Je Unachokifanya Kimeshikamana Na Moyo Na Mwili wako?

Unataka kujua kitu gani kinasemwa hapa, kwanza habari za kwako, umeamka salama, kama ni ndio mshukuru Mungu na kama ni hapana pia shukuru maana uzima wako ni uhai wako, mwili unatibika ila uhai ukiondoka hurudishwi. Itumie fursa hii ya pumzi uliyonayo kujiletea mabadiliko ya maisha yako, usiishi kama ulizaliwa kwa bahati mbaya, usiiishi kama haya maisha ni kwa ajili ya watu fulani, usiishi kama yatima aliyekata tamaa, wote tu yatima, unashangaa mimi kukuita yatima? ipo hivi siku unaingia kaburini hakuna wa kukusindikiza hata kama walikuwa wanakupenda zaidi watakusindikiza na udongo mwingi juu yako, huo ndio upendo mkuu kwao kukufanyia hicho kitendo, sasa basi haijalishi umeondokewa na wazazi/mume/mke/watoto unayo nafasi kubwa ya kujiletea mafanikio makubwa zaidi, haijalishi unao wazazi/watoto wote kama hujajua wewe ni nani na hujajitambua unachofanya, unafanya tu ilimradi mkono uende kinywani wewe ni yatima, tena wa fikra.

 
Wengi tunatamani maisha mazuri, hakuna anayependa kuishi maisha mabaya anayoishi sasa, hakuna mtu anayependa kula vibaya, hakuna mtu anayependa kutembea kwa miguu masaa yote eti akisingizia haya ndio mazoezi mazuri, hakuna anayependa kulala sehemu iliyo ya kawaida tu, hakuna anayependa kuwa hivyo alivyo, uchumi wake ndio unamsababisha awe hivyo alivyo lakini kama kila mmoja angepewa yale maisha ya kiwango cha juu aishi naamini asingetamani kurudi kwenye hali yake ya awali, tunajitetea kwa sababu nyingi na kuponda baadhi ya vitu ni kwa sababu tu hatuna uwezo navyo, tunapenda kusema aisee fulani ana matumizi mabaya ya pesa hivi hili gari linavyotumia mafuta ya gharama kubwa kiasi hichi si angenunua tu la kawaida, yaani gari linatumia mafuta sio chini ya elfu hamsini!! je maisha unayoishi unayapenda, naomba ujijibu bila unafiki.
SOMA; Kitu Kimoja Ambacho Wapenda Mafanikio Wote Wanacho Kwa Pamoja.
Hizo zilikuwa ni salamu zangu kwako, tuje kwenye lengo la makala yetu, mara nyingi inatokea tunashindwa kutofautisha walio na kitu cha kufanya yaani ajira na wasio na kitu cha yaani wasio na ajira. Kwa nini nasema hivi, aliye ndani ya ajira analalamika sana na maisha yake ni ya kawaida, ufanyaji kazi wake hauna mfano wa kuigwa, yaani yupo yupo ilimradi kumekucha ameenda kazini, mwisho wa mwezi anapokea mshahara wake maisha yanasonga, miaka inazidi kwenda hana alichofanya, wakati anafikiri hii kazi ninayofanya ni ya muda tu nitapata nyingine nzuri zaidi, wakati anawaza hivyo anaishi ki kawaida na kushindwa kujiwekea akiba kwa sababu nipo kwa muda tu na pesa anayopata anatumia ovyo, kumbuka siku hazingoji mtu, siku inapita, wiki, mwezi, miezi, mwaka, miaka, anajikuta yupo palepale aliposema ni pa muda tu na yule asiye na ajira kabisa anaitamani ile ajira yake, huyu anafikiri nikipata kazi kama ya huyu maisha yangu yatabadilika tu.
Maisha ya namna hii unaona kama vile mchezo fulani hivi usiokuwa na kocha halafu wanaocheza wana maanisha kwa kile wanachofanya, ambapo ni hatari kubwa sana, una weza ukaona wanatumia nguvu nyingi ukaona hawa tayari wana maisha mazuri kumbe wanacheza michezo ambayo hakuna anayeweza kuwaambia ushindi wenu ni mkubwa dunia imeona.
Umewahi kukaa chini ukajiuliza hichi ninachotaka kufanya kimeshikamana na moyo wangu na mwili wangu? Ili inapotokea shida asitokee mmoja wapo akamsaliti mwenzie, unashangaa eeh kuwa moyo na mwili wanasalitiana? ndio wanasalitiana, moyo usipopenda kile unachofanya/unachotaka kufanya itakuletea shida tu pale mwili utakapochoka kwa kuumizwa na vitu mbalimbali na mwili usipokubali kile unafanya itatokea shida pale utakapotumia nguvu kubwa kufanikisha jambo fulani cha kushangaza utafanikisha ila moyo hautokuwa na amani kabisa unaona kama vile ulichokifanya bado hakina maana, ule muda wa kujipongeza kuwa umefanya vizuri hutokuwa nao, hata atokee mtu akwambie umefanya vizuri utaona ni unafiki tu, kwa sababu ndani ya moyo wako kumejaa lawama na manung’uniko ya kutojua thamani iliyozalishwa na mwili wako.
Huu ni ugonjwa unaotesa wengi sana, wengi walianzisha vitu vizuri vyenye kuiletea jamii na dunia kwa ujumla manufaa ya kutosha ila waliishia njiani kwa kutaka tamaa, wengi wapo makazini ila hawafurahii kazi zao kutwa kulalamika, wengi wapo kwenye mahusiano ya ndoa ila hawana furaha nayo, wengi wanafanya biashara ila hawana furaha na biashara zao, wengi ni waandishi wazuri wa makala zenye kuelimisha jamii ila hawana hamasa ndani yao ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na wengine wameacha kabisa kuandika baada ya kukutana na vikwazo mbalimbali, wengi ni watumishi wazuri wa Mungu ila hawatendi sawasawa na wito wao juu ya waumini wao, wengi ni waimbaji wazuri wa nyimbo ila wamebaki watu wa kawaida tu waliochoka ndani mwao, wengi ni wasomi wazuri wenye kuliletea taifa letu mabadiliko makubwa ila hawafanyi hivyo zaidi wanalalamikia tu mishahara, wengi ni wabunifu wazuri ila wamekumbatia ubunifu wao wakifikiri upo muda maalum wa kutumia ujuzi wao, wamepigwa giza la akili wamesahau nguvu aliyonayo sasa na uwezo wa kufikiri vitu kwa kina hautakuwepo miaka mitano ijayo. Haya yote na mengine mengi ambayo sijafanikiwa kukutajia ni vitu ambavyo tumepitwa na wenzetu wazungu, huwa tunafanya vitu ki kawaida sana, tunapenda kugusagusa tu kitu kitokee, hii ni kwa sababu moyo wako na mwili wako hauna ushirikiano, hauna mapatano, ni vita vyako vya ndani kwa  nje, unatumia nguvu kubwa kufikiri na kufanya jambo fulani ukitegemea utapata amani ya moyo wako unashangaa inakuwa kinyume chake.

