Habari za wakati huu rafiki?
Karibu tena kwenye mazungumzo yetu mazuri haya ambapo tunashirikishana mambo mbalimbali kwa ajili ya mafanikio.
Kama uliandika email kupata nafasi kwenye program mpya ya ukocha, email bado zinafanyiwa kazi ili kuchagua ni watu gani nitafanya nao kazi. Niwashukuru na kuwapongeza sana wote ambao mmeitaka program hii. Utapata majibu muda sio mrefu.
Leo katika mazungumzo yetu haya tutajadili kitu kimoja muhimu sana kwa mafanikio ya kila mmoja wetu. Kwa kuwa na kitu hiki inakurahisishia wewe harakati zako za kuboresha maisha yako. na kwa kukikosa inaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwako kupiga hatua.
Tunachozungumzia hapa leo ni kuwa chanya, kufikiria katika mazingira ya uwezekano, kuwa na moyo kwamba mambo yatakwenda sawa hata kama unapitia magumu na kuendelea kuiona picha kubwa ya wewe kufikia malengo yako hata kama kwa sasa mambo sio mazuri.
Kuwa chanya ni muhimu sana kama kweli unayataka mafanikio makubwa.
Lakini hatupo chanya.
Wote tunaanzia kwenye hali hasi, kila mmoja wetu anakuwa ametawaliwa na hali hasi zaidi kuliko chanya. Na hali hii tunajifunza kwenye mazingira tunayoishi, ambapo ni nyumbani, shuleni, na hata kwenye jamii kwa ujumla. Inawezekana ulikuwa na mawazo mazuri sana ya kufanya kitu cha maendeleo lakini ukaambia achana nacho, hutaweza, utashindwa, hailipi na kadhalika.
Jamii inayotuzunguka ipo hasi, na chochote tunachojifunza kwenye jamii hii kinaanzia na mambo hasi.
Unaendelea kujilisha hasi.
Jambo jingine muhimu linalofanya iwe vigumu kuondoka kwenye hali hasi ni kwamba kadiri siku zinavyokwenda, tunaendelea kujilisha hasi. Tunakula hasi nyingi kiasi kwamba hatuwezi tena kupiga hatua kufikia malengo na mipango yetu.
Tunakula hasi nyingi kwenye habari tunazopata kila siku. Zaidi ya asilimia 90 ya habari zote unazopokea kila siku kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari ni hasi. Kila unaposikiliza habari hizi, unaondoka ukiwa unajisikia vibaya sana kwako binafsi au kwa watu fulani. Hali hii inazidi kuwa kikwazo kwako kupiga hatua zaidi.
Kuwa chanya kunalipa kuliko kuwa hasi.
Unaweza usiweze kudhibitisha hili ila ni la kweli kabisa, kuwa chanya unavutia fursa nyingi kuliko kuwa hasi. Unapokuwa hasi ni kama kuna nguvu fulani ambayo inakuzunguka na inawazuia watu kufanya kitu muhimu na wewe. Unapokuwa chanya unakuwa na nguvu zinazokuzunguka ambayo inawavutia watu wengi kuendelea na wewe.
Kwa kuwa chanya utashangaa kila tatizo au changamoto unayokutana nayo, badala ya kuichukia na kuona ndio mwisho wa safari, unaanza kuipenda na kuona safari ndio kwanza imeanza na hapa umepata darasa muhimu sana.
Nikushirikishe mfano wangu mdogo sana, kwa vitu ambavyo vimekuwa vinanitokea kwa kuwa tu chanya.
Mwishoni mwa wiki iliyopita nilipata simu kutoka kwa mmoja wa wasomaji wenzetu akiniambia kwamba anahitajika mtu wa kufundisha kuhusu biashara na ujasiriamali. Nilimjibu nipo tayari na hivyo akaniunganisha na mhusika mkuu wa mafunzo hayo niliyotakiwa kuyatoa. Tuliwasiliana naye na akanipa maelekezo yote kuhusiana na mafunzo hayo na yalikuwa yanafanyika wiki hii. Tulikubaliana malipo na akanitumia mkataba wa kazi hiyo na mambo yote yalikuwa yanaonekana kwenda sawa.
Sasa mwanzoni mwa wiki hii, mtu yule alinipigia kuniambia kwamba hawataweza kunichukua kutoa mafunzo hayo kwa sababu sikuwa nimefikia vigezo wanavyotaka wao, ni shirika kubwa, na hivyo maamuzi yanafanywa kulingana na taratibu walizoweka au kuwekewa.
Baada ya hili ningeweza kuwa hasi sana, ningeweza kulalamika au kulaumu kwa nini aliniweka kwenye hali ya kuanza kuandaa mafunzo halafu anakuja kunipa taarifa za kutokushiriki dakika za mwisho.
