Habari msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu, karibu katika jukwaa hili la kujifunza mambo 20 kutoka kwenye kitabu, makala hizi zinakujia kila wiki. Wiki hii tunakuletea mambo 20 kutoka kwenye kitabu kizuri kinachoitwa How to Act like a CEO (Jinsi ya kutenda kama CEO). Kitabu kimeandikwa na mwandishi D. A. BENTON. 
Kwanza tufahamu nini maana ya neno CEO, neno hili ni kifupisho cha maneno ya kiingereza yaani Chief Executive Officer, ikiwa na maana ya Afisa Mtendaji Mkuu, au wengine wanatumia Mkurugenzi mtendaji (Managing Director). CEO ndiye kiongozi mkuu wa kampuni au shirika, na wapo CEO ambao kampuni ni zao, yaani anakua yeye pia ndiyo mmiliki na mwanzilishi wa kampuni mfano CEO wa Facebook (Mark Zuckerberg) ndiye mwanzilishi na mmiliki wa Facebook. Pia wapo CEO ambao wanaajiriwa kuongoza kampuni, mfano CEO wa Microsoft (Satya Nadella) ni mwajiriwa, lakini mmiliki wa Microsoft ni Bill Gate. Kitabu hiki kinafundisha kanuni ambazo zinatumiwa na CEO ambao ni bora. 
Lakini unaweza kusema huna haja ya kujifunza maana wewe sio CEO, basi nikwambie ukweli, wewe ni CEO sema hujajua tu. Kila mtu ni CEO wa maisha yake, unaweza kua CEO wa familia yako au CEO katika nafasi yeyote unayoiongoza au kusimamia, bila kujali ukubwa au udogo wa nafasi husika. Kanuni namba moja inayotumiwa na CEO ni uadilifu (integrity) na ameielezea vizuri sana, na hakuna anayeweza kukwepa hii kanuni, hata uwe mfanya usafi wa kampuni unaweza kuwa CEO. Lipa gharama kwa kujifunza vile CEO wanavyotenda, jijengee tabia za ma CEO na tenda kama wao. 

Hapa nimekuwekea mambo 20 niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hicho.
Karibu sana
1. Sifa ya kwanza ya CEO ni uadilifu (Integrity), hata kama utakua na akili nyingi, uwezo mkubwa wa kutenda, maono makubwa na uwezo wa kuongoza, ukikosa uadilifu tu yote hayo hayana maana. Popote pale uadilifu ndio nguzo muhimu sana, na ndiyo maana hata unaona watu wanapiga kelele kuhusu kuwepo kwa tume ya maadili ya viongozi, wengine wakisema iliyopo haina uwezo wa kufanya kazi yake vizuri na wakipendekeza kwenye katiba mpya kamati ya kusimamia maadili ya viongozi inapaswa kupewa meno zaidi ili iweze kuwashughulikia viongozi waliokosa maadili. Kama utakumbuka hata katika chama cha mapinduzi kilipopitia hatua ya kuwapata wagombea wake wa uraisi, kwa mujibu wa taarifa ni kwamba kamati yao ya maadili iliwaondoa baadhi ya wagombea kwa kukosa maadili.
