Usifanye Mabadiliko Kwenye Biashara Yako Pasipo Kumpa Mteja Wako Taarifa.

Habari za leo rafiki na mfuatiliaji wa makala za AMKA MTANZANIA, mimi rafiki yako naendelea vyema kusafisha njia ya kwenda mji uitwao mafanikio, sijajua kwako ni vivyo hivyo ama ni kinyume, ila nina imani tupo pamoja ndio maana umekuwa na hamasa kubwa ya kuingia kwenye mtandao huu kila siku kutaka kujua nini cha kukuongezea ili uendelee kuwa bora zaidi ya jana.
 

WAPE WATEJA TAARIFA.

Kufikia mafanikio lazima upambane, na pambano lolote huwezi kuwa mshindi pasipo kupigana kweli, na kupigana huko ni lazima uwe ulifanya mazoezi vya kutosha hapo kabla. Nasi kama wapiganaji wa kupigania mafanikio ya kweli na ya halali ni lazima tuwe makini na haraka kukabiliana na changamoto na mabadiliko yanayotokea kila siku katika maisha yetu. Tambua kwamba Hatutaweza kuzuia mabadiliko, kujaribu kuzuia mabadiliko ni sawa na mtu anaye jaribu kuzuia mafuriko ya maji kwa mikono, japo mwanzoni utajitahidi kuzuia lakini mwisho utajikuta unazidiwa, hili hatuwezi kukwepa kwa sababu hata maandiko matakatifu yalinena haya kuwa maarifa yataongezeka. Ukiendelea kung’ang’ana na mfumo wa jana halafu dunia imeshahama huko, na lengo lako ukue kiuchumi katika biashara yako, utakuwa umekubali kushindwa kukua na utakuwa mtu uliyekubali kupotezwa kabisa sokoni.
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kupata Mtaji Wa Kuanzia Biashara.
Ni kwamba, kama huna muda wa kutosha kuifuatilia biashara yako kwa umakini na ukaribu zaidi, na hujatengeneza mfumo wowote mzuri wa ufuatiliaji wa soko lako linataka nini kwa wateja wako na utawasaidia nini kwa kero/shida wanayokumbana nayo, umeridhika na faida unayoipata, huna muda wa kukaa chini na kumsikiliza mteja anayekufanya uendelee kudumu sokoni, jiandae kumpoteza mteja huyo kwa kuchukuliwa na mshindani wako wa soko. Hapa ndipo wengi hudhani wamelogwa, na ndipo wengi hufikiri kuna njia ya mkato mshindani wake ameitumia kumnyang’anya wateja wake, kumbe sivyo. Unapokubali kuingia kwenye soko ambapo kila mmoja anamtaka mteja huyo huyo unayemtaka wewe lazima uwe mbunifu na mtu wa kubadilika haraka sana unapogundua njia mpya ya kuendelea kuwavuta zaidi wateja wapya na kuendelea kuwafurahisha wale ambao tayari umewapata. Siku zote mnapofanya biashara ya aina moja, kuna vitu vingi sana mtakuwa mnafanana kiutendaji, kila mmoja kati yenu hatakubali mwenzake ampite kwenye ubunifu wake mpya, maana mteja unayemhitaji wewe tayari mwenzako amemchukua, utafanya nini sasa umpate na wewe na ukimpata utafanyaje aendelee kuwa wako? Lazima uangalie sana uhitaji wa mteja wako kwa wakati husika ili uwe na nguvu ya kukabiliana na mabadiliko mapya. Unajiuliza sasa hiyo nguvu gani ambayo siwezi kuwa nayo? upo sawa kabisa, nguvu ninayoizungumzia hapa ni ule uwezo wa kupokea jambo jipya na la ghafla linalohusu kuboresha huduma yako na kukabiliana nalo kwa vitendo pasipo kuchelewa.
Je unapofika kwenye kipindi hichi cha mabadiliko huwa unamkumbuka mteja wako kwa kumweleza hali halisi kwa kile unachotaka kufanya kumboreshea bidhaa anayopenda kuitumia au huwa unafanya mabadiliko kimyakimya?, mteja anajikuta tu anapata changamoto kubwa katika upatikanaji wa bidhaa/huduma yako, unapoona wateja wamechukua hatua ya kukufikishia malalamiko ya moja kwa moja, tayari hiyo ni ishara ya kuonyesha kumkera mteja wako, tayari hiyo inaonyesha hutambui thamani ya mteja wako. Kufanya hivi kwa mteja unaonyesha tafsiri ya kutoelewa unachofanya, na kutokujua mchango wake kwako, hii ina mfanya aanze kutafuta sehemu nyingine ya kumjali na kumsaidia tatizo lake zaidi, bahati nzuri na si mbaya huko katika kutafuta kwake msaada/suluhisho anakutana na mshindani wako anaonyesha kuumia kwa kile ulichomfanyia na akaonyesha kumsaidia na kuondokana na shida yake kabisa, wakati mteja ana hofu/mashaka ya kupatwa na tatizo lile lile alilokutana nalo kwako atafanya kujaribu bidhaa ya mpinzani wako, kitendo cha kujaribu tu akapata huduma ya uhakika kwa mpinzani wako hapo utakuwa umempa mteja wako mkono wa kwaheri. Elewa kwamba dunia ya sasa sio kama ya zama mawe/chuma sasa hivi mambo yote ni digital(kisasa zaidi) yaani kitu unachokihitaji kwangu yupo mwingine na mwingine anayo sasa inakuja mimi natoaje na mwingine anatoaje hapo ndipo mteja hupima kwa kujaribu.
SOMA; HII HAPA NDIO BIASHARA INAYOLIPA
Unachotakiwa kufanya ni kwamba, usifanye mabadiliko yeyote yanayomgusa mteja wako moja kwa moja pasipo kumjulisha siku moja/mbili/tatu kabla, usiseme mbona mambo mengine hutokea ghafla sawa lakini lazima uwe na njia ya pili kumsaidia mteja wako huku unamweleza kilichotekea, kama itashindikana kabisa jitahidi kumfanya hakupoteza muda wake kwako na hakupoteza sana kile alichokihitaji kwenye huduma yako, hapa unaweza kumpa ofa ya kumjali ama punguzo la huduma/ bidhaa yako unayoitoa kwake, hii itamfanya ajisikie vizuri kwa kuona unamjali na atasahau hata machungu aliyoyapata hapo nyuma, elewa sisi binadamu hatutaepuka kutokosea/kukosewa na wengine, sasa inapotokea aliyekukosea akaja kukuomba msamaha kwa ulilomfanyia akakiri kutorudia kosa kama hilo tena, yeye ni binadamu atakuelewa tu hata asipokuelewa kwa muda huo.
Mwisho nikukumbushe tena, usifanye mabadiliko kimya kimya pasipo mteja wako kujua, usifunge ofisi yako pasipo kuwajulisha wateja wako, usihame ghafla bila kuwapa wateja wako taarifa ulipohamia, usibadili mawasiliano yako bila kuwaambia wateja wako, chochote kile unachoona kabisa kitamgusa mteja wako na kitamletea kero pale utakapokaa kimya bila kumjulisha usikubali kufanya uzembe huo, kuwa na njia nzuri na rahisi ya kuwajulisha wateja wako kwa pamoja.

Makala hii imeandikwa na rafiki yako Samson Ernest, waweza wasiliana nami kwa njia zifuatazo; piga/wasap 0759808081, samsonaron0@gmail.com pia waweza kusoma makala nzuri zaidi kwa kutembelea www.mtazamowamaisha.blogspot.com.
Asante sana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: