Kuna sehemu ambapo umekuwa unajificha.

Unajificha sehemu hii sio kwa ajili ya kujilinda bali kwa ajili ya kutoroka kufanikiwa, kwa ajili ya kutoroka kufanya mambo makubwa.

Umetafuta sehemu ambayo ukishajificha pale hakuna mtu anayeweza kukulaumu kwamba kwa nini hujafanya mambo makubwa au kwa nini hujatimiza ulichoahidi.

tabia

Wewe mwenyewe umeshafurahia hapo unapojificha, ila leo nataka nikuambie hiyo ni sumu kubwa sana kwa mafanikio yako.

Na kwa bahati mbaya sana unaweza kuwa hujui kwamba unajificha, unaweza kuwa unaona ni maisha ya kawaida tu.

Leo mambo yote yatakuwa hadharani na wewe mwenyewe uamue kama utatoka na uanze kufanya makubwa au utaendelea kujificha.

Sehemu ambayo umekuwa unajificha ni kwenye tabia zako.

Kuna usemi unakwenda, TUNAJENGA TABIA, HALAFU TABIA ZINATUJENGA. Tumekuwa tunatumia tabia ambazo tulijijengea kujificha ili tusifanye mambo makubwa kwenye maisha yako.

SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Unajenga Tabia Za Mafanikio.

Kama umejijengea tabia ya uvivu, pale utakapokazana kuweka juhudi unajikumbusha, lakini mimi ni mvivu, na juhudi zinayeyuka.

Unataka kupata muda mwingi zaidi kwenye kazi zako ili uongeze uzalishaji zaidi, lakini kabla hujaanza hilo unajikumbusha kwamba, mimi ni mlevi, na mpango huo unaisha.

Kuna tabia nyingi sana ambazo zimekuwa zinakurudisha nyuma, umekuwa unatumia hizi kujificha ili usifanye makubwa na kufikia mafanikio makubwa.

TAMKO LANGU;

Najua nimekuwa natumia tabia nilizonazo kujificha ili nisifanye mambo makubwa na kufikia mafanikio makubwa. Kuanzia sasa sitakubali tena tabia ziniongoze, nitaanza ubadili tabia zote ambazo ni kikwazo kwangu kuweza kufikia mafanikio makubwa.

NENO LA LEO.

“First we form habits, then they form us. Conquer your bad habits or they will conquer you.”
Rob Gilbert
kwanza tunazitengeneza tabia, halafu tabia zinatutengeneza sisi. Zishinde tabia zako mbaya la sivyo zitakushinda wewe.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.