Unapoyafikiria maisha yako, kuna picha ambayo unaiona.

Unapofikiria siku zinazokuja, kwenye kazi yako, biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla, kuna taswira ambayo huwa inakujia kwenye akili yako.

TASWIRA UNAYOJIJENGEA KWENYE AKILI YAKO NDIO INAYOTOKEA KWENYE MAISHA YAKO.
TASWIRA UNAYOJIJENGEA KWENYE AKILI YAKO NDIO INAYOTOKEA KWENYE MAISHA YAKO.

Mara nyingi taswira hii huwa ni hasi, kujiona umefukuzwa kazi, au kazi inazidi kuwa ngumu na huku kipato hakitoshelezi.

Au kujiona unafanya biashara ambayo haina wateja, au washindani ni wengi na biashara yako haiendi vizuri.

Au unayaona maisha yako yako hovyo sana, mwenza wako amekuacha, ndugu zako wamekutenga na hata wale uliokuwa unawaamini wamekusaliti.

Yote hayo hakuna hata moja ambalo tayari limeshatokea, lakini unajua nini, akili yako inatengeneza taswira hizi, tena mara nyingi kutokana na hofu. Na kinachotokea ni kwamba akili yako ya ndani(subconscious mind) inatengeneza mazingira ambayo yataleta kile ambacho unafikiria kwa muda mrefu.

Ndio maana baada ya muda utasema, nilijua tu, lazima watanifukuza kazi. Nilijua tu lazima ataniacha. Nilijua tu kwamba hii biashara haitanilipa, nitapata hasara. Na mengine mengi.

Wakati unaweza kuona ya kwamba wewe ni mtabiri mzuri, sio, ila akili yako imekuletea kile ambacho umekuwa unafikiri kwa muda mrefu. Hakuna zaidi ya hapo.

SOMA;  Hii Ndio Sababu Kubwa Inayokufanya Ushindwe Kutatua Matatizo Yako.

Ufanye nini sasa?

Badilisha mawazo ambayo unaingiza kwenye kichwa chako, badili taswira ambazo unajaza mawazo yako. Badala ya kuwa na taswira hasi za kushindwa, anza kujijengea taswira chanya na za kushinda. Jione ukiwa mfanyakazi bora sana kwenye kazi unayofanya, jione ukiwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa. Jione ukiwa na mahusiano mazuri sana na wale wote muhimu kwako na wanaokuzunguka. Na akili yako itakutengenezea mazingira hayo.

Naomba unielewe, sijasema ukishajiona una mafanikio basi mafanikio yanakuja, hapana. Hii ni hatua ya kwanza na muhimu, ni lazima uweke kazi ya kutosha kwenye kazi yako, biashara yako na hata mahusiano yako. Tofauti ni kwamba unapojiona unafanikiwa unakuwa na moyo wa kuweka jitihada zaidi na unapojiona unashindwa unakata tamaa ya kuweka jitihada zaidi.

Vyovyote vile, mwenye taswira chanya, mwenye kujiona akifanikiwa, atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa kuliko anayejiona kinyume na hivyo.

Fanya zoezi hili dogo, kila siku unapoamka asubuhi, tulia na jitengenezee taswira ya vile maisha yako unataka yawe. Weka taswira hii kwenye akili yako angalau kwa dakika tano kila siku. Ndio dakika tano tu kila siku, halafu ianze siku yako ukifanyia kazi taswira hiyo. Kama utafanya hivi kila siku kwa miezi mitatu niandikie kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz nieleze ni mabadiliko gani umeyaona kwenye maisha yako.

TAMKO LA LEO;

Najua ile taswira ambayo nimeitengeneza kwenye akili yangu ndio inayotokea kwenye maisha yangu. Mara nyingi nimekuwa najipa taswira ya mambo mabaya, kushindwa na kuanguka na ndio maana nimekuwa napata mambo haya mabaya kwenye maisha yangu. Kuanzia sasa nitakuwa najipa taswira ya mambo mazuri, kushinda na kwenda mbali zaidi. Najua taswira hii chanya ni msingi muhimu kwangu kufikia mafanikio makubwa.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.