Ngoja nikuambie kitu, maisha ni mazuri sana.
Ila maisha yanakuwa mazuri kama utayaishi kwa viwango vyako mwenyewe.
Kama utaamua kuishi maisha yako kwa viwango vya wengine, maisha yako yanakuwa ya hovyo na yanakuwa maisha ya mashaka.
Njia moja ambayo wengi wanatumia kuishi maisha yao kwa viwango vya wengine ni kujilinganisha na wengine.
Na unapojilinganisha unakuwa kati kati.
Juu yako kunakuwa na watu ambao unaona wamekuzidi kwa vile wanavyofanya au vile walivyo.
Chini yako kunakuwa na watu ambao unaona umewazidi kwa vile unavyofanya au vile ulivyo.
Kama mambo yangekuwa yanaishia hapa bado maisha yangekuwa bora sana. Ila sasa hayaishii hapa. Maisha yanazidi kuwa ya mashaka kutokana na watu hao wawili, watu hao wanakupa hofu kubwa sana.
Walioko juu yako wanakupa hofu kwamba wanapata zaidi yako au huenda wanaweza kukuzuia wewe usipate, au unaweza kuona wana mbinu za kukuacha wewe mbali zaidi. Hivyo unawahofia.
Walioko chini yako wanakupa hofu kwa sababu unaona nao wanakazana ili kukupita wewe. Unaona kama ukizubaa kidogo basi watakupita na kukuacha nyuma. Hili linakupa hofu kubwa sana.
Kwa kujilinganisha na wengine maisha yako yanakuwa ya hofu na mashaka makubwa. Kila mara unafikiria kuna mtu anakuzidi au kukupita, ni maisha ya hovyo sana haya.
Ufanye nini?
Unajua cha kufanya, kimbia mbio zako mwenyewe. Fungua makala hii kusoma zaidi; Hiki Ni Kipimo Kibovu Sana Cha Kupima Mafanikio Yako.
TAMKO LANGU;
Najua maisha ni mazuri sana kama nitaamua kuyaishi kwa vigezo vyangu mwinyewe. Ila kama nitajaribu kuyaishi kwa viwango vya wengine, kujaribu kujilinganisha na wengine, maisha yanakuwa ya hofu na mashaka makubwa kwa sababu wakati wowote naona kuna wengine wananipita. Nimeamua kuishi maisha yangu kwa vigezo vyangu, naweka malengo yangu na kuyafanyia kazi. Najua hakuna anayefanana na mimi, na hivyo hizi ni mbio zangu mwenyewe.
NENO LA LEO.
When you are content to be simply yourself and don’t compare or compete, everybody will respect you.
Lao Tzu
Unapokuwa umeridhika na vile ulivyo na kutokujilinganisha au kushindana, kila mtu atakuheshimu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
