Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha TIME WARRIOR (Shujaa Wa Muda).

Habari msomaji wa uchambuzi wa vitabu. Ni matumaini yangu waendelea salama. Wiki hii tunaangazia kitabu cha Time Warrior (Shujaa wa Muda). Kitabu hiki kimeandikwa na mwandishi mahiri sana wa vitabu anaitwa Steve Chandler. Mwandishi anaelezea kuhusu Shujaa wa muda ambaye ni mtu anayeweza kushinda vikwazo vya upotezaji wa muda. Pia anaelezea kwamba Kuahirisha mambo ndio kikwazo kikubwa kinachowazuia watu wengi kutokufikia mafanikio. Mwandishi anaelezea vizuri mbinu mbalimbali za jinsi ya kuibuka shujaa wa muda, na kufikia mafanikio. 

 
Karibu sana tujifunze
1. Shujaa hakimbii tatizo, anapita hapo hapo kwenye tatizo. Ili uwe shujaa wa muda (time warrior) lazima upambane na changamoto mbalimbali zinazokupotezea muda. Mfano kama shughuli zisizokua na athari yeyote, vikwazo vinavyokufanya uahirishe mambo mara kwa mara. A warrior does not “get out.” A warrior goes through.
2. Muda unatengenezwa. Watu hufikiri kwamba wako bize na hawawezi kupata muda wa kufanya shughuli fulani muhimu. Utasikia yaani natamani sana kusoma vitabu, ila sina muda. Si kweli kwamba hana muda, ila ni kwamba hajalipa jambo hilo umuhimu wa kutosha. Kwa maana ukilipa umuhimu jambo, tena umuhimu wa kutosha, lazima utalitengenezea muda wa kulifanya. Mfano umepata safari ya nje ya nchi, na safari ni leo, ndege itaondoka saa 7 kamili mchana na muda wa mwisho kuingia uwanjani (check In) ni saa 6 kamili mchana. Halafu saa 5 ndio unatoka nyumbani, ili uwahi airport, wakati unatoka hivi anakuja mtu (ndugu au rafiki) anakwambia analo jambo la muhimu sana na anataka mfanye kikao na wewe kwa muda huo, na kikao kitachukua kama dakika 30 au 40. Je utasubiri mfanye kikao ndio uondoke? Ukweli ni hapana, hilo jambo lake litabidi lisubiri hadi wakati mwingine, maana kuna jambo la muhimu zaidi. Hivyo hivyo, jambo la muhimu lazima litengenezewe muda kama hii safari, ambao shughuli nyingine zinawekwa kando. Ukiona kuna jambo unataka kulifanya na unasema ni la muhimu , halafu hulifanyi kwa kisingizio huna muda, basi ujue, jambo hilo hujalipa umuhimu.
3. Hakuna kitu kinapoteza muda kama kutaka kuwapendeza watu. Maana itabidi uache mambo yako, muda mwingi uutumie kufahamu mambo ya wengine ambayo wanataka wafurahishwe nayo. Yaani mtu yuko tayari kuacha mambo yake ya muhimu katika maisha, ili tu afanye vitu ambavyo atapongezwa na wengine. Sasa ukifanya hivi wewe utaishi lini?
4. Tofauti ya msingi iliyopo kati ya mtu wa kawaida (ordinary man) na Shujaa (warrior) ni kwamba Shujaa yeye anachukulikia kila kitu kama ni changamoto, wakati mtu wa kawaida yeye anachukulia kila kitu aidha kama Baraka au laana.
5. Sio hofu ya kushindwa inayotuzuia kujaribu mambo, bali ni hofu ya kuonekana kushindwa. Kuna mambo mawili hapa. Hofu ya kushindwa na Hofu ya kuonekana kushindwa. Hii ya mwisho ndiyo kizuizi kikubwa cha watu wengi. Watu wanaogopa sana, kuonekana kua wameshindwa. Yaani anajiuliza hivi nikishindwa, jamii itanionaje? Marafiki na ndugu wataniona nimeshindwa. Ndio maana mtu akiwa peke yake, kujaribu haimpi shida, atajaribu hata mara kadhaa, hata kama zote anashindwa. Ila sasa ikifika jambo ambalo litaonekana na dunia (watu) hayupo tayari kujaribu kwa hofu ya kuonekana kushindwa.
