Ingekuwa kuweka tu mipango ndio kufanikiwa, basi kila mtu angekuwa na mafanikio makubwa sana.
Kila mtu anaweka mipango mizuri sana, yaani sana.
Lakini mipango hii haijitekelezi yenyewe, unahitaji kuweka kazi kubwa ili kuweza kuitekeleza.
Kadiri mpango ulivyo mzuri na mkubwa, ndivyo ulivyo mgumu kutekeleza na utakutana na changamoto nyingi.
Na ugumu huu na changamoto ndio zimekuwa zinawafanya wengi kushindwa kuendelea. Kwani wanapokutana navyo huona haiwezekani na kuacha wanachofanya. Kwa kuwa kuweka mipango ni rahisi, basi huwa wanakimbilia kuweka mipango mingine.
Kama utafanya hivi, kila mara kuweka mipango mipya, huwezi kufikia mafanikio makubwa.
Mafanikio makubwa utayapata pale utakapokomaa na mpango mmoja mpaka unaukamilisha. Ukishaamua kwamba hiko ndio unachotaka, basi komaa, hata ukutane na ugumu kiasi gani, usikate tamaa, endelea kufanyia kazi mipango yako.
Kama utakomaa na mipango yako, naweza kukuhakikishia kitu kimoja, ni lazima utaifikia. Kwa sababu dunia haiwezi kumzuia mtu aliyejitoa kweli kupata kile anachotaka.
Kumbuka inaruhusiwa kubadili njia, lakini hairuhusiwi kubadili safari, pita popote utakapopita, lakini ufike pale ulipopanga kufika.
SOMA; Sababu 5 Kwa Nini Ni Marufuku Wewe Kukata Tamaa.
TAMKO LANGU;
Najua mafanikio yangu kwenye maisha yanakuja sio kwa kuweka tu mipango, bali kuifanyia kazi mipango hiyo. Na katika kutekeleza mipango hiyo najua kuna vikwazo na changamoto nyingi zinazokatisha tamaa. Mimi nimejitoa kweli na sitakata tamaa mpaka nifikie kile ambacho nakitaka. Hata mambo yawe magumu kiasi gani, sitorudia njiani, nitakomaa mpaka nifikie kile nilichopanga.
NENO LA LEO.
“Plan for what is difficult while it is easy, do what is great while it is small.” – Sun Tzu
Panga magumu wakati bado ni marahisi, fanya makubwa wakati bado ni madogo.
Chochote kigumu huwa kinaanza kwa urahisi, na chochote kikubwa huwa kinaanza kidogo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.