Sehemu kubwa ya maisha yetu inaendeshwa na tabia, ambazo tumejijengea kwa muda mrefu.
Tabia zinatusaidia tuweze kuweka mawazo yetu kwenye yale mambo ambayo ni muhimu zaidi.
Kwa mfano kila siku unapiga mswaki, lakini sio kwamba kila siku utakuwa kama ndio unaanza. Ukishachukua tu mswaki basi mengine yanafuata kama ulivyozoea.

Tabia ni nzuri sana kwa sababu zinaturahisishia maisha, zinafanya kile ambacho tumezoea kufanya tukifanye kwa haraka badala ya kuwa kama ndio tunajifunza.
Sasa uzuri huu wa tabia unakuja na mzigo wake pia. Tabia ni kikwazo kikubwa sana cha kufikia mafanikio makubwa.
Hii ni kwa sababu watu wengi wameshajijengea tabia ambazo haziendani na mafanikio. Na kuvunja tabia hizi ni kazi kubwa ambayo pia wanaweza kuwa hawapo tayari kuifanya.
Jambo lolote unalofanya na ambalo unataka likufikishe kwenye mafanikio, jiulize je unafanya jambo hilo kwa ubora au unalifanya kwa mazoea. Kama unafanya kwa mazoea tayari umeachwa nyuma na hutaweza kufikia mafanikio makubwa.
SOMA; Sheria 65 Za Mafanikio, Furaha Na Maisha Bora Kutoka Kwa ROMAN.
Usikubali kabisa kuleta mazoea kwenye kazi au biashara yako. fanya kwa ubora wa hali ya juu. Hakikisha kila siku kuna kitu ambacho unaboresha, ambacho kinakufanya uwe mbele zaidi.
Tabia ni nzuri kwa mambo ambayo hayahitaji umakini mkubwa, lakini kwa mambo yanayohitaji umakini kama mafanikio, basi usiweke kabisa mazoea.
Kama unafanya kazi au biashara kwa sababu ndio umezoea kufanya hivyo, umechagua njia mbovu sana ambayo haitakufikisha mbali.
Kuwa bora, kuwa tofauti, kila siku.
TAMKO LANGU;
Najua tabia zinaniwezesha kurahisisha sana maisha yangu, kwa kuyafanya mambo niliyozoea kufanya kuwa rahisi. Lakini mimi sitaki kufanya kwa mazoea mambo yale ambayo nataka kufikia mafanikio makubwa. Kila siku nitafanya kwa ubora na kwa utofauti ili niweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yangu. Najua mafanikio hayaji kwa mazoea, bali kwa ubora na utofauti.
NENO LA LEO.
Any business today that embraces the status quo as an operating principle is going to be on a death march.
Howard Schultz
Biashara yoyote ya sasa ambayo inaendelea kufanywa kwa misingi ya mazoea inaelekea kwenye kifo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.