Tunaishi kwenye dunia ambayo tunasukumwa sana kuwa wanunuaje, wateja.
Tunalazimika kununua vitu vingi ambavyo hata hatuna matumizi navyo, na kama tunayo basi sio muhimu sana.
Tunalazimika kununua kwa sababu tu tunaogopa tusipitwe. Na hapa ndipo utumwa mkubwa wa dunia unapoanzia.
Sio vibaya kununua, ila kununua kwa msukumo ni utumwa mkubwa zaidi.
Na hapa ndipo matatizo mengi ya kifedha ya watu wengi yanapoanzia. Pale wanaponunua vitu ambavyo hawana mahitaji navyo makubwa.
Matangazo mengi ya vitu yanakupa msukumo kwamba kinapita, na usiponunua sasa basi unapitwa, au utaonekana mshamba kwa sababu wajanja wote wanacho kitu hiko. Na wewe unalazimika kununua ili uwe sehemu ya wajanja hao.
Ni muhimu uelewe kwamba kufanikiwa kwenye dunia ya sasa unahitaji uweze kusimama mwenyewe, kufanya vile vitu ambavyo unavipenda wewe hata kama wengine hawafanyi na kuweza kusema hapana hata kama watu wengi wanasema ndio.
Kama utashindwa kusimama mwenyewe, basi utajikuta unapelekwa na kila kitu na kuishia kuwa mteja wa kila siku,
Kumbuka kama hutaweza kusimama kwa kitu fulani, basi utaanguka kwa kila kitu.
Kwenye dunia ya sasa ambayo inakusukuma uwe mteja wa kila kitu, kama hutakuwa na vipaumbele vyako ambavyo unavisimamia, utaanguka kwa kila kitu na hivyo kuwa mteja wa kila kitu.
Na mbaya zaidi ni kwamba mwanzo unasukumwa kununua vitu, ili uvimiliki, lakini mwishoni vitu hivi ndio vinakumiliki wewe. Na unakosa uhuru wa kuwa na maisha unayoyataka wewe.
SOMA; Tabia Tano Mbaya Ambazo Kila Mtu Anazo Na jinsi unavyoweza kuzitumia kufanikiwa.
TAMKO LANGU;
Najua dunia ya sasa inanisukuma kuwa mteja wa kila kitu. Inanivutia sana niwe mteja kwa kuniambia nisipochukua hatua ninapitwa au nitaikosa. Mimi nimeshaweka vipaumbele vyangu na hivi ndio vitakavyoniongoza. Nakataa kuongozwa na kundi na badala yake najiongoza mwenyewe kwa sababu najua kipi muhimu kwangu.
NENO LA LEO.
“The things you own end up owning you. It’s only after you lose everything that you’re free to do anything.”
― Chuck Palahniuk
Vitu unavyomiliki vinaishia kukumiliki wewe. Baada ya kupoteza kila kitu ndio unaweza kuwa huru kufanya chochote.
Tunashawishiwa kununua kila kitu ambacho kila mtu ananunua, na vitu hivi vinaishia kutumiliki, na kutunyima uhuru wetu. Achana na hili mara moja, fuata vipaumbele vyako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.