Kuna aina mbili za kufanya kazi yoyote ile unayojishughulisha nayo.

Iwe ni kazi ya kuajiriwa, ya kujiajiri, biashara au hata kazi ya sanaa kama muziki au uandishi.

Aina ya kwanza tayari unaijua kwa sababu tumekuwa tunaijadili sana. Aina hii ni kufanya kazi iliyo bora, kuboresha kila siku, kufanya kwa utofauti, kuongeza ubunifu na hatimaye kutopa kilicho bora sana.

Aina ya pili ni kufanya kazi kuepuka kukosolewa. Hapa unafanya kazi kwa kile kiwango ambacho watu hawatakukosoa, au hawatakupinga, au hawatakushangaa, au hawatakuambia una kiherehere, au hawatakuambia unajipendekeza ili uonekane wewe ni zaidi. Hapa ni kufanya kwa viwango vile ambavyo kila mtu anafanya, na kuepuka kuwa tofauti na wengine ili wasikusumbue sana.

Watu wengi hujikuta wakifanya kazi kwa aina ya pili, kwa sababu hawapendi kusumbuliwa. Lakini njia hii ya pili haileti mafanikio, haileti kuridhika na pia inapoteza furaha yako.

Njia pekee kwako mwana mafanikio ni kufanya kazi iliyo bora, iliyo tofauti na yenye thamani kubwa. Ndio watu watakukosoa, ndio watu watakupinga, ndio watu watakushangaa lakini hilo sio tatizo kwako. Na wala usikubali watu hawa wakurudishe nyuma. Endelea kusonga mbele.

SOMA; Sababu Namba Moja Kwa Nini Hufanikiwi Kwenye Kazi Unayofanya.

TAMKO LANGU;

Najua kwamba naweza kufanya kazi yangu kwa njia mbili, njia ya kwanza kufanya kwa ubora na njia ya pili kufanya kuepuka kukosolewa. Najua njia hii ya pili ni njia mbovu sana ya kufanya kazi. Kuanzia sasa ninajitoa kufanya kazi iliyo bora sana, sitojali wengine wanafanya nini, sitojali wengine wananichukuliaje, mimi nimeamua kufanya kazi iliyo bora sana. Hakuna wa kunitoa kwenye hili.

NENO LA LEO.

“To avoid criticism say nothing, do nothing, be nothing.”

― Aristotle

Kuepuka kukosolewa usiseme chochote, usifanye chochote na usiwe chochote.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.