunguza sana tabia na mitazamo ya watu kabla hujawaajiri.
14. Watu wengi huchoka wakiwa kazini ila wakiwa kwenye michezo hawaonekani kuchoka. Mtu akiwa kazini atatafuta kila sababu ya kukwepa majukumu, lakini kwenye mchezo atakuwa tayari kufanya makubwa.
Ifanye sehemu ya kazi kuwa kama mchezo. Wafanye watu wasione ni mzigo bali iwe sehemu ya birudani kwao na watakuwa na hamasa kubwa.
15. Katika wakati wowote ule, una mambo mengi ya kufanya zaidi ya muda ulionao. Unaweza kujiumiza kwa kushindwa kufanya mambo yote hayo. Lakini hilo halitasaidia.
Badala yake chagua jambo ambalo ni muhimu kufanya na fanya hilo tu. Jambo moja kwa wakati mmoja.
16. Kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja sio kuongeza ufanisi, bali kupunguza.
Unaweza kufikiri utafanya zaidi kwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, badaka yake unapunguza ufanisi wako na unashindwa kufanya jambo moja kwa ukamilifu wake.
Acha kabisa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Wahamasishe watu kufanya jambo moja kwa wakati.
17. Katika wakati wowote ule, tulia(relax) hata kama kuna jambo baya kiasi gani limetokea, usipanick, kwa sababu unapopanik unafanya maamuzi ambayo sio sahihi.
Kuwahamasisha watu wako wawezeshe kutulia hata pale mambo yanapokuwa mabaya. Watapata njia nzuri za kuyatatua.
18. Kama inataka kuwahamasisha wengine, basi acha kuwa muongeaji sana na sikiliza.
Sheria ni hii, acha mtu aongee, acha mtu ajieleze na usimkatishe kwa njia yoyote ile. Unapompa mtu nafasi ya kuongea unajua tatizo hasa ni nini na hivyo kuweza kulifanyia kazi.
19. Wewe kama kiongozi unahitaji kuwa polisi mzuri na polisi mbaya kwa wakati mmoja.
Unakuwa polisi mzuri kwa kuwatia moyo watu wako, kuwaongoza na kuwaonesha kwamba wanaweza.
Unakuwa polisi mbaya kwa kuhakikisha watu wanatimiza walichoahidi, wanatekeleza majukumu yao na kutokubali sababu ambazo sio za msingi.
20. Timiza ahadi zote unazotoa kwa watu wako. Hata kama ni ahadi mdogo kiasi gani, itimize.
Watu wanahamasishwa zaidi na wewe kama utakuwa mtu wa kutekeleza ahadi zako.
Ila kama utakuwa muongeaji na sio mtekelezaji, na wao wataona ni sawa kuongea na kutokufanya.
Yafanyie kazi mambo haya na kazi yako, biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla yatabadilika sana.