SOMA; NJIA KUU TANO ZA KUONGEZA UZALISHAJI WAKO.
6. Hofu ni kama giza, na giza si kitu bali ni ukosefu wa mwanga. Mwanga ni kitu ila giza sio kitu. Ulishawahi kusikia mwendokasi (speed) wa giza?, Lakini mwanga unayo mwendokasi, tena wa haraka sana ambao ni 3 x 108m/ s. Unaweza kuondoa giza kwa kuleta mwanga. Hivyo hivyo hofu sio kitu bali ni ukosefu wa upendo, ukiweza kuleta upendo wa kutosha basi hakuna tena hofu. If you can bring enough love, there is no more fear.
7. Kitendawili cha mabadiliko kwa wengine ni hiki. Watu wanabadilika haraka zaidi, pale panapokua hapana uhitaji wa wao kubadilika. Watu wanabadilika haraka zaidi pale wanapokua wamekamilika. Mfano kama una wafanya kazi wako wawili, mmoja anafanya vizuri na mwingine anafanya vibaya. Yule anayefanya vizuri ni rahisi zaidi kuendelea kubadilika kufanya vizuri zaidi, kuliko Yule mwenye kufanya vibaya kubadilika kuelekea kwenye uzuri, hata kama ataanza kubailika lakini kasi yake itakua ndogo sana, tena anaweza kurudia makosa yaleyale. Hata darasani, mwanafunzi anayepata alama 80 mara kwa mara, ni rahisi kwake kubadilika na kuanza kupata 95, kuliko Yule anayepata 20 kubadilika na kupata 80. Mfano mwingine, kama una mpenzi au mke wako ambaye ni mnene kiasi, na wewe unataka apunguze unene, usimuonyeshe kwamba hufurahii unene wake, au hapendezi na unene wake. Akikuomba ushauri kuhusu kupunguza unene muonyeshe kwamba unampenda hata jinsi alivyo, japo pia akitaka kuanza mazoezi ya kupunguza unene utamuunga mkono, maana atazidi kupendeza zaidi.
8. Kama unayo changamoto zinazoonekana kubwa sana kwako, tafuta kocha (mshauri) mzuri kisha kaa naye chini mwelezee kwa kina hilo tatizo. Halafu wote mtalitazama vizuri hilo tatizo. Sababu kwa nini makocha (wasahuri) wanafanya vizuri sana kwenye kutatua matatizo ya watu, ni kwa sababu kocha hatumii hisia kwenye hilo tatizo bali anatumia akili zaidi. Mwenye tatizo, ni kwamba hisia (emotions) ndio zinakua juu kuliko akili kitu ambacho wakati mwingine kinaweza kuishurutisha akili nini kifanyike, ndio maana unaona mtu kafanya jambo la ajabu sana. Sio akili yake imeamua hivyo bali ni hisia zimetawala akili. Kumbuka suluhisho hapa ni kutafuta kocha mwenye uzoefu wa kukabiliana na changamoto.
9. Tatizo linalowafanya watu wengi kuahirisha mambo, ni kwamba hawaoni uhusiano uliyopo kati ya kumaliza jambo na ile nguvu mpya inayopatikana baada ya kumaliza. Kama wamefika katikati ya shughuli, na kujihisi uchovu, ni rahisi kuiweka pembeni na kusema nitamalizia kesho, wakidhani kwamba wakimalizia leo watachoka zaidi. Kumbe ukimaliza jukumu, kuna nguvu mpya unapata, na unaweza kukabili jukumu lingine kwa ujasiri wa kufanikisha pia.
10. Asilimia kubwa ya watu wanaondoka maofisi wakiwa wamechoka, ujue hawajamaliza majukumu ya siku. Watu wengi wanadhani kwamba wanapoacha shughuli bila kuzimalizia wanafikiri wanaokoa nguvu ambayo wangeitumia kuimalizia hiyo kazi. Hii si kweli, badala yake nguvu ndio zinaisha, hakuna kitu kinamaliza nguvu kama kutokumaliza majukumu yako. Hebu fikiria una majukumu 5 kwa siku, halafu siku inaisha umefanya 2 tu, na hayo mengine umeyaacha nusu nusu hayajakamilika, kitu ambacho utabidi uondoke unayafikiria mara kwa mara, na utajihisi kuchoka akili na mwili. Lakini tena hebu fikiria una majukumu 5 kwa siku yako ya leo, halafu umefanikiwa kuyamaliza yote vizuri. Utajisikiaje? Ni ukweli usiopingika kwamba utajisikia mwenye furaha na mwenye nguvu. Wala uchovu hautausikia.
