Asilimia 99.99 ya wasomaji wa makala ninazoandika ni watu ambao hatukujuana hapo awali.
Sasa nikuulize wewe, ulijuaje hii mitandao ambapo ndipo naandika makala za kufundisha?
Kwa sehemu kubwa sana ni kwamba ulikuwa unatafuta mafunzo haya, ulikuwa unatafuta sehemu ambapo unaweza kujifunza na kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa kwa wakati huo.
Na wakati huo ambapo wewe unatafuta yalipo mafunzo mazuri, mimi nilikuwa na mafunzo na nilikuwa natafuta mtu ambaye anaweza kuyahitaji. Hivyo wote wawili tulikuwa tunatafutana.

Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba yeyote unayemtafuta, na yeye anakutafuta wewe. Chochote unachotafuta, na chenyewe kinakutafuta wewe. Ndivyo sheria ya asili ilivyo.
Kama hiyo ni kweli, kwa nini kuna vitu natafuta kwa muda mrefu sivipati?
Jibu ni kwa sababu unatafuta sehemu ambazo sio zenyewe. Kama ungekuwa unatafuta mafunzo kama haya unayopata sasa, halafu ukawa unayatafuta kwenye magazeti au blogu za udaku ungeyapata?
Ni dhahiri usingeweza kuyapata, hivyo chochote unachotafuta, na chenyewe pia kinakutafuta, ila una kazi moja kubwa ambayo ni kutafuta kwenye eneo sahihi.
SOMA; Hiki Ndio Kinachokuzuia Wewe Kupata Kile Unachotaka Kwenye Maisha Yako.
Ndio maana utasema mimi natafuta fedha, lakini mbona sioni zenyewe zikinitafuta? Kama unataka kuona fedha zinakutafuta, anza kuweka ubora wa tofauti kabisa kwenye kazi au biashara ambayo unaifanya, na utaona jinsi ambavyo fedha zinakukimbilia.
Lakini watu hawazitafuti fedha sehemu sahihi kwa kuongeza thamani ya kile wanachotoa, wanatafuta fedha kwa kuwa na malalamiko. Fedha inawasubiri kwenye thamani wao wanaitafuta kwenye malalamiko. Sasa hebu niambie wataipata hapo?
TAMKO LA LEO;
Nimejua ya kwamba kitu chochote ambacho nakitafuta, na chenyewe kinanitafuta, na mtu yeyote ambaye ninamtafuta, na yeye ananitafuta mimi. Jukumu langu ni kwenda sehemu sahihi ya mtu au kitu hiko kinakoweza kupatikana na pale tutakutana na mambo yatakuwa mazuri sana. Kama natafuta fedha zaidi na zenyewe zinanitafuta, ni mimi kuongeza ubora na thamani ya kile ambacho ninatoa, na fedha zitaongezeka mara dufu.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.