Karibu sana rafiki tuendelee kujijengea falsafa mpya ya maisha ambayo tutaishi nayo maisha yetu yote. Falsafa hii itafuata misingi yote ya dunia na hivyo kutuweka kwenye nafasi nzuri sana ya kushinda.

Moja ya vitu ambavyo watu wengi tumekuwa tunajidanganya ni kufikiri kwamba sisi tunaweza kuwa wajanja kuliko dunia yenyewe. Huwa tunafikiri kuna njia tunaweza kuidanganya dunia, tukafanya mbinu na tukanufaika sana kwa kuweka juhudi kidogo.

Leo nataka nikuambie kwamba njia hiyo haipo na kama ipo basi madhara yake ni makubwa sana ukilinganisha na kile ambacho unakitaka. HUWEZI KUIDANGANYA DUNIA, KAMWE HUWEZI NA ACHA KUJIDANGANYA MARA MOJA. Huu ni moja ya msingi muhimu sana wa kila mmoja wetu kujijengea kwenye falsafa hii mpya ya maisha.

Kama utasoma makala hii ya leo, halafu ukaja kutapeliwa basi nitakuwa nimeshindwa kazi yangu ambayo ni kukupatia wewe maarifa.

Dunia ina akili kuliko wewe.

Mara nyingi tunavyofikiria kuidanganya dunia huwa tunaona ya kwamba sisi tuna akili sana kuishinda dunia. Na hivyo tunajaribu kuidanganya. Sasa kabla hujaendelea kufanya hivyo nataka nikukumbushe kwamba hii dunia ina akili nyingi sana kukushinda wewe. Kwanza kabisa dunia hii imekuwepo kwa muda mrefu kuliko watu wote ambao tumewahi kuwepo hapa duniani. Sisi tunapita hapa kwa kipindi kifupi sana, lakini dunia ilikuwepo, ipo na itaendelea kuwepo.

Kama dunia isingekuwa na njia ya kujilinda yenyewe wala sisi tusingeikuta. Kwa sababu kwa mambo yote ambayo tunayasoma tu kwenye historia, kama dunia isingekuwa na njia za kujilinda yenyewe ingeshaangamia zamani sana. Lakini kwa kitendo cha dunia kuendelea kuwepo licha ya kupitia changamoto nyingi ni kidhibitisho tosha kabisa ya kwamba dunia ina ujanja wake yenyewe.

Moja ya njia ambazo tunafikiri tunaweza kuidanganya dunia ni kufikiri ya kwamba tunaweza kupata zaidi kwa juhudi kidogo. Kumekuwa na mitego mingi sana ambayo watu wasiokuwa na falsafa imara ya maisha wanaingia na kunasa. Mitego kwamba kuna njia ya haraka ya kupata utajiri, kwamba kuna njia isiyohitaji kazi ya kutajirika, hii ni mitego iliyonasa watu wengi ambao hawana msingi huu wa falsafa.

Ndio maana nikasema kama utasoma hapa na bado ukaenda kutapeliwa nitakuwa nimeshindwa kazi yangu ya kukushirikisha wewe maarifa ambayo ni muhimu sana kwenye maisha yako.

Hujanielewa vizuri bado?

Ngoja tuanze na DECI, unaikumbuka? Ilikuja kwa umaarufu sana, panda mbegu na uvune. Watu walioneshwa kuna njia rahisi sana ya kupata fedha nyingi. Unachohitaji kufanya wewe ni kupanda mbegu, halafu unatafuta watu wengine nao waje wapande mbegu, halafu utavuna mara tano ya mbegu uliyopanda.

Nakumbuka mwaka 2009 wakati ndio DECI inafikia kileleni nilikuwa nafundisha shule moja ya sekondari na mwalimu mmoja akaja na habari hizo za DECI, aliwakusanya watu kikundi na akawa anawaeleza jinsi ya kupanda na kuvuna. Nakumbuka nilimwambia hicho kitu ni uongo. Lakini aliona kama sijui ninachozungumza, na ukichangia ilikuwa inaendeshwa na viongozi wa kidini basi watu waliona ni kitu sahihi kabisa.

Wakati watu wanaanza kuipigia kelele deci nilipata shauku ya kutaka kuifahamu vizuri zaidi, na hivyo kuanza kutafuta ni nini hasa. Katika kutafuta kwenye mtandao ndio nikajua kwamba ni kitu kinaitwa PYRAMID SCHEME. Sitaeleza sana hilo kwa undani, ila kama unataka usidanganywe tena kwenye amisha yako, tafuta hiko kitu kwenye google na ujifunze zaidi.

Msingi wa dunia ni kwamba, huwezi kuvuna bila ya kupanda, kitu ambacho watu waliambiwa vizuri kwenye DECI, panda laki mbili utavuna milioni. Vizuri sana. Lakini pia msingi huu wa dunia haushii kupanda tu, ni lazima upalilie, ni lazima uweke mbolea, ni lazima uweke maji kama mvua hakuna ndio uweze kuvuna. Kwenye DECI hiki hakikuwepo, ni kupanda na kuvuna tu.

Sasa hebu niambie kwa akili ya kawaida tu, ni nani umewahi kumuona ameenda shambani akapanda mbegu na kuondoka, akarudi siku ya kuvuna na akavuna mazao mengi sana? Hakuna. Lakini sisi tulifikiri tunaweza kuidanganya dunia. Tulifikiri tunaweza kuleta mchezo wa ujanja kwenye fedha na tukatajirika.

