Kila mmoja wetu kuna kitu fulani alishajutia, yaani ulishafanya kitu fulani na baadaye ukagundua ya kwamba ulikosea. Kila mmoja wetu.
Lakini majuto haya hayafanani kwa kila mmoja wetu, hasa jinsi ambavyo tunayatumia kwa baadae.
Kama ningejua, ningechukua ile fursa mapema….
Kama ningejua nisingeingia kwenye hii kazi au biashara….
Kama ningejua nisingeingia kwenye haya mahusiano…
Kama ningejua ningejali zaidi…
Na kama ninge nyingi sana.
Unawezaje kutumia majuto?
Tumekuwa tukitumia majuto kwa aina mbili tofauti.
Aina ya kwanza; kuturudisha nyuma.
Sehemu kubwa ya watu wamekuwa wakitumia majuto kujirudisha nyuma. Kila unapotaka kuchukua hatua unajikumbusha ya kwamba ulichukua hatua kipindi fulani na mambo hayakuenda vizuri, na hivyo unaacha kuchukua hatua.
Utasikia mtu anatoa kauli kama, siwezi tena kuingia kwenye biashara, siwezi tena kuja kumwamini mtu na mengine mengi. Haya yanamzuia mtu kuweza kwenda mbele zaidi.
Aina ya pili; kuwa kichocheo cha kusonga mbele.
Sehemu ndogo sana ya watu wanatumia majuto kama kichocheo cha kwenda mbele zaidi. Hawa wanajua ya kwamba mwanzo walikosea na wanatumia makosa yale kama msingi wa kufanya maamuzi sasa. Wanaepuka kile ambacho walikosea awali na kuhakikisha wanafanya maamuzi bora kabisa.
Hawa ndio wale wanaosema, ndio sikujua, ila sasa najua na nitafanya hivi badala ya vile nilivyofanya awali.
Je wewe unayatumiaje majuto?
SOMA; Acha Kutafuta Pesa Ambazo Hutazipata, Tafuta Hiki Kimoja Na Usahau Matatizo Yako Ya Pesa.
TAMKO LANGU;
Najua majuto yangu yanaweza kuwa kichocheo cha mimi kwenda mbele au yakawa kikwazo na kunirudisha nyuma. Lakini hayo yote nachagua mimi mwenyewe. Na mimi nimechagua kuyatumia majuto yangu kama kichocheo, kile ambacho sikujua ndio nimeshakijua na sasa ninasonga mbele.
NENO LA LEO.
If you don’t learn from your mistakes, then they become regrets.
John Cena
Kama hujifunzi kutokana na makosa yako, yanakuwa majuto.
Yatumie majuto yako kama kichocheo cha wewe kwenda mbele zaidi na sio yakurudishe nyuma.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.