Linapokuja swala la fedha, kuna misingi mitatu muhimu sana kuhusu fedha ambayo kila mtu anatakiwa kuijua.
Msingi wa kwanza ni jinsi ya kutengeneza fedha au kutafuta fedha. Msingi huu wengi kidogo wanaujua. Kila mtu anajua ni kitu gani afanye ili aweze kupata fedha. Japo katika njia hizi kuna ambazo ni za kweli na sahihi na kuna ambazo sio za kweli au sio sahihi.
Msingi wa pili ni kuzitunza fedha baada ya kuzipata. Huu ni msingi muhimu sana ambao umekuwa unawashinda watu wengi. Kwani watu wengi wanapopata fedha hujikuta wakitumia yote mpaka inaisha. Msingi huu ndio muhimu sana kwa ajili ya kufikia utajiri.
Msingi wa tatu ni kuifanya fedha uliyoitunza iweze kukuzalishia fedha zaidi. Hapa ni pale ambapo unapata fedha hata kama umelala na hufanyi kazi. Huu ni msingi muhimu sana na ndio utakaokufikisha na kukufanya uendelee kuwa tajiri.
Kuna watu wengi sana ambao wamepata fedha, tena sio kidogo ni nyingi, na kuwa na maisha bora sana lakini baadae wanapoteza fedha hizo na kuwa na maisha magumu sana na umasikini w akutupwa.
Kwa lengo la kuelewana vizuri kwenye makala hii, naomba nigawe watu wanaopata fedha nyingi kwenye makundi matatu.
Kundi la kwanza ni wale ambao wanapata fedha nyingi kwa wakati mmoja bila ya kuweka juhudi zozote kwenye upatikanaji wa fedha hizo. Kundi hili lina wale ambao wanashinda bahati nasibu na pia tunaweza kuwaweka wale ambao wanaridhi mali kutoka kwa wazazi au walezi wao.
Kundi hili ndio linaongoza kwa kupoteza fedha wanazopata kwa haraka sana. Ni mara nyingi tumekuwa tunasikia mtu anashinda bahati nasibu ya fedha nyingi lakini baada ya mwaka maisha yake yanakuwa magumu kuliko hata yalivyokuwa awali.
Au kwenye urithi unaweza kushangaa mzazi alijinyima na kuweka misingi mizuri, lakini baada ya kufariki na mali kugawanywa kwa watoto baada ya muda mfupi unakuta mali zote zimekwisha, kama ni vitu vinauzwa na watu wanatumia fedha na mwishowe kurudi kwenye hali zao ngumu.
Kundi la pili ni wale wanaopata fedha nyingi kwa wakati mmoja ila wanakuwa wameweka juhudi kwenye kupata fedha hizo. Kundi hili lina wale watu ambao wameweka juhudi kubwa na hatimaye kupata fedha nyingi kwa wakati mfupi. Kwa mfano wasanii ambao wanakuwa wamefanya kazi kubwa na hatimaye kuanza kulipwa kipato kikubwa sana. Au wafanyakazi ambao wanapokea mafao yao baada ya kustaafu.
Kundi hili pia wapo kwenye nafasi kubwa ya kupoteza fedha hizi kwa haraka na kurudi kwenye maisha ya umasikini.
Kila siku tunasikia maisha ya wasanii ambao walikuwa na vipato vikubwa sana lakini baadaye wanaishia kwenye umasikini wa kutupwa. Pia tunasikia habari za wastaafu ambao baada ya kupokea mafao walijikuta wakipoteza fedha zote na kurudi kwenye umasikini.
Kundi la tatu ni wale wanaopata fedha nyingi ila wanazipata kidogo kidogo na kwa muda mrefu. Kundi hili lina wale watu ambao wameanzia chini na kupanda kidogo kidogo. Inaweza kuwa kwenye kazi au biashara, ila wanaanza na kipato kidogo na wanaendelea kuongeza na baada ya miaka mingi wanakuwa na fedha nyingi.
Kundi hili wana uwezekano mdogo sana wa kuishia kuwa masikini kwa muda mfupi. Ila pia wapo ambao wanafanya makosa na kujikuta wanapoteza kila kitu ambacho wamekifanyia kazi kwa muda mrefu.
Ni nini hasa kinasababisha hali hii ya kutoka utajiri mpaka umasikini?
Zipo sababu nyingi zinazopelekea hali hii ya kutoka utajiri mpaka umasikini wa kutupwa. Hapa tutajadili baadhi ya sababu hizo na nyingi zitawalenga wale ambao wanapata fedha nyingi kwa wakati mfupi, iwe wameweka juhudi au la. Japo pia sababu hizi zinaweza kuwahusu wale wanaojenga utajiri wao taratibu.
1. Kufikiri kuwa na fedha nyingi ndio kuwa tajiri.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba ukiwa na fedha nyingi basi wewe ni tajiri. Lakini hili sio kweli, kuwa na fedha nyingi ambazo unatumia na hazizalishi sio utajiri, bali ni umasikini ambao umefunikwa kwa muda.