2. CEO wazuri hua wanakua wamefanya mazoezi ya kutosha kabla ya kufika kwenye hiyo nafasi ya CEO. Watu wanatamani kua CEO lakini hawako tayari kulipa gharama ya kufanya mazoezi kabla, wanakwambia watajifunza wakifika pale, kitu ambacho kinawagharimu wote wanaofika pale bila kua na mazoezi ya kutosha kabla. Ili uwe CEO mzuri wa kesho, ni lazima uanze kujifunza leo. Tambua kazi za CEO ni zipi, kisha anza kutenda sawasawa na CEO. Hata kama cheo chako ni kidogo katika kampuni, usijalishwe na hilo, kua CEO hakuamuliwi na cheo ulichonacho, bali ni sifa anazopaswa kua nazo CEO unazo? Unaweza kutenda sawasawa na CEO?. Ukianza kujifunza, yaani moja kwa moja utajikuta unapanda vyeo tu, maana utakua unatenda kwa utofauti na kwa viwango vya juu. Sasa acha kulalamika kwamba hupandishwi cheo na mshahara ni mdogo, bali jifunze vitu vinavyofanywa na mtu wa nafasi unayotaka, halafu anza kufanya kama ndio tayari umeshapata, utaongeza thamani yako na lazima utatambuliwa tu. Kuna mwanamama mmoja wa China (Juliet Wu Shihong) ambaye ni CEO kabla ya kufika hapo alikua yeye ni mfanya usafi wa kampuni, kuna wakati hadi walinzi walikua wanagoma kumfungulia kuingia ndani maana alionekana mchafu na haendani na hadhi ya watu wa huko kwenye kampuni. Siku hiyo alijisikia vibaya sana kudhalilishwa huko, lakini aliichukua hiyo kama changamoto akaanza kujiongeza, kila siku akawa anajifunza vitu vipya, anakua wa kwanza kuingia kazini na wa mwisho kutoka, thamani yake iliiongezeka na akapanda vyeo kadhaa, na leo hii yeye ni CEO
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kujijengea Nidhamu Ya Fedha Na Kuifanya Ikuzalishie Zaidi.
3. Ili kua mzuri au vizuri jifunze kwa watu wazuri .Tafuta mentors ambao wana mafanikio unayotamani na wewe uyafikie, hata kama biashara wanayofanya haifanani na ile unayotaka kufanya, lakini utajifunza na kutumia kanuni walizotumia kufikia hapo walipo.
4. Jiwekee viwango vyako binafsi vya mwenendo (behavior). Hakikisha unaishi kulingana na viwango ulivyojiwekea. Wafundishe wale wanaopenda kufuata viwango vyako. Na wakati unawafundisha tambua kwamba sio kila mtu yuko kama wewe, kiuhalisia ni kwamba mtazamo wao unaweza kua tofauti na mtazamo wako.
5. Watu watakufuata kwa sababu ya tabia yako na sio kwa sababu ya cheo chako cha kazi. Njia rahisi ya kupoteza uongozi wako ni kuikosa tabia ya uadilifu, watu wakigundua kama wewe sio mwadilifu hawawezi kukufuata. Hivyo tambua kwamba tabia yako {hasa ya uadilifu} ndiyo inayovuta watu.
6. CEO ni mtu wa mfano (role model). Ili uweze kuonyesha uadilifu wako, ni lazima uonyeshe kwa vitendo na wala sio kwa kusema tu. Na mfano mmoja wapo ni kufanya kile ambacho ungetegemea watu wako wakifanye. Maana ukumbuke ukiwa kwenye cheo hicho cha CEO una watu wengi unaowaongoza kwenye kampuni, sasa ukishindwa kufanya yale unayoyahubiri, ni ngumu sana watu wako kuyafuata. Maana watasema bosi mwenye yamemshinda sembuse sisi. Fanya kwa matendo zaidi.
7. Ukiwa mwadilifu watu wazuri watapenda kufanya kazi na wewe. Katika biashara watu waadilifu ni wachache sana, kuna ujanjaujanja mwingi sana, ndio maana kuaminiana kwenye biashara inakua ngumu sana. Hii ni fursa kwako, maana ukiwa mwadilifu lazima utatambulika tu, na watu waadilifu watapenda kufanya kazi na wewe.
8. Ili maisha yawe na maana lazima upate changamoto. Maisha yasiokua na kikwazo chochote hayana ladha. Ukibahatika kukutana na mtu mzee ukajaribu kuomba akusimulie safari ya maisha, katika vitu atakavyokua anakusimulia ni jinsi alivyokutana na changamoto akazivuka. Hata mjasiriamali yeyote yule aliyefanikiwa katika historia yake vitu vitakavyogusa watu ni changamoto alizokutana nazo na kuweza kuzivuka. Hua inaridhisha (satisfy) unaposhinda changamoto au kikwazo na inakupa uimara kwa wakati mwingine. Ukivuka changamoto huwezi kua sawa na awali. Hivyo furahia pindi unapokumbana na changamoto.