11. Waathirika (victims) au unaweza kuwaita Wahanga, ni watu ambao wanafikiri sana kuhusu vitu ambavyo wangepaswa kuvifanya ili kuboresha maisha yao, lakini wanadhani kwamba wako bize sana kuvifanya kwa wakati wa sasa. Baada ya muda mfupi tu wanajikita kwenye matatizo yao. Kitu ambacho kinawafanya wazidi kuona matatizo tu. In life, what you focus on grows.
SOMA; Tumia Muda Huu Mchache Kufanya Mabadiliko Makubwa Na Endelevu Katika Maisha Yako.
12. Ubongo wa Mwanadamu ni kompyuta ya ajabu sana. Kompyuta hii inatupatia nguvu pale tunapoipatia kitu fulani cha hamasa. Lakini pia inatutoa nje ya mstari pale tunapoilisha vitu hasi au habari mbaya. Kitu muhimu hapa ni kwamba sisi ndio chanzo, ndio tunaotuma taarifa aidha za hamasa au mbaya. Maisha kama maisha hayatumi chochote kwenda kwenye ubongo (akili), wala ndugu wa familia sio wao wanaofanya hivyo, hata taarifa za kwenye vyombo vya habari wala hazifanyi hivyo. Ni sisi pekee ndio wenye uwezo wa kuzifikia akili zetu. Again. The brain sends the body energy when we send the brain something inspiring.
13. Kuna hatua tatu za kupata tiba ya kuondokana na kuahirisha mambo (procrastination). Tiba hii ni kiboko, ukiitumia tiba hii, kuahirisha mambo itakua ni stori tu. Je wataka kufahamu tiba hiyo? Twende sasa. Anza hivi. Andika mambo 3 ambayo umekua ukiyapiga dana dana kuyafanya, yaani umekua ukiyasogeza mbele kila mara. Ukisha yaandika mambo hayo matatu, mambo hayo 3 ndiyo yatakayokua hatua 3 za muhimu sana za mwanzo. Anza kufanya hayo mambo sasa hivi. Hakikisha unaanza kufanya hayo mambo, bila kuangalia pembeni. Habari ndio imeishia hapo. Hakuna tiba zaidi ya hiyo.
14. Mambo makubwa ni mtiririko wa mambo madogo madogo yanapoletwa pamoja. Ukitaka kufanikisha mambo makubwa lazima ukubali kuanza kidogokidogo. Watu wengi hudhani kwamba mambo makubwa hua yanaanzia kwenye ukubwa huohuo, hii husababisha wengi kukata tamaa ya kukabili mambo makubwa, au huishia kuahirisha mambo hayo mara kwa mara. Siri ipo kwenye mambo madogo madogo yanayofanywa kwa mtiririko. Kama kuna jukumu kubwa unataka kulifanikisha, ligawe kwenye vipengele au hatua kadhaa, kisha anza kufanyia kazi kipengele kimoja hadi kingine, kadri utakavyokua unafanikisha hivyo vipengele ndivyo utakavyokua unapata hamasa na nguvu ya kuendelea kukamilisha hivyo vingine, na mwishowe unakua umemaliza hilo jukumu kubwa kwa nguvu kubwa. Great things are not done by impulse, but by a series of small things brought together. By Vincent van Gogh
15. Asilimia kubwa ya hofu (fears) na imani (beliefs) tulizonazo huku ukubwani, zilianzia toka tukiwa watoto. Imani hizi tulizirithi kutoka kwa wazazi/walezi na jamii zetu, vilevile hofu nyingine tulizichukua kutoka kwa watu wengine waliotuzunguka, kutoka kwenye movies, TV na hata riwaya (novels) mbalimbali. Tulipokua tukijifunza kipi cha kuogopa, pia tulijifunza jinsi ya kujilinda (protection). Ulinzi ulikuja kwa kuwapendezesha wazazi/walezi wetu, waalimu, na mamlaka husika. Tuliwapendezesha kwa kua na tabia “nzuri”. Na uzuri huu ni kutokana na wao walivyokua wakitafsiri