Ni muhimu sana kujali muda na kuwahi kwenye kila kitu ambacho unahusika nacho wewe.
Ila kuna maeneo ambayo unahitaji kuchelewa kwa makusudi. Kwa kuchelewa huku inakuwa ni faida kubwa kwako baadae.
Jana katika makala hizi za kurasa tuliona jinsi ambavyo jamii inakuaminisha kwamba unapitwa na hivyo kukusukuma ununue kila kitu ambacho kila mtu ananunua, hata kama sio muhimu sana kwako.
Unaanza kwa kununua vitu na kuvimiliki, baadae vitu hivi vinaanza kukumiliki wewe na hapa ndipo unapokosa uhuru mkubwa wa maisha yako.
Jana tuliona baadhi ya njia za kuepuka hilo, kama hukusoma makala ile ya jana uisome hapa; UKURASA WA 330; Unapitwa….
Leo nakushirikisha njia nyingine muhimu ya kuepuka kuingia kwenye gereza hili la kununua vitu halafu baadae vinakumiliki. Na njia hii ni kuchelewa kwa makusudi.
Njia hii iko hivi, unapoona unasukumwa sana kununua kitu, unapoona unataka kabisa kununua kitu, usikinunue muda huo, jicheleweshe. Kwa kujichelewesha utapata muda wa kutafakari vizuri kama kitu kile kweli unakipenda na ni muhimu sana kwako.
Unapokuwa karibu na kitu, na mwuzaji akaanza kukupamba maneno, ni rahisi sana kufanya maamuzi ya kununua.
Swali; ni mara ngapi umeshanunua vitu na baadae ukagundua umekosea. Au unanunua kitu na usikitumie kabisa.
Dawa ya hii ni kujichelewesha, jiwekee utaratibu wewe mwenyewe kwamba hutanunua kitu mara ya kwanza unapokutana nacho. Badala yake jicheleweshe, na katika kuchelewa huku ndio utajua kama kitu kile ni muhimu kwako.
Na vitu vingi ambavyo unanunua chini ya msukumo ni vitu ambavyo sio muhimu sana kwako. Maisha yako yanaweza kwenda vizuri hata bila ya vitu hivyo.
Vikwazo vitakavyokufanya ushindwe kutekeleza hili.
Najua umeona hili ni wazo zuri sana, lakini katika kutekeleza utakutana na changamoto.
Kuna wakati utaona au kuoneshwa kwamba kile unachoona ndio cha mwisho, usiponunua sasa hutakipata tena. Nikupe uhakika kwamba ni uongo, hakuna kitu cha mwisho na kama unakitaka kweli hutashindwa kukipata.
Wakati mwingine unaweza kujishawishi wewe mwenyewe kwamba kile unachokwenda kununua ni muhimu sana kwako, hivyo kufanya manunuzi hayo haraka. Sikiliza kwa makini, pale ulipo hisia zako zimeshachajiwa, huwezi kufikiri kwa makini, ndio maana nakushauri uchelewe kwa makusudi, hisia zako zishuke na ndio utaweza kufikiri kwa kina kama kweli kile ndio unachotaka. Kama kitu sio dharura, yaani kwa kutokuchukua hatua mtu atakufa, basi kinaweza kusubiri.
SOMA; Tabia Kumi Mbaya Kuhusu Fedha Zinazokufanya Uendelee Kuwa Masikini.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kuchelewa kwa makusudi kwenye kufanya manunuzi ni njia bora ya kujua kama kweli kile ninachokwenda kununua ni muhimu sana kwangu. Kuanzia sasa sitanunua kitu papo kwa hapo, nitajichelewesha kwa makusudi ili nipate muda wa kufikiri kwa kina, wakati ambapo hisia zangu zinakuwa zimeshuka.
NENO LA LEO.
“We buy things we don’t need with money we don’t have to impress people we don’t like.”
― Dave Ramsey
Tunanunua vitu ambavyo hatuvihitaji, kwa fedha ambazo hatuna na kuwafurahisha watu ambao hatuwapendi.
Kamwe usiendelee kununua vitu ili kuwafurahisha wengine, nunua kile ambacho ni muhimu kwako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.