9. CEO ni lazima uwe na maono (Vision), na hili ni hitaji la msingi. Vision ndiyo inayotoa mwongozo wa wapi kampuni inatakiwa kufika. Ili vision yako iwe na maana ni lazima iweze kuwaongoza watu kwenye matokeo makubwa au mabadiliko makubwa. La sivyo hutapata matokeo yeyote na huenda ikakuwia vigumu sana kuwasaidia watu kupata picha itakayowawezesha kufikia hiyo Vision. Vision isiyoonyesha utofauti mkubwa wa sasa na kule kwenye hatima yenu, inafanya wale unaowaongoza kukosa hamasa ya kazi.
10. Baada ya kutengeneza Vision yako, au ya kampuni unayoongoza, hakikisha unawashirikisha wengine. Wafanya kazi wanapaswa waielewe vyema. Hakikisha unairudia rudia kwao mpaka imewakaa kichwani. Lakini pia Vision inaweza kubadilika kwa kadri ya uhitaji, marekebisho yoyote yawe shirikishi. Itakua vizuri kabla Vision haujaanza kuitekeleza uwapatie wale unaowaongoza waipitie kama kuna maboresho wanaweza kuweka. Wakishiriki katika maboresho au utengenezaji wa Vision kuna faida mbili muhimu, kwanza wataelewa vizuri ni wapi kampuni inatakiwa kufika maana wameshiriki, Pili hutatumia nguvu nyingi kwenye utekelezaji kwakua wenyewe watakua na hamasa maana watakua wakijihisi wao ndio wamiliki wa Vision, na watataka kuona kitu walichokiunda wanakifikia.
11. Wapatie watu taarifa kwa kuzingatia jinsi wao wanavyopenda kuzipokea na sio kama jinsi wewe unavyopenda kuzitoa. Bila kujali dhamira yako njema katika kutoa taarifa hizo wale wanaozipokea wataelewa ndivyo sivyo. Ndio maana ni muhimu kujifunza watu wako wanapenda kupokeaje taarifa, fanya kila uwezalo kufikiri njia mbalimbali ambazo ukifikisha ujumbe watu watauchukua kwa usahihi. Katika hizo chagua njia nzuri zaidi, halafu sikilizia majibu yao kwa ajili ya kufanya tathimini wamepokeaje. Don’t assume you know. Ask how they interpreted what you said.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
12. CEO unapaswa kuzungukwa na watu ambao ni wazuri kuliko wewe. Kama kiongozi wewe kazi yako ni kuhakikisha unafanikisha matokeo kupitia Watu unaofanya nao kazi. CEO huwezi kufanikisha kazi zote wewe mwenyewe. Hivyo ni lazima uwe umezungukwa na watu wazuri kuliko wewe, japo wengi wanahofia kuajiri watu wazuri kuliko wao, labda pengine anaweza kuja kuchukua nafasi yake, hii ni hofu isiyo na msingi wowote. Ukiwa na watu ambao wewe ndiyo mzuri kuliko wao, ina maana huwezi kufika mbali zaidi ya ule uwezo wako. You have to surround yourself with people better than you are—it only makes you look better and do your job easier.
13. Thamini wafanyakazi wako zaidi ya unavyothamini wateja wako. Watendee mema watu wako (wafanyakazi) na wao watawatendea mema wengine mema (wateja). Ukiwatenda mabaya wafanyakazi wako, usitegemee wao wawafanyie mazuri wateja wako. Kumbuka wao ndio wanakutana na wateja wengi kuliko wewe. Haimaanishi kwamba uwe legelege kwao hapana, wapatie majukumu yakutosha na wanapoyatimiza vizuri wapongeze, onyesha unajivunia kuwa nao. Hakikisha unawafanya wafanyakazi wako wajione ni wa muhimu kwenye kampuni yako. Wanapokua na hamasa hivyo hivyo watawahudumia wateja kwa hamasa. To keep good people, you, the CEO, have to appreciate and recognize good action from your people.
14. Kama CEO ni lazima uweze kutambua mahitaji ya msingi ya wafanyakazi wako, hususani wale wanaoripoti kwako moja kwa moja. Kila mmoja anauhitaji wa tofauti, usidhani kwamba wote ni sawa. Wapo ambao wanatafuta usalama wa kazi zao (job security) mpaka wastaafu, wengine wanataka kutambuliwa hadharani (public recognition), wengine wanahitaji kutuzwa fedha, wengine wanataka waonekana wao ni wataalam (expert) wengine wanataka shukrani za kimyakimya (quiet appreciation). Don’t give them what you like or need yourself. Give them what they need.