SOMA; Kama Unafanya Hivi Hakuna Unayemkomoa, Unajikomoa Mwenyewe
Ufanye nini sasa kuepukana na hii hali, jua wewe hutakiwi kuwa hivyo ulivyo, jua uwezo ulioutumia leo kufanya kitu fulani sio kikomo cha kitu ulichonacho ndani na si kipimo cha uwezo wako wa ndani, unachotakiwa kujua upo uwezekano wa kufanya vizuri zaidi na zaidi, uwezo wa jana hufananishwi na uwezo wa leo, ufanisi wako wa jana si ufanisi wako wa leo, ujuzi wako wa jana si ujuzi wa leo, ni zaidi na zaidi ya jana, haya yote unahitaji mawasiliano yako ya mwili na moyo wako, ukishindwa kuelewa hapo basi tumia neno UPENDO, penda kile unafanya kifanye kwa juhudi zote ukijua ndio mwisho wako leo kuonyesha ujuzi wako, kesho tena vivyo hivyo, utashangaa nguvu uliyotumia jana utaona ni ya kawaida sana tena utaanza kujicheka kwa kukosea baadhi ya sehemu hukupaswa kufanya hivyo, hii itakupa hamasa kubwa mno hata ikitokea mwili umechoka sana, hata ikitokea umevunjwa moyo sana, ukipata muda wa kuangalia yale uliyofanya hapo nyuma utapata nguvu nyingine mpya kabisa ni kwa sababu ipo nguvu ya mapatano ndani yako. Chochote kinachofanywa na mwanadamu halafu hakimkosei Mungu kina faida kubwa sana kukuletea mafanikio ya maisha yako, unachotakiwa kufanya ni kuacha kulalamika, penda kuchukua maamuzi ya kile moyo wako umekubali na mwili wako umeitikia kufanya.
Nimalize kwa kukushukuru, umefanya vizuri kutenga muda wako kusoma makala hii, isingeleta maana ya mimi kuandika makala kama hii asisome mtu, hata kama ingekuwa nzuri kiasi gani bado isingeleta umhimu wowote, ni wewe ndio umeifanya ionekane nzuri, nakushukuru sana, naamini umeondoka na kitu cha kufanyia kazi.
Makala hii imeandikwa na rafiki yako Samson Ernest, napatikana kwenye mitandao ya kijamii kwa jina hilohilo pia unaweza tembelea Blog yangu, www.mtazamowamaisha.blogspot.com.
WhatsApp
0759808081, email; samsonaron0@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: