Ugumu wa maisha yetu unaanzia kwenye macho ya watu wengine, wale wanaotuzunguka. Hawa wamekuwa chanzo kikubwa kwetu kuwa na maisha ambayo hatuyapendi, kufanya kazi ambazo hatuzipendi na kuwa na vitu ambavyo hatuvifurahii.
Binadamu tunapenda uhuru lakini hatupo huru kwa wale wanaotuzunguka. Huwa tunafungwa na watu hawa, kwa kujikuta tukifanya kile ambacho kila mtu anafanya au kufanya ili kuonekana kwamba na sisi tupo, na sisi tunaweza.
Wakati mwingine hufanyi kwa sababu kila mtu anafanya, bali unafanya ili tu upate ule ufahari wa kuonekana na wengine kwamba unaweza au umefanya. Huu ni mzigo mkubwa sana ambaye hakuna yeyote anayeweza kuubeba, huu ni mzigo ambao umefanya wengi kukimbiza maisha na sio kuyaishi.
Njia moja nzuri ya kuutua mzigo huu ni kujiuliza swali hili muhimu sana;
Kama ningekuwa naishi jangwani mimi na familia yangu tu, hakuna anayenizunguka, je ningefanya haya ninayofanya sasa? Kama jibu ni hapana unaacha mara moja, kama jibu ni ndio unaweka akili, moyo na nguvu zako zote.
Ukishaweza kujitenganisha maisha yako na macho ya wengine, hapo unakuwa umefikia hatua nzuri ya uhuru na sasa unaweza kufikia mafanikio makubwa.
Sikuambii hivi ili uchague kuishi maisha ya hovyo kwa sababu hujali wengine wanafanya nini au wanasema nini, bali nataka wewe uishi yale maisha ambayo ni bora sana kwako. Mwisho wa siku utakachokumbuka ni maisha uliyoishi na sio mashindano uliyofanya.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoua Ndoto Zako Kubwa Za Mafanikio.
TAMKO LANGU;
Najua mambo mengi ninayofanya sasa, kama ningekuwa jangwani peke yangu na familia yangu nisingeyafanya. Nafanya mambo haya kwa msukumo wa wengine kwa sababu nao wanafanya au nataka nionekane. Najua huu ni mzigo mzito sana wa mimi kubeba. Ninahitaji uhuru wa kuishi maisha ambayo yatakuwa bora sana kwangu. Na nitapata uhuru huu kwa kujiuliza swali muhimu kama ningekuwa naishi jangwani, je ningefanya ninachofanya? Kama jibu ni hapana nitaachana nacho, kama jibu ni ndio nitakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.
NENO LA LEO.
Sing like no one is listening.
Love like you’ve never been hurt.
Dance like nobody’s watching,
and live like it’s heaven on earth.
Mark Twain
Imba kama vile hakuna anayekusikiliza.
Penda kama vile hujawahi kuumizwa.
Cheza kama vile hakuna anayekuangalia,
Na ishi kama uko mbinguni hapa duniani.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.