Kipato chochote duniani kinatokana na thamani. Huwezi kupata kipato kama hujatoa thamani, na kama ukikipata bila ya kutoa thamani hakitaweza kudumu muda mrefu. Huwezi kuidanganya dunia, acha kupoteza muda wako.

Epuka sana wanaokuambia kuna njia rahisi ya kutajirika.

Katika kujijengea falsafa mpya ya maisha nimeona tuanze na hili kwa sababu kama kuna sehemu ambayo watu wengi wanadanganywa na kujidanganya wenyewe basi ni kwenye swala la fedha. Watu wengi sana wametapeliwa kwenye kazi, biashara na hata fedha zao binafsi. Wamekuwa wakitapeliwa kutokana na tamaa zao za kufikiri kwamba wanaweza kupata zaidi bila ya kuweka kazi zaidi au kutoa thamani zaidi. Mwisho wake wanajikuta kwenye wakati mgumu wakiwa wamepoteza fedha na muda wao pia.

Ukisikia mtu anakuambia kuna njia hii hapa inakuletea utajiri haraka sana. Kabla hata hujamjibu chochote jiulize ni thamani gani unayokwenda kutoa, ni kazi gani unakwenda kuweka. Kama hakuna basi usimjibu chochote, kimbia haraka sana na endelea kufanya kile ambacho unafanya na kinakuingizia kipato. Nimekuwa naona watu wengi wanaanzia chini na kuweka juhudi sana, halafu wanafika hatua fulani wanadanganyika na kufikiri wanaweza kuizidi ujanja dunia. Ni jambo la kusikitisha sana. Ndio maana sitaki wewe uingie kwenye mtego huu.

SOMA; Kauli KUMI Za Marcus Aurelius Zitakazokufanya Uyaone Maisha Kwa Utofauti.

Kungekuwa na njia rahisi ya kupata fedha hivi unafikiri ni nani hapa duniani angetaka kuteseka? Kila mtu si angekimbilia njia hiyo na akapata fedha? Lakini njia hiyo hakuna ndio maana dunia nzima watu wakakazana kufanya kazi, wanakazana kuboresha zaidi. Na hii ndio inafanya dunia kuwa sehemu nzuri sana ya kuishi.

Lakini pamoja na hili, bado watu wamekuwa wakifikiri labda wao wana akili sana kuliko wale ambao wanafanya kazi kwa juhudi. Hufikiri kwamba wao ndio wamegundua njia rahisi ya kupata kipato, wengine hawajastuka bado. Huwa tunajidanganya sana.

Ngoja nimalize na mfano mwingine ambao ulitokea siku sio nyingi. Mwanzoni mwa mwaka 2014 kuna biashara mpya iliingia hapa Tanzania ambayo ilikuwa inafanywa kwa njia ya mtandao(network marketing). Nimewahi kufanya biashara hizi za mtandao na hivyo najua misingi yake iko wapi(huwa siingii kwneye kitu chochote bila ya kuijua misingi kwanza). Sasa ikawa imekuja hiyo mpya na ya kipekee, inatumia mtindo wa biashara ya mtandao ila yenyewe ilikuwa ya kitapeli.

Sasa ilipoanza kushamiri hapa Dar, watu wengi walinitafuta wakiniambia kuna fursa mpya imeingia. Nilikutana na rafiki yangu ambaye amekuwepo kwneye biashara za aina hii kwa muda mrefu na akanieleza mpango wa biashara hii. Alipofika mwisho nikawa nimeshaona mtego ulipo ambapo wao hawakuwa wameuona. Nilimuuliza maswali kuhusu mtego ule niliouona lakini aliyajibu kulingana na uelewa wake. Akanialika kwenye mkutano ambapo fursa hiyo ilikuwa inajadiliwa. Swali lile lile ambalo nilimuuliza rafiki yangu liliulizwa tena kwenye mkutano ule, na kiongozi aliyekuwa akiendesha ule mkutano alilijibu kwa jibu ambalo liliashiria kwamba wao walioiona ile fursa ni wajanja sana kuliko wengine. Alijibu kwamba, tatizo watanzania mnapenda muone kazi ngumu ndio muamini, sasa hivi mambo yamebadilika. Niliondoka kwenye mkutano ule nikiwa na azimio kwamba sitafanya ile biashara na nilimwambia rafiki yangu akishazikamata fedha zinazotokana na biashara hiyo kwenye mikono yake ndio tuongee tena. Muda haukupita sana, serikali ilikuja kufunga biashara ile. Mpaka leo wanaamini serikali ilifunga kimakosa, kama ambavyo walioingia kwenye DECI wanavyoamini kwamba serikali ndio haikuwaelewa mchezo wao unakwendaje.

Nimalize kwa kusema kwamba dunia ina akili sana kuliko wewe, dunia imeweza kupita vipindi vingi mpaka kufika sasa. Usifikiri kwa njia yoyote ile unaweza kuidanganya dunia. Na linapokuja swala la fedha, epuka sana tamaa inayoletwa na fikra kwamba unaweza kuidanganya misingi ya dunia, utapoteza muda wako bure.

Huu ulikuwa moja ya misingi muhimu sana katika kujijenga falsafa mpya ya maisha, ili usiendelee kuyumbishwa na kupoteza muda na fedha. Wiki ijayo tutaangalia baadhi ya sheria za asili ambazo huwezi kuzikwepa, na unapojaribu kuzikwepa unakutana na changamoto nyingi sana.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz