Wewe kama mfanyabiashara ni lazima uweze kuwaelewa wateja kwa njia mbalimbali.
Kuelewa kile wanachosema, na jinsi wanavyokisema ikiambatana na vitendo vinavyoendana na kile wanachofanya.
Kuna baadhi ya kauli ukizisikia kutoka kwa wateja zinakupa moyo kwamba ni dalili nzuri, lakini ukweli ni kwamba kauli hizo zinaashiria umeshampoteza mteja.
Kauli moja muhimu sana nitakayokushirikisha leo ni hii; NIKIWA TAYARI NITAKUTAFUTA.
Hapa umeshamwambia mteja kuhusu bidhaa au huduma unayotaka kumuuzia. Umeshamweleza kila kitu, amekuuliza maswali na umemjibu. Mwisho kabisa anakwambia ASANTE, NIKIWA TAYARI NITAKUTAFUTA.
Kwanza kabisa elewa huo ni uongo, mteja anajaribu kutafuta njia laini ambayo haitakuumiza ya kukwambia kwamba sitanunua unachouza.
Anajua akikuambia moja kwa moja utaumia, ukizingatia muda uliotumia kumwelewesha.
Hivyo anatafuta kauli laini ya kukwambia, na wewe unaipokea na kufurahi kwamba mteja amekuelewa.
Kuanzia sasa usipokee tena kauli hiyo kirahisi, maana yake unapoipokea unakuwa umekubaliana na mteja kwamba asinunue.
Na hii inakwenda hivyo sio kwenye biashara tu, hata kwenye makubaliano yako na wengine, ukiona mtu anakuambia nikiwa tayari nitakuambia, jua anakukimbia.
Sasa ufanye nini pale unapopewa kauli hii?
Hii tutajifunza kesho kwenye kipengele hiki cha BIASHARA LEO, usikose.