Kadiri unavyofanya maamuzi mengi ndivyo unavyochosha utashi wako na hivyo kushindwa kufanya mambo ya msingi.

Kila siku unapoamka asubuhi utashi wako unakuwa kwenye viwango vya juu sana. Lakini kila unapoanza kutumia utashi huu kufanya maamuzi unaupunguza na hatimaye kuchoka kabisa.

KADIRI UNAVYOFANYA MAAMUZI MENGI NDIVYO UNAVYOCHOSHA UWEZO WAKO WA KUTENDA.
KADIRI UNAVYOFANYA MAAMUZI MENGI NDIVYO UNAVYOCHOSHA UWEZO WAKO WA KUTENDA.

Unaweza kufananisha utashi huu na simu, hasa hizi smartphone. Chukua mfano kwamba kila siku unapoingia tu kulala, unaweka simu yako kwenye chaji. Ukiamka inasoma chaji asilimia 100. Sasa unapoitoa pale kwenye chaji na kuanza kufungua vitu vingi, mfano kwa wakati mmoja unafungua facebook, wasap, instagram, unajibu ujumbe, unapiga na kupokea simu, haitachukua muda utashangaa chaji inapungua sana.

Hivi ndivyo utashi wako unavyopungua kila siku. Unapoamka utashi upo asilimia 100, unapoanza kufanya maamuzi mengi asubuhi, niamke nisiamke, nivae nini, nitumie nini asubuhi hii na mengine mengi, yanachosha utashi na hatimaye unajikuta huna tena nguvu ya kuweza kufanya jambo lolote zuri.

Ili kuondokana na hali hii, hakikisha unafanya maamuzi machache sana, usiwe na ubishani wa maamuzi. Na njia nzuri ya kufanya hivi ni kuwa na ratiba ya vitu utakavyofanya kabla hata hujalala. Ili unapoamka unajua moja kwa moja nitaanza na kitu fulani, halafu kifuate kitu fulani na kuendelea. Hii itakuwezesha kufanya mambo bila kuahirisha.

Kwa mfano kama unataka ukiamka ufanye mazoezi, basi andika kwenye kijitabu chako muda huo unaoamka na kufanya mazoezi, na pia weka nguo zako za mazoezi mahali ambapo ukiamka unachukua na kuvaa. Hii itakuwa rahisi kwako kuamka, kuvaa na kukimbia. Lakini kama hutapanga muda na utakuwa hujui nguo ziko wapi, ukiamka utaanza kufikiria nikimbie sasa hivi au nikimbie baadae, utashi unapungua, unakuja tena sawa nakimbia, nguo ziko wapi, unazidi kupunguza utashi, baada ya muda unasema nitakimbia kesho.

SOMA; Maamuzi Uliyofanya Awali Na Maamuzi Mapya.

Kama wewe ni mwandishi, kabla hujalala panga siku inayofuata utaandika nini na ni muda gani, na siku inapoanza fanya hivyo. Kama utakuwa hujapanga uandike nini, utatumia utashi wako kubishana na wewe mwenyewe kama unachopanga kuandika kiko vizuri.

Punguza idadi ya maamuzi unayofanya na utajipa nafasi kubwa ya kuweza kuyafanya kwa sababu utakuwa na utashi mkubwa.

TAMKO LA LEO;

Nimejua ya kwamba kadiri ninavyofanya maamuzi mengi ndivyo ninavyochosha utashi wangu na kujiweka kwenye nafasi ya kutokutekeleza maamuzi hayo. Kuanzia sasa nitakuwa napanga mipango yangu kabla ya siku ya kuitekeleza ili siku inapofika naanza kufanyia kazi, badala ya kuanza kubishana mwenyewe kama nifanye au la. Najua utashi wangu ni muhimu sana katika kufikia mafanikio, nitautumia vizuri badala ya kuacha upotee kwa kufanya maamuzi yasiyo ya msingi.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.