Kukosa umakini kwenye vitu ambavyo tunafanya kumekuwa chanzo cha matatizo makubwa sana.

Watu wengi wamepata hasara kubwa, watu wengi wamepoteza maisha yao, watu wengi wamejikuta kwenye hali ngumu kwa sababu tu kuna mtu hakuwa makini kwenye kutimiza majukumu yake.

FANYA KAZI YAKO KWA UMAKINI MKUBWA.
FANYA KAZI YAKO KWA UMAKINI MKUBWA.

Na kwa nini watu hawapo makini kwenye kutimiza majukumu yao?

Kwa sababu akili yao haipo pale kwenye kile kitu wanachofanya. Unafanya kazi lakini akili yako inafikiria vitu vingine. Mwishowe unafanya kazi ambayo ni mbovu sana na mbaya zaidi inakwenda kuwadhuru watu wengine.

Kama kila mtu angeweka akili yake kwenye kile anachofanya na akakifanya kwa umakini mkubwa, tungekuwa na maisha bora sana. Kwa sababu tungekuwa na vitu vilivyo bora sana ambavyo vingerahisisha maisha yetu.

SOMA; Mambo Matano Yatakayokuwezesha Kushirikiana Vizuri Na Watu Kwenye Kazi Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

Kuwa makini unaposikiliza. Mazungumzo yamekuwa yanakosa maana kwa sababu wasikilizaji hawapo makini. Mwenzako anaongea, badala ya kusikiliza kwa makini uelewe anachosema ni nini, wewe akili yako inafikiria umjibu nini. Kwa njia hii mawasiliano yanakuwa sio mazuri na ujumbe uliotakiwa kufika haufiki sawasawa.

Kuwa makini unapozungumza, usiongee tu kwa sababu na wewe unaweza kuongea, na usiongee tu kwa sababu umesukumwa kuongea, kuwa makini kwenye kila neno unalotoa, kila neno linaweza kujenga au kubomoa. Tumia maneno ya kujenga tu.

Umakini ni muhimu sana kwenye kila jambo unalofanya kwenye maisha yako.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba umakini kwenye maisha ni jambo muhimu sana. Kukosa umakini kunaweza kuleta madhara makubwa sana kwenye maisha yangu na ya wanaonizunguka. Kuanzia sasa nitakuwa makini sana kwenye kazi yangu. Nitahakikisha akili yangu yote iko pale kwenye kitu ninachofanya ili nikifanye kwa ubora. Pia nitakuwa nasikiliza kwa makini na hata ninapopata nafasi ya kuongea, nitaongea kwa umakini mkubwa.

NENO LA LEO.

Let us realize that: the privilege to work is a gift, the power to work is a blessing, the love of work is success!

David O. McKay

Tunahitaji kutambua kwamba; nafasi ya kufanya kazi ni zawadi, nguvu ya kufanya kazi ni baraka, na mapenzi kwenye kazi unayofanya ni MAFANIKIO.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.