Tunazaliwa na kuingia kwenye jamii ambapo tunakuta taratibu mbalimbali. Tunakua tukiambiwa fanya hiki, usifanye kile na vingine vingi. Taratibu za kijamii zinatujengea mipaka mingi sana ambayo inaweza kuwa mizuri kwetu au ikawa kizuizi kwetu kuwa na yale maisha ambayo ni bora zaidi kwako.
Katika kukua pia tukarithishwa imani ambazo familia au jamii zetu zimekuwa zikiamini. Inaweza kuwa imani za kidini au imani nyingine za kijamii. Tulipokea imani hizi na kuzifanya kuwa sehemu ya maisha yetu.
Tukapata nafasi pia ya kwenda shuleni, ambapo huko nako tuliongezewa mambo mengine mengi. Tukafundishwa mwingi kuhusu dunia, kuhusu historia na hata kuhusu maisha kwa ujumla. Huko nako tukajifunza mengi ambayo yaliweza kutengeneza maisha yetu vile yalivyo sasa.
Sasa mpaka hapo mambo yote yalikuwa yanakwenda vizuri, hapo ni wakati ukiwa bado unakua, ila sasa umeshapita kipindi cha ukuaji, na umekuwa mtu mzima, ndio unaanza kuona changamoto kubwa.
Uliahidiwa kwamba kama utasoma kwa bidii ukafaulu masomo yako vizuri utapata kazi nzuri sana na maisha yako yatakuwa bora. Ukafanya hivyo kweli, ukasoma, ukafaulu, ukapata kazi, lakini bado huoni maisha yakiwa bora.
Uliahidiwa kama utakazana ukapata kazi nzuri, yenye malipo makubwa na ukawa tajiri basi maisha yako yatakuwa bora sana. Ukakazana kweli, ukapata kazi yenye malipo makubwa, ukazipata fedha, lakini bado unaona maisha yako yana utupu fulani.
Changamoto zote hizi zinaanzia sehemu moja muhimu sana, ambayo hakuna ambaye amewahi kukuambia ufanyie kazi. Na kama hukupata nafasi ya kujifunza wewe mwenyewe basi unakosa nafasi ya kufanyia kazi kitu hiko muhimu na hivyo kwenda maisha yako yote ukijaribu vitu vingi lakini bado usipate kuridhika.
Ni jukumu lipi muhimu sana kwenye maisha yako?
Jukumu hili ni KUJIJUA WEWE MWENYEWE. Unahitaji kujijua wewe mwenyewe, ndiyo uweze kuendesha maisha ambayo yatakuwa bora sana kwako. Hili ni jukumu ambalo utaweza kulifanya wewe mwenyewe tu, hakuna atakayekusaidia kufanya jukumu hilo. Wengine wanaweza kukusaidia kwa kukupa mwongozo, ila zoezi zima utalifanya wewe mwenyewe.
Kama mpaka sasa hujafanya jukumu hili ni kwa sababu katika maisha yote uliyopita hakuna mahali ambapo ulipata mwongozo hua wa kujijua wewe mwenyewe. Sio kwenye familia, sio kwenye jamii, sio shuleni. Kote umekuwa unapita na kufundishwa makubwa, lakini lile la msingi kabisa hujapata nafasi ya kufundishwa.
Haijalishi una umri gani sasa, haijalishi umepitia nini, bado hujachelewa kufanya jukumu hili muhimu sana kwenye maisha yako. na kadiri utakavyolifanya mapema na kuanza kufanyia kazi, ndivyo utaacha kupoteza muda wa maisha yako na kuanza kuyafanya kuwa bora zaidi.
Hatua tano za kujijua wewe mwenyewe.
Unawezaje kujijua wewe mwenyewe? Hapa kuna hatua tano muhimu za kufanya hivyo, zifanyie kazi zote na utaanza kuona mabadiliko kwenye maisha yako.
Hatua ya kwanza; jua haiba yako.
Kila mmoja wetu ana haiba yake, na kuna haiba za aina mbalimbali baina ya watu. Kuna mambo mengi sana kwenye haiba, lakini wewe mwenyewe ndiye unayeweza kujua wewe unaangukia wapi.
Jiangalie kwa makini, tafakari maisha yako mpaka hapo ulipofika sasa, umekuwa unapelekaje mambo yako?
Umekuwa unataka vitu kwa haraka, kung’ang’ana mpaka upate, au umekuwa ukitaka vitu bila ya haraka na unasubiri mpaka vitakapojitokeza?
Je ni kwa namna gani unaona ukifanya ndiyo maisha yako yanakuwa bora? Je umekuwa uko tayari kujituma na kufanya vitu mwenyewe au huwa unasubiri mpaka upangiwe na cha kufanya ndiyo ufanye?
Je umekuwa na uvumilivu kiasi gani katika mambo unayopitia? Huwa unavumilia au kukata tamaa mapema?
Yote hayo ni muhimu sana kujiuliza na kujipa majibu maana yatakupa picha ni tabia zipi za msingi ambazo zipo ndani yako. na baada ya kujua tabia hizo, unaangalia zipi nzuri za kuendeleza na zipi sio nzuri na hivyo kuziacha.