Lakini sikuwa na muda w akufanya hivi, badala yake nilifikiria ni namna gani ninaweza kupata mteja wa kuziba pengo hilo, ambaye atalipa kiasi kile kile ambacho ningelipwa kwenye kutoa mafunzo yale. Na kabla hata sijafikiria zaidi nilipata simu kutoka kwa mtu mwingine ambaye alikuwa anataka huduma zangu na angelipia gharama inayokaribiana na ile ambayo ningepeta kwa kutoa mafunzo. Tulielewana vizuri na kufanya malipo huku kazi nyingine inaendelea.
Unaweza kuchukulia hili vyovyote utakavyo, labda ni bahati tu, labda ni mwingiliano, labda imetokea tu na kadhalika. Lakini mimi nachukulia hili kama hali chanya ambayo imenivutia fursa nyingi zaidi. Kama ningekuwa hasi, nguvu hasi inayonizunguka ingemkimbiza kabisa huyu mteja mpya. Na nguvu hasi haiwaathiri tu wale wanaokuzunguka, bali hata waliombali. Kama uko hasi utaonesha hilo kwenye mazungumzo yako ya simu na hata jinsi unavyojibu ujumbe.
Pia hii sio KAMA IPO IPO TU, maana kuna watu huwa wanatumia usemi huo kuepuka kujituma zaidi na kwenda hatua ya ziada. Wao wanaamini fursa zimeshapangwa tayari na hivyo hata ufanye nini utapata kile ulichopangiwa kupata. Wanaweza kuwa kweli lakini kimoja ambacho hawajui ni kwamba fursa wanazipanga wenyewe kutokana na mawazo waliyonayo kwenye akili zao.
Unawezaje kuwa chanya?
Kwa ufupi sana hapa nakushirikisha mambo yatakayokufanya uwe chanya na uendelee kuwa chanya.
1. Mara zote fikiria katika uwezekano, hata mara moja usiseme HIKI HAKIWEZEKANI bali sema na jiulize NAWEZAJE KUFANYA HIKI? Mara zote kuwa mtu w akufikiria hali ya vitu kuwezekana na njia bora za kufanya na kupata kitu.
2. Soma na sikiliza vitu chanya. Soma vitabu chanya, sikiliza vitabu chanya, ongea mambo chanya, yaani hakikisha chochote kinachoingia kwenye akili yako ni chanya.
3. Epuka kusoma na kusikiliza vitu ambavyo ni hasi. Anza kwa kutokusoma wala kuangalia habari kabisa. Mtu aliyejinyonga huko rukwa hana msaada wowote kwako zaidi ya kukuletea hisia hasi. Acha kujiingiza kwenye uhanga huu kwa kusikiliza na kusoma habari. Ni kupoteza muda wako na kuzipoteza fursa nyingi.
4. Epuka watu ambao ni hasi. Hapa panaweza kuwa pagumu lakini unahitaji kufanya. Kama kuna watu kwenye maisha yako ambao huwa unakaa nao kwa muda mrefu, na watu hawa muda wote ni kulalamika na kulaumu, unahitaji kuwaepuka watu hao haraka sana. Kwa sababu nilichojifunza kwa uzoefu ni kwamba unapokuwa na mtu anayelalamika ni rahisi sana na wewe kuigia kwenye kulalamika.
5. Jiambie kauli chanya mara kwa mara kwenye siku yako. angalau kila unapoamka na kabla hujalala.
Kujijengea mawazo chanya na kuwa mtu chanya wakati wote sio zoezi rahisi ila kadiri unavyolifanya kwa moyo utaanza kuona matokeo mazuri. Utaanza kuona fursa nyingi za wewe kuchukua hatua na kunufaika zaidi. Anza sasa, ndio yaani sasa hivi kwa kuilisha akili yako mambo ambayo ni chanya.
Karibu kwenye dunia ya uchanya.
Kama tulivyoona kwenye jamii tunayoishi, tunazungukwa na watu ambao ni hasi sana na hivyo mazingira yetu yote ni hasi. Sasa unaweza kupata mazingira ambayo ni chanya na kila siku ukawa katika hali chanya. Mazingira haya yanapatikana kwenye kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA.
Kupata nafasi ya kuingia kwenye kundi hili la wasap, lipia ada ya mwaka ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni tsh elfu 50 kwenye namba; tigo pesa 0717396253 au mpesa 0755953887. Ukishafanya malipo, nitumie ujumbe kwenye wasap kwenye namba 0717396253 na nitakupa maelekezo mengine pamoja na kuingia kwenye kundi. Kama kweli unataka kuwa chanya, kama kweli unataka kuvutia fursa zaidi, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA sasa hivi kama bado. Tuma malipo na tuma ujumbe kwenye wasap.
Nakutakia kila la kheri kwenye kufanyia kazi haya uliyojifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,