Kwa kufikiri kwamba fedha nyingi ni sawa na utajiri watu hawa huanza kuiga maisha ya utajiri wasijue kwamba matajiri hawaishi kwa kutegemea fedha walizonazo, bali uwekezaji unaowazalishia.
Kufikiri hivi kumewafanya wale wanaopata fedha nyingi kwa wakati mmoja kurudi kwenye hali yao ya umasikini haraka sana.
2. Kuruhusu matumizi yakue haraka pale kipato kinapokua.
Sababu nyingine kubwa ambayo imekuwa inawafanya watu kurudi kwenye umasikini pale wanapopata fedha nyingi kwa muda mfupi, ni kuruhusu matumizi yakue haraka kuendana na kipato walichonacho sasa.
Kuna kitu kimoja cha ajabu sana kuhusu fedha na matumizi, hata siku moja, fedha haijawahi kukosa matumizi na unaporuhusu matumizi yaongezeke kwa sababu kipato kimeongezeka, yanaongezeka kwa kasi kubwa sana na yanachukua sehemu kubwa ya fedha zako.
3. Kipimo cha fedha kwenye akili kuwa chini.
Sababu nyingine kubwa sana ambayo inawafanya wanaopata fedha nyingi kurudi kwenye umasikini ni kipimo chao cha fedha kwenye akili zao kuwa chini.
Iko hivi kila mmoja wetu ana kipimo chake cha fedha kwenye akili. Kipato unachopata sasa kinaendana na kipimo ulichojiwekea. Na kwa hali hii mipango yako yote ipo kwenye kile kiwango ulichojiwekea kwenye akili yako. kama labda kipato chako ni milioni moja, unaweka hiki kama kipimo kwenye akili yako. hivyo hata mipango yako mingi itakuwa kwenye vipimo ya milioni moja mpaka milioni kumi.
Sasa ikatokea leo umekabidhiwa milioni 100, zinakuwa nyingi sana kulingana na kile kipimo chako, hujawahi kuzifikiria, hujawahi kuzipangia. Kwa fedha hizi nyingi utajikuta unafanya mambo ya ajabu mpaka pale zitakapopungua na kurudi kwenye kile kipimo chako ulichozoea. Hii imekaa kisaikolojia zaidi na inamuathiri kila mtu, japo unaweza usielewe vizuri.
4. Kufanya maamuzi mabovu ya uwekezaji.
Watu wengi hufikiri wakishakuwa na fedha nyingi basi pia wanajua jinsi ya kuziwekeza vizuri, hasa wale ambao wanakuwa wamezipata kwa kipindi kifupi. Kwa hali hii hujikuta wanawekeza kwenye maeneo mabovu na hivyo kupoteza fedha zao.
Nafikiri umewahi kuona watu wengi wanaostaafu, wanapewa mafao yao, wanakwenda kuwekeza kwenye maeneo ambayo hawayajui vizuri na mwishowe kupoteza fedha zao zote. Unashangaa mstaafu anachukua fedha na kwenda kununua gari la biashara ila anaishia kununua gari bovu. Hivyo kila siku inakuwa ni kutengeneza gari na haoni faida.
5. Ndugu, jamaa na marafiki.
Fedha zinavutia watu, na zinavutia watu wazuri na watu wabaya pia. Na wakati ambao mtu ana fedha, huwa anavutia zaidi watu wabaya, wabaya kwa maana kwamba hawana ushauri mzuri kuhusu fedha. Watu hawa wanakuwa wamekuja ili nao wanufaike.
Ndugu nao kwa kujua umepata fedha nyingi basi wanajua matatizo yao yote yameisha na wewe ndio mkombozi. Utegemezi unakuwa mkubwa sana na hili linaweza kumrudisha mtu nyuma.
Jamaa na marafiki ndio usiseme kabisa, karibu kila siku tunasikia hadithi hizi, mtu anakuwa na marafiki wengi anapokuwa na fedha lakini zinapoisha wote wanamkimbia. Siku sio nyingi kuna mtu aliuza nyumba ya urithi hapa dar na alipata fedha nyingi kidogo, alikuwa akitembea na na kundi kubwa la marafiki kwenda bar moja mpaka nyingine, haikuchukua muda fedha ikawa imeisha na akaanza kuuza hata uwekezaji mdogo aliokuwa amefanya.
Uchukue hatua gani ili na wewe usijikute kwenye hali hii?
Wewe kama mwana mafanikio, moja ya malengo yako ni kuwa tajiri na kuendelea kuutunza utajiri huo. Kwa mazingira yanayotuzunguka hii ni kazi ngumu kiasi, lakini sio kwamba haiwezekani. Hapa kuna baadhi ya hatua unazohitaji kuchukua ili na wewe usijekufa masikini licha ya kuwa na kipindi cha utajiri kwenye maisha yako.
1. Pata elimu ya fedha na uwekezaji.
Kuanzia sasa iwe una fedha nyingi au unazo kidogo, elimu ya fedha na uwekezaji ni muhimu sana kwako, ipate kila siku. Jifunze sana kuhusu fedha, jinsi ya kupata zaidi, jinsi ya kutunza vizuri na jinsi ya kuwekeza vizuri.