Hatua ya pili; jua misingi yako.
Kila mmoja wetu ana misingi yake kwenye maisha. Kuna vitu ambavyo uko tayari kuvisimamia hata kama watu wanasema nini. Na kuna vitu ambavyo huwezi kufanya hata kitokee kitu gani. Katika kujijua wewe mwenyewe ni muhimu sana kujua msingi unayosimamia kwenye maisha yako.
Ni vitu gani ambavyo ni mwiko kabisa kwako wewe kufanya? Iwe ni kwenye maisha yako ya familia, kazi au biashara zako. Ni vitu gani ambavyo uko tayari kuvisimamia hata kama dunia nzima itakuwa inavipinga?
Ni muhimu uwe na vitu unavyosimamia na uvijue kwa sababu hivi ndio vitakavyokutofautisha na wengine na vitakuwa sifa yako kwa wengine pia. Inaweza kuwa ukweli, uaminifu, uadilifu, wema, uhuru, usalama na mengine mengi.
Kwa kujua ile misingi yako kwenye maisha, unakaribia kujijua wewe mwenyewe.
Hatua ya tatu; jua mwili wako.
Unaweza kuona hili ni jambo dogo, kwa kuwa mwili ni wako basi unafikiri unaujua sana. Ukweli ni kwamba unaujua mwili wako kwa kiasi kidogo sana. Katika kujijua wewe mwenyewe, unahitaji kuujua mwili wako. Kwanza jua uimara wako uko wapi, jua udhaifu wako uko wapi, na jua kikomo chako kiko wapi.
Kwa kuwa mwili wako ndio unakubeba wewe, kwa kuujua vizuri kutakuwezesha kujua jinsi ya kuutumia vizuri, kwa kujua kikomo chako iwe ni kwenye kazi au jambo lolote kutakuwezesha kujua upangeje kazi zako.
Pia kwa kuujua mwili wako utaweza kuuandaa vyema kukabiliana na changamoto za maisha unazokutana nazo. Na mwili wako ni wako mwenyewe, hakuna mwingine anayeweza kuujua kuliko unavyoujua wewe. Kuna watu ambao wanaweza kufanya mambo yao kwenye utulivu mkubwa sana, wengine wanaweza kufanya hata kukiwa na kelele. Kuna watu ambao wanaweza kufanya kazi zao usiku sana, wengine wanapendelea asubuhi na mapema. Ujue mwili wako ili uweze kuutumia vyema.
Kitu kingine muhimu sana kwenye kuujua mwili wako ni kujua nguvu zako. Nguvu za miili yetu zinatofautiana kulingana na wakati wa siku. Unapoamka asubuhi unakuwa na nguvu kubwa, unapofika jioni nguvu zinakuwa zimepungua sana. Hivyo kwa kupanga yale majukumu muhimu unapokuwa na nguvu kubwa, kunakuwezesha wewe kuweza kuyafanyia kazi vizuri.
Hatua ya nne; jua ndoto yako kubwa.
Tulipokuwa watoto, kila mtu alikuwa na ndoto kubwa sana, lakini kadiri tulivyokuwa tunakua, dunia ilitukatisha tamaa na kutuambia tuache kufikiri mambo ya kitoto na tufikiri mambo yanayoweza kufanyika. Tulikubaliana na dunia, tukazika ndoto zetu na sasa tunaona maisha yetu bado yana deni.
Jua ipi ni ndoto yako kubwa kwenye maisha yako. jua ni kitu gani ungependa kufanya kwenye dunia hii na kuacha alama kubwa hata utakapoondoka. Ijue ndoto yako na ichambue vyema.
Na ukishaijua ndoto yako anza kuifanyia kazi mara moja, anza kidogo na kila siku fanya kitu kukamilisha ndoto yako.
Hatua ya tano; jua ni mambo gani unayopenda na usiyopenda.
Hakuna kitu kinafanya maisha kuwa magumu kama kufanya kitu ili tu kuwaridhisha wengine, wakati wewe hutaki kufanya kitu hiko. Huku ni kuishi kwa mateso ya kujitakia wewe mwenyewe.
Katika kujijua wewe mwenyewe, jua ni mambo gani unayopendelea kufanya kwenye maisha yako ya kila siku. Ni vitu gani ukifanya unapata furaha moyoni mwako. Na vitu hivi visiwe tu anasa kwako binafsi, bali viwanufaishe na wengine pia.
Pia jua ni vitu gani ambavyo hupendi kufanya, jua ni vitu gani ukifanya hujisikii furaha moyoni. Hata kama kila mtu kwenye jamii anafanya vitu hivyo, bado wewe unaona sio muhimu kwako kufanya.
Hii ni hatua ya awali kabisa ya kujijua wewe mwenyewe, anza na hatua hizi tano na katika makala zijazo kwenye FALSAFA YETU hii ya maisha tutaendelea kuangalia kwa undani kitu kimoja kimoja kama haiba, na hata kujenga imani bora kwetu ambayo itafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.
Nakutakia kila la kheri katika kujenga falsafa hii mpya ya maisha yako ili yawe bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.