Kuna zawadi bora sana unayoweza kuwapa watu wa karibu yako, watu wanaokuzunguka, ndugu, jamaa na marafiki.
Zawadi hiyo ipo ndani yako wewe na kuweza kuwapa kunafanya maisha yenu wote na hata mahusiano yenu kuwa bora zaidi.
Na zawadi hii bora sana ya kuwapa watu wako wa karibu ni wewe kuwa na maisha bora.
Ndio, wewe kuwa na maisha bora ni zawadi nzuri sana kwa wale wanaokuzunguka, wale walio karibu yako. na sio tu zawadi kwa sababu utawasaidia moja kwa moja, hiyo ni sehemu ndogo sana.
Sehemu kubwa ya zawadi hii iko hapa,
1. Unaacha kuwa mzigo kwao. Ni kweli kwamba hakuna mtu ambaye anapenda kubeba mzigo wa mtu mwingine, kwa sababu tayari mzigo wake pekee unamsumbua. Hivyo unapokuwa na maisha bora, ni zawadi sana kwa wanaokuzunguka. Mnakuwa na mahusiano mazuri na sio tegemezi.
2. Unawapa hamasa pia. Kwa wewe kuwa na maisha bora, mtu ambaye wanakujua, inawapa hamasa kwamba hata wao wanaweza. Wanaona mafanikio sio kwa wachache waliopo sehemu fulani, kwa sababu wewe wa karibu yao unayo, basi hata wao wakikazana wataweza.
Hivyo basi, kuwa na maisha bora, kuwa na mafanikio, sio kwa sababu yako tu, na sio kwa sababu ya kuwasaidia wengine tu, bali pia kuwapunguzia mzigo na pia kuwapa hamasa kwamba hata wao wanaweza.
NENO LA LEO; Kuhusu Zawadi Kubwa Uliyopewa.
TAMKO LANGU;
Kila siku nitahakikisha maisha yangu yanakuwa bora zaidi sio kwa ajili yangu mwenyewe, bali kwa kuwa najua hata wale wanaonizunguka nao wananufaika sana kwa mafanikio yangu. Licha ya kuwasaidia moja kwa moja, ninaacha kuwa mzigo kwao na pia nitawapa hamasa ya wao kuona wanaweza zaidi.
NENO LA LEO.
The greatest gift in life is to be remembered.
Ken Venturi
Zawadi kubwa ya maisha ni kukumbukwa.
Je wewe utakumbukwa kwa lipi?
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.