Habari mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema bila kusahau kuwa bora kila siku. Kila siku ni siku mpya kwako katika kufikia mafanikio yoyote yale unahitaji kukua ili uwe bora zaidi ya jana. Karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza kwa nini wafanyakazi wengi wanakosa ufanisi wa kazi katika kazi zao.
Kuna wafanyakazi wa aina mbili ambao wanafanya kazi au wameajiriwa na sekta ya umma yaani serikalini na wafanyakazi ambao wameajiriwa na sekta binafsi. Katika hali ya kawaida wafanyakazi wa serikali na wafanyakazi wa sekta binafsi wapo tofauti sana katika utendaji wao wa kazi. Fanya uchunguzi mwenyewe halafu utaona. Hii ina sababisha hata matokeo yao ya uzalishaji kuwa tofauti sana na kupelekea sekta Fulani kufanya vizuri zaidi na nyingine kuwa na matokeo ya kawaida sana ambayo hayana athari katika ushindani.

 
SOMA; Sehemu Kubwa Ya Watanzania Hatufanyi Kazi, Na Hili Ni Tatizo Kubwa Kwa Maendeleo.
Nini maana ya ufanisi? kulingana na kamusi ya oxford toleo la saba ufanisi ni ubora wa kufanya kitu vizuri bila ya kupoteza muda au fedha. Sasa tuangalie kwa nini watu wanakosa ufanisi kazini?

  1. Hawapendi kazi yao;

Siku zote ukitaka mafanikio fanya kazi unayoipenda ukitaka kufanikiwa fanya kazi unayoipenda utaleta matokeo mazuri sana katika kazi yako. Utaongeza ufanisi katika kazi yako utafanya kazi yako kwa hamasa kubwa toka moyoni, utakuwa bora kila siku ,utakua na furaha na kazi yako. kwa hiyo kufanya kazi ambayo huipendi ni utumwa. Ndio ni utumwa kwa sababu unafanya kitu ambacho hukipendi unafanya tu ili mradi siku ziende yaani bora liende. Watu hawapendi kazi zao wanazofanya ndio maana hawaleti matokeo mazuri yaani wanakosa hamasa na kuwa na ubunifu katika kazi.

  1. Hawapendi kujifunza;

Wafanyakazi wengi hawapendi kujifunza kutokana na mabadiliko. Mabadiliko yalikuwepo, yapo na yataendelea kuwepo hivyo basi huna budi kujifunza kulingana na mabadiliko kama wewe ni mfanyakazi uliyeajiriwa unatakiwa uendane na dunia inavyoenda tuko katika mfumo au zama za taarifa katika dunia bila taarifa una kosa mengi katika dunia ya leo. Kuna watu tokea waingie kazini hawajawahi kujifunza wameridhika na hali waliyonayo wanafanya kazi kimazoea ndio maana kazi zao zina kuwa hazina ubora wa hali ya juu zina kosa ufanisi kabisa. Wengine wanapomaliza mtihani wa mwisho labda katika stashahada, shahada nakadhalika hawajawahi kujifunza tena wakifikiria kwamba elimu waliyoipata vyuoni inatosha kabisa. Unatakiwa kujifunza kwa kusoma vitabu, angalia wenzako wanafanya nini taarifa zipo ni wewe tu ni jinsi gani unaweza kuleta matokeo chanya katika kazi yako. Kuna watu elimu zao za juu zimekuwa hazina matokeo(impact) katika maeneo ya kazi wanabaki kujisifia na vyeti wakati utendaji kazi hakuna kwa namna hii usitegemee kuongezewa mshahara au cheo wakati huna kitu unachoongeza cha ziada yaani huongezi thamani huna athari chanya.
SOMA; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.

  1. Wanapenda kulaumu;

Ukirejea katika maana ya ufanisi ni ubora wa kufanya kitu vizuri bila ya kupoteza muda au fedha. Sasa kama wewe ni mfanyakazi ni mtu wa kulalamika ujue unapoteza rasilimali muda bure. Usilalamike bali chukua hatua stahiki ya tatizo hapo ndio utakua umefanya jambo la maana ukiendelea kulalamika unatengeneza mazingira ya kutokufanya vizuri na unazipoteza fursa pia. Wafanyakazi wengine kazi yao ni kulalamika kwa nini sipandi cheo au kwa nini siongezewi mshahara lakini mbona wenzako wanapanda ni kwa sababu ya kulalamika kwako badala ya kuchukua hatua. Unafanya kitu cha kawaida kila siku halafu unategemea kupandishwa cheo au kuongezewa mshahara? Badilika fanya kitu tofauti ongeza uzalishaji bora weka ufanisi katika kazi yako halafu utaona matunda mazuri yanakuja.

