Kuwa bora ni vita kali sana, kwa sababu kila kinachokuzunguka kinakulazimisha kuwa kawaida.
Kuwa tofauti ni vita kali sana, kwa sababu kila mtu anategemea uwe kama wengine walivyo.
Kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako ni vita kuu kuliko zote utakazokuja kupigana kwenye maisha yako.

Vita hii itaanza na wewe binafsi, utapambana na mawazo yako, kuna ambayo yatakuambia inawezekana na nenda. Kuna mengine yatakuambia ya nini kujitesa na wakati maisha yenyewe ni mafupi. Unahitaji kushinda vita hii ndani ya akili yako kwanza.
Halafu unakuja nje ambapo kuna maadui wengine wengi wanakusubiri kwa hamu sana wazigaragaze ndoto zako. Wataanza kukuambia huwezi, haiwezekani, hujui unachofanya, wenzako walijaribu na wakashindwa. Safari inaweza kuishia hapa, ila kama utakuwa na moyo na kuendelea bado vita haijaisha.
Ukiianza safari utakutana na vita nyingine kubwa sana. Hii ni vita ya changamoto, kushindwa. Ni vita ngumu sana na njia pekee ya kuishinda ni kutokukata tamaa, kuwa king’ang’anizi na kuwa mvumilivu. Ni vita ngumu mno na inawashinda wengi. Lakini hata utakaposhinda vita hii bado sio mwisho.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoua Ndoto Zako Kubwa Za Mafanikio.
Ukishafanikiwa kuna vita nyingine kubwa sana, na hii ni vita ya kulewa mafanikio, kuona wewe ndio umeshaweza kila kitu. Hapa unasahau kufanya vile ambavyo vimekufikisha kwenye mafanikio yale na hivyo unaanza kuporomoka kwa kasi kubwa sana. Kushinda vita hii ni kutokubweteka na mafanikio yoyote yale, hata yanapokuwa makubwa kiasi gani. Wewe endelea kuweka juhudi bila ya kujali umefikia kiwango gani. Endelea kuwa tofauti kila siku.
Hii ni vita kali sana ambayo haina mwisho, ni ngumu na ukizubaa kidogo tu inakumaliza. Unahitaji kujitoa sana na kuwa tayari kufanya lolote ili usiondolewe kwenye njia hiyo uliyochagua.
Kama watu 100 watapanga kufikia mafanikio, hivi ndivyo vita hii kali itakavyowapangua;
50 watashindwa kwenye vita vya ndani ya akili zao wenyewe. Wataona haina maana na ni bora kuendelea kuwa kawaida. Wanabaki 50.
30 watashindwa kwenye vita ya kukatishwa tamaa na wengine. Hawa watakubaliana na maneno ya kutisha watakayoambiwa na hawatachukua hatua. Wanabaki 20.
15 wanashindwa kwenye vita ya changamoto na ugumu wa safari. Wanakata tamaa wakiwa wameshainza safari. Wanabaki 5.
4 wanashindwa kwenye vita ya kulewa mafanikio. Wanakazana sana na kufikia mafanikio ila baada ya hapo wanapoteza au wanashindwa kukua zaidi. Anabaki 1.
1 ndio anafikia mafanikio ya kweli na anakuwa ameshinda vita zote.
Nina hakika huyu mmoja ndio wewe kwa sababu kuna watu 99 wanaokuzunguka hawapati maarifa unayopata wewe.
TAMKO LANGU;
Najua kufanya jambo lolote kubwa kwenye maisha yangu ni vita kubwa na kali sana. Sio lele mama kwamba nikishajua ninachotaka basi ninakipata. Kuna gharama kubwa ya kulipa, kuna vikwazo vingi vya kuvuka ndio niweze kufikia ninachotaka. Mimi nimejipanga kwa vita hii kali na hakuna kitakachonizuia kufika pale nilipopanga kufika.
NENO LA LEO.
Success is not final, failure is not fatal: it is the courage to continue that counts.
Winston Churchill
Mafanikio sio mwisho, kushindwa sio kiama: ni ujasiri wa kuendelea ndio unaoleta tofauti.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
Hii Makala ni ya Moto Sanaaa…. Kila neno ni dini,
Hapa Kocha ulikua deep Sanaa..
Naichukua yote Kama ilivyo.
Asante sana.
LikeLike
Kwa hakika maisha yetu yote ni vita. Kila unapopata ushindi mmoja, adui mwingine anaibuka. Ni mapambano mwanzo mwisho, tusichoke.
LikeLike