hata kama si hivyo inapaswa kua. Tulipofanya “vizuri” wazazi wetu walitupongeza kwa kutuambia “leo umekua mtoto mzuri”. Hivyo ili kuendelea kua mtoto mzuri na usipate adhabu, ili tubidi kuendelea kutengeneza hofu, au kufuata imani fulani zinazowapendezesha wale wakubwa zetu, kama vile wazazi, waalimu n.k. Imani hizi zimekua na athari kubwa hata katika maisha yetu ya ukubwani, kwani inatuwia vigumu sana pale tunapofanya jambo ambalo haliwapendezeshi wengine hata kama ni sahihi na lenye manufaa kwetu. Huu ni ukilema wa akili
16. Watoto wanajifunza zaidi kutokana na wewe ulivyo kuliko unachowaambia. Hii ni kusema kwamba watoto hawafuati maneno yako bali wanafuata vitendo na tabia yako. Yamudu maisha kwanza wewe binafsi, kisha itakua kazi rahisi kwa wanao kufuata mfano bora. Jifanyie kazi wewe zaidi kuliko unavyotaka kuwafanyia kazi watoto wako.
SOMA; Sehemu 7 Ambazo Unatumia Kupoteza Rasilimali Muda Wako
17. Uhuru wa kifedha unakuja kwa kufanya uchaguzi (choices) wa kijasiri na unaohusisha akili sana. Sio kwenda kichwa kichwa tu bila ufahamu, wakati unafanya uchaguzi wa vitu. Lazima akili yako ifanye kazi sawa sawa.
18. Acha mara moja kujidanganya mwenyewe. Watu hua wanajidanganya wenyewe sana, yaani unakuta mtu anatamani kufanya jambo fulani, ila kabla hajaanza hata kufanya jambo hilo tayari ashaanza kujitabiria uongo kwamba hataweza. Mfano unakuta mtu anataka kua mwimbaji, utasikia “Sijui kama nitaweza, maana sauti yangu sio nzuri….” Au Mtu anataka kua mwandishi mashuhuri lakini anasema “ yaani sijui kama nitaweza …” Huo ni uongo tunaojilisha wenyewe, maana uwezo tulio nao ni mkubwa sana. Mashujaa hawahitaji kujua nini chakufanya wala hawahitaji kujua jinsi ya kufanya jambo. Shujaa anachofanya ni kuchagua kufanya hilo jambo. Kama unataka kua mwimbaji, anza kuimba, kama unataka kua fundi mtaalamu wa ujenzi, anza kujenga. Kama unataka kua mwandishi, anza kuandika. Fanya uchaguzi sasa, kasha anza.
19. Maana ya kweli (true meaning) ya kitu chochote inatoka ndani mwako. Ukiamua kukipa kitu chochote au jambo lolote maana, litakua na maana. Ndio sababu unaweza kuta jambo fulani linaonekana lina maana, kwa mtu huyu, lakini jambo hilohilo likawa halina maana kwa mtu mwingine. Kama wataka kufurahia maisha huna budi kuyapatie maana mambo yako, kabla wengine hawajayapa maana, ambayo pengine wewe hutaifurahia. Maana inapatikana ndani yako, chimba ndani yako.
20. Vitendo (action) ndivyo vinavyotangulia furaha. Tumekua tukichelea kuchukua hatua kwenye jambo kwa kisingizio kwamba hatujisikii furaha, wala Amani kufanya jambo hilo. Hii imekua ni tabia, kwamba mpaka uwe na furaha ndio uchukue hatua. Kumbe hua tunajinyima furaha mara kibao kweli. Siri ni kwamba, utakapoanza kuchukua hatua, furaha itakuja. Hata kama hujisikii wakati unaanza kufanya wewe endelea kutekeleza hilo jukumu furaha itakukuta njiani. Weka commitment ya hali ya juu mpaka matokeo mazuri yameonekana, halafu uone kama hutajihisi mwenye furaha. Take action and then happiness will follow.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: