Ni asili ya binadamu kujificha pale anapokutana na jambo ambalo anaona haliwezi, au linamzidi, au hayupo tayari kuweka juhudi kubwa kwenye jambo hilo.
Na kwa sababu hataki kuonekana na wengine kwamba jambo lile hawezi, au haweki juhudi, basi mtu hujificha.
Unapoona unahitajika kuchukua hatua kubwa kwenye biashara yako na wewe hupo tayari kufanya hivyo basi unajificha, kwa kukwepa hatua ile, na kuja na sababu kwa nini huwezi kufanya hivyo.
Kazi yako inapohitaji ujitoe zaidi, uende hatua ya ziada ili kuweza kupata unachotaka, na wewe hupo tayari kufanya hivyo, unajificha. Unakuja na sababu kwa nini huwezi kuchukua hatua hiyo, ambayo itakuridhisha wewe na wengine pia.
Tunapenda kujificha pale ambapo mabadiliko yanahitajika.
Pale ambapo unahitajika kusimama na kutetea unachoamini, unapohitaji kusimamia kile ambacho wengi wanakipinga, mara nyingi wengi hujificha.
Ni wakati sasa wa kuacha kujificha, wa kutoka mbele, kufanya kile ambacho unahitaji kufanya, kile ambacho unakiamini kweli. Ni wakati wa kuchukua hatua kwa jambo lolote ambalo unalitaka, maana hiyo ndiyo njia pekee na ya uhakika ya kulipata.
Ukiendelea kujificha, utaishia kuona wengine wakipiga hatua na kupata kile wanachotaka. Jitokeze sasa na anza kuchukua hatua, kubwa kadiri uwezavyo.
SOMA; Muda; Mambo Muhimu Ya Kuzingati Ili Kuwa Na Matumizi Mazuri Ya Muda Wako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mara nyingi nimekuwa najificha pale ninapohitajika kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yangu. Kuanzia sasa nimeamua kutokujificha tena, nitachukua hatua ile ambayo ni muhimu kwangu kuweza kupata kile ambacho ninakitaka.
NENO LA LEO.
“Man is not what he thinks he is, he is what he hides.”
― André Malraux
Mtu hayuko vile anavyofikiri yupo, bali yupo vile anavyojificha.
Umefika wakati sasa uache kujificha na kuanza kujitokeza, kufanyia kazi yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.