  1. Wanapenda kutimiza majukumu yao kwa shuruti;

Kuna watu kazi yao ni kuambiwa kila kitu akiwa kazini hawezi kufanya kitu mpaka aambiwe au ashurutishwe Fulani fanya hivi ndio unafanya, kwa kufanya hivi huwezi hata siku moja kuleta mabadiliko katika kazi yako mwenyewe mpaka ukumbushwe majukumu yako mwenyewe hii itasababisha kuendelea kuchukia kazi unayoifanya maisha yako yote. Fanya kazi bila shuruti, timiza majukumu yako kwa wakati bila kushurutishwa utaona mabadiliko yanakuja pasipo kufanya hivi usitegemee kupata mabadiliko chanya katika kazi yako.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.

  1. Hawaongezi thamani;

Wafanyakazi wengi wanaangalia sana pesa kuliko thamani wanayotoa. Maisha ya sasa unalipwa kulingana na thamani unayotoa kama hutoi thamani yako usitegemee kupokea pesa ambayo unataka. Ongeza thamani katika kazi yako utapata mabadiliko makubwa sana kama mshahara utaongezewa na cheo utapanda. Usiringe na elimu uliyokuwa nayo hapo ofisini unatakiwa ujiulize kutokana na elimu yako umeongeza thamani gani katika kampuni yako waajiri hawaangalii elimu yako siku hizi wanaangalia unaongeza thamani gani unazalisha nini je una kitu cha ziada? Chukulia mfano wachezaji wa mpira wanasajiliwa na kulipwa kulingana na thamani anayotoa katika klabu yake kama hana mchango anafukuzwa hafai kwa sababu hana athari chanya, hazalishi, hana matokeo chanya. Watu wengi wanapenda kufanya kazi na sekta ambazo haziwabani hii yote ni kukwepa majukumu na dalili ya uvivu katika kazi. Wafanyakazi wanaoongezewa mshahara na kupandishwa cheo ni wale wanaoongeza thamani kubwa katika kampuni au taasisi unatakiwa uwe tegemeo katika kazi yako yaani asipokuwepo fulani lakini kuna wengine hata wasipokuwepo hawana thamani hawaonekani ni wa muhimu.

  1. Hawapendi kufikiri;

Katika kazi ambayo ni nzuri sana na itakulipa ni kufikir, usiache kufikiri hata siku moja. watu wanaoleta matokeo chanya katika dunia hii ya leo ni watu wanaofikiri. Bila kufikiri hakuna mabadiliko unatakiwa kufikiri tofauti ni jinsi gani au kwa namna gani unaweza kuleta faida au matokeo chanya katika kazi yako unawezaje kuboresha, na utatuaje matatizo katika kazi yako na siyo kulalamika? Kuna watu wanafanya vitu kwa kiwango cha chini sana kwa sababu ya kutowajibika katika kufikiri vema. Endelea kufikri kila siku utaleta mabadiliko na utaongeza ufanisi wako katika kazi.
SOMA; Leo Nakuwa Mganga Wako; Kama Una Tabia Hizi Tano Huwezi Kufanikiwa Kamwe.

  1. Wana matumizi mabaya ya muda;

Mtu mwenye matumizi mabaya ya rasilimali muda akiwa kazini hawezi kuongeza ufanisi wowote katika kazi ataishia kuzalisha kazi ambazo hazina viwango bora. Muda mwingi unautumia kwenye vitu ambavyo havina tija kwako kama unautumia vizuri muda na kujua muda una thamani kubwa lazima utafanya kitu cha ufanisi mkubwa. hutoweza kushindana bali utakuwa bora tu utazidisha ubora katika kazi zako na siyo kushindana. Utakuwa mbunifu wa kazi yako na ubunifu ni sanaa ili kitu chako kiwe bora unatakiwa uwe mbunifu mzuri mfano kama wewe ni mwalimu na umetoa kazi kuchora picha kwa wanafunzi halafu katika wanafunzi wote mmoja tu ndio aliweza kuchora na kupaka rangi picha yake na wengine hawajapaka rangi kazi yao je unafikiri kama wewe ni mwalimu utampa yupi alama nzuri? Lazima utampa alama nzuri yule aliyepaka picha yake rangi kwani ameonyesha ubunifu wa hali ya juu sana.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com