Maamuzi yoyote tunayofanya kwenye maisha yetu, yamegawanyika katika aina mbili.

Aina ya kwanza ni maamuzi tunayofanya kwa kusukumwa na hofu, unafanya maamuzi kwa sababu unahofia kitu fulani kitatokea au hakitatokea.

Aina ya pili ni maamuzi tunayofanya kwa kusukumwa na mapenzi au ukuaji, hapa unafanya maamuzi kwa sababu unataka kukua zaidi.

Hivi ndivyo unavyoweza kuyagawa maamuzi yote unayoyafanya.

Kwa mfano, unafanya kazi unayofanya sasa kwa sababu unahofia ukiacha maisha hayataenda au unafanya kwa sababu unaipenda na kupitia kazi hiyo utakua zaidi?

Je kwenye mahusiano uliyopo sasa, yawe ya kirafiki, kiuchumba au hata ya kindoa, unaendelea kuwepo kwenye mahusiano hayo kwa sababu unaogopa ukiondoka hutapata mwingine au upo kwa sababu uliyenaye ana mchango kweli kwenye maisha yako?

Sasa tofauti hii ya maamuzi haiishii tu hapo kujua yapo ya aina mbili, inakwenda mbali zaidi.

Unapofanya maamuzi ya hofu huwa sio maamuzi bora kwenye maisha yako, ni maamuzi ambayo yatakuumiza sana na yatakuzuia kuishi maisha ya furaha na mafanikio.

Unapofanya maamuzi ya ukuaji, ni maamuzi ambayo ni bora kwako na yatafanya maisha yako kuwa ya furaha na bora sana.

Na pia unapofanya maamuzi ya hofu unaweza kuona yana manufaa kwa muda wa sasa, ila yatakutesa kwa muda mrefu sana. Na maamuzi ya ukuaji yanaweza kukupeleka kwenye changamoto kubwa, lakini utayafurahia sana baadae.

Je wewe umefanya maamuzi yako makubwa kwa njia ipi? Hofu au ukuaji?

SOMA; Usifanye Maamuzi Yako Kwa Kigezo Hiki, Utajuta Sana…

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba maamuzi ninayofanya kwenye maisha yangu yanaweza kuwa yanaongozwa na hofu au ukuaji. Maamuzi yanayoongozwa na hofu ni yale ninayofanya kwa kuhofia nisipofanya mambo yatakuwa mabaya, na hivyo nalazimika tu kufanya. Maamuzi ya ukuaji ni yale ambayo nayafanya kwa kitu ambacho ninakipenda. Kuanzia sasa nitakuwa nafanya maamuzi ya ukuaji na sio ya hofu.

NENO LA LEO.

“Trust your instincts, and make judgements on what your heart tells you. The heart will not betray you.”
― David Gemmell

Amini machale yako, na fanya maamuzi kwa kile moyo wako unakuambia. Moyo wako hauwezi kukusaliti hata siku moja.

Siku zote fanya maamuzi kwa kusukumwa na upendo, ukuaji na sio kusukumwa na hofu.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.