Kamwe kamwe kamwe usije kuwekeza kwa sababu kila mtu anasema ni uwekezaji mzuri. Usikimbilie kufanya uwekezaji kwa sababu kila mtu anafanya hivyo. Jipe muda na jifunze vizuri kuhusu uwekezaji huo. Tafuta taarifa zaidi, uliza wanaohusika na wanaofanya uwekezaji ule. Jua changamoto za uwekezaji huo. Hakikisha unajiridhisha kwamba unawekeza ukiwa una taarifa za kutosha.
Ndio hii sio rahisi na ndio maana wachache ndio wanaoweza kuendelea kuwa na utajiri baada ya kupata fedha nyingi.
2. Unapopata fedha nyingi, tulia kwanza.
Unapopata fedha nyingi utakuwa na msukumo mkubwa sana wa kuanza kutumia, wa kuanza kununua vitu ambavyo ulikuwa unatamani kwa muda mrefu, wa kuanza kuwekeza kabla hujachelewa, na hapa ndipo unapoingia kwenye mtego mkali na unaokumaliza.
Unapopata fedha nyingi, iwe ni mafao, iwe ni kutokana na kazi au iwe ni urithi, kwanza tulia, iache fedha hiyo ikae kwanza benki huku wewe unafikiria hatua nzuri za kuchukua. Usiwe na haraka, usiwe na papara hakuna unachokosa, hakuna unachochelewa, unahitaji kufanya maamuzi ukiwa umetulia na sio ukiwa unaendeshwa na hisia za fedha hizo.
3. Kwa vyovyote vile, matumizi yako yawe chini ya kipato chako.
Na soma kwa makini hapo, MATUMIZI YAWE CHINI YA KIPATO CHAKO. Ukiwa na milioni mia moja benki kipato chako sio milioni 100, bali kipato chako ni kile unachozalisha kutoka kwenye hiyo milioni 100. Kama fedha hiyo haizalishi kabisa, basi ni bora hata usiitumie, maana unakwenda kupoteza yote.
Hakikisha fedha unayopata inakuzalishia na unachotumia wewe ni ile faida iliyozalishwa, na tena siyo yote kwa sababu unahitaji kuongeza uzalishaji zaidi kutokana na kile ulichozalisha. Yaani kwa kifupi fedha yako inatakiwa izae watoto na hao watoto wazae wajukuu.
Hakikisha matumizi yako yanakuwa chini ya kipato, na kama unataka kuongeza matumizi, ongeza kwanza kipato.
4. Kuwa makini na wale wanaokuzunguka.
Ngoja nikuambie kitu kimoja kuhusu shida za watu, HUWA HAZIISHI, na watu wakishajua una fedha nyingi na wanaweza kupata kiurahisi, watakuja na kila sababu ya kukushawishi wewe uwape fedha. Unahitaji kuwa makini sana na watu wote wanaokuzunguka, ukianza na ndugu zako wa karibu sana. Usiogope kusema hapana kwenye baadhi ya mahitaji yao ambayo unaona siyo ya msingi sana.
Ndio watakuona una roho mbaya, ndio watakuona unawakatalia, lakini ni bora hivyo kuliko wote mkaishia kurudi kwenye umasikini na kushindwa hata kusaidiana kwa yale ya msingi. Wasaidie watu kwenye yale mahitaji ya msingi kweli ambayo unaona hakuna namna.
Unapokuwa na fedha nyingi kila mtu wa karibu atakujia na wazo zuri sana la kuhitaji fedha, lakini wengi hawatakwenda kufanyia kazi kweli, kuwa makini. Nilikuwa naongea na rafiki yangu siku moja kuhusu hili la undugu na fedha akanipa mfano yeye alipomaliza kidato cha sita alikuwa na wazo fulani la biashara, alimwendea mjomba wake aliyekuwa na uwezo na kumweleza mpango mzima. Mjomba wake alimjibu sawa kwamba atampa fedha hiyo na kumwahidi aje kesho yake. Alipofika kesho yake alikuta ameandaa mkataba wa kumkopesha fedha na kumwambia asome na kuweka sahihi yake. Rafiki yangu ananiambia hali ile ilimfanya awe makini sana kwenye matumizi ya fedha zile.
5. Kuza kiwango chako cha fedha kiakili.
Hata kama sasa hivi bado kipato chako ni kidogo, anza kuweka mipango ya vipato vikubwa. Kwa mfano kuwa na mpango wa milioni 10, wa milioni 50, wa milioni 100 na hata wa bilioni moja.
Unachofanya ni hiki, kwenye kitabu chako cha malengo na mipango yako, andika nikiwa na milioni 50 nitafanya yafuatayo, halafu unaorodhesha mambo yote unayopanga kufanya kwa kiwango hiko cha fedha. Kwa kufanya zoezi hili utaanza kujizoesha viwango vikubwa vya fedha na hivyo utakapozipata hutababaika kama ambaye hana mpango kama huo.
Naamini kwa haya machache umepata mwanga kuhusiana na fedha nyingi na kufilisika. Anza kufanyia kazi kile ambacho unaondoka nacho hapa. Nakutakia kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,