15. Changamoto kubwa aliyonayo CEO ni kuhakikisha anawafikiria mara kwa mara wafanya kazi wake. Anapaswa kuwa makini sana kwa wale anaowaongoza bila kujali yupo kwenye hali (mood) gani. Hata kama hauko kwenye mood nzuri hupaswi kuwaonyesha wafuasi wako.
16. Ukiwadharau watu unaowaongoza utawapoteza hata kama wanapata maslahi mazuri. Ukiwa kama CEO lazima ujue kwamba pamoja na mshahara mzuri kwa mfanyakazi, unapaswa kuonyesha wafanyakazi wako kwamba wao ni wa muhimu katika kampuni. Ukimdharau anaweza kuvumilia kwa muda fulani, ila akishapata mahali ambapo anathaminiwa hata kama maslahi yanafanana na ya hapo kwako, lazima utampoteza huyo mfanyakazi. Toa maslahi mazuri kwa wafanyakazi na pia wathamini na kuwapa heshima wanayostahili.
17. CEO mwenye ufanisi mzuri hua anatoa ahadi kidogo lakini anatenda zaidi ya vile anapaswa. Ni tofauti na wengine wale ambao wanatoa ahadi chungu nzima (ooh nitafanya hili na lile) lakini utendaji wao ni mdogo sana.
SOMA; USHAURI; Barua Ya Wazi Kwa Wafanyakazi Wote. Maswali Sita Muhimu Ya Kujiuliza.
18. Kuuza (selling) ni moja kati ya ujuzi (skills) tatu muhimu sana ambazo CEO anahitajika awe nazo. Skills nyingine ni kusikiliza (listening) na kuwapatia wengine majukumu (delegating). Kwa wale CEO ambao hawawezi kuuza basi biashara lazima itawashinda tu. Kuuza ni ujuzi namba moja ambao CEO lazima ajue tena sio kwa nadharia tu bali kwa vitendo. Hii ni kwa sababu uuzaji ndio uhai wa kampuni, unapofanya vizuri katika kuuza na mauzo yakaongezeka ina maana ndio ukuaji wa kampuni.
19. Fanya mazoezi makali ukiwa kijana. Kuwa vizuri kimwili ni muhimu sana kwa afya yako. Unapokua kijana ukaona uko vizuri kimwili watu hudhani wataendelea kuwa hivyohivyo, na vijana wengi hawajishughulishi kufanya mazoezi kwa kigezo cha kua vizuri. Ukimwambia kijana kuhusu mazoezi atakwambia atafanyaje mazoezi wakati yuko fiti wala hana uzito uliozidi?. Wengi hudhani kwamba mazoezi ni kwa ajili ya wale waliosogea umri, lakini ni kujidanganya huko. Ujana ndio muda wa kufanya mazoezi tena makali. Kama hujajijengea tabia ya kufanya mazoezi tokea ukiwa kijana unapoanza mazoezi uzeeni huwezi kudumisha kufanya mazoezi na utaona ni mateso sana. Anza kujizoesha kufanya mazoezi ukiwa bado ungali kijana ili kujenga tabia hii na ukifika uzeeni haitakusumbua maana itakua ni tabia iliyojijenga kwa muda.
20. Usijutie wakati ulipita bali badili wakati wako ujao (future). Huwezi kubadili chochote kilichotokea wakati uliopita, kama ulikosea, huwezi kurekebisha ili iwe hukukosea. Unachoweza kufanya ni kubadili maisha yako kuanzia wakati ulionao sasa hivi na wakati ujao. Usitumie muda wako kujutia mambo uliyoyatenda au uliyokutana nayo. Tumia muda wako kufikiria wakati wako ujao, utabadilishaje maisha yako ya kesho yawe mazuri kuliko yaliyopita. Kumbuka kila dakika unayotumia kuwaza na kujutia yaliopita, ndivyo unavyotumia muda vibaya ambao ungeutumia kubadili kesho yako. DON’T REGRET THE PAST, CHANGE THE FUTURE
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com