Barua hii ya wazi iende kwa vijana wote ambao wamechagua kuanza maisha yao ya kujitegemea kwa mwaka huu 2016. Bado tupo kwenye mwanzo wa mwaka na wakati huu bado malengo na mipango ya wengi ipo hai sana. Na hivyo ni wakati muafaka kwako kusoma barua hii na nina imani kuna mengi au machache utakayoondoka nayo hapa ambayo yatakusaidia sana.
Inawezekana umemaliza masomo yako, na kutafuta kazi sana bila ya mafanikio na sasa upo tayari kuangalia njia nyingine za maisha. Inawezekana hukupata elimu kubwa ila pia umeamua kuangalia upande mwingine wa maisha. Katika barua hii nitakwenda kukushirikisha mambo kumi muhimu sana kwako kuzingatia katika safari hii unayokwenda kuanza. 
Mambo ninayokwenda kukushirikisha hapa ni mambo ambayo niliyafanya mimi nilipoanza safari kama hiyo unayokwenda kuanza wewe. Hivyo ni vitu ambavyo vinawezekana kama ukiamua kuchukua hatua.
Kwanza kabisa nianze kwa kukupongeza sana kama umefikia maamuzi ya kuanza maisha ya kujitegemea. Hiyo ni hatua kubwa sana kwenye maisha yako na inaonesha ya kwamba umeanza kukomaa.
Na pia nikutahadharishe kwamba safari uliyochagua siyo rahisi, kama ilivyo kwa jambo lolote zuri kwenye maisha. Safari hiyo ina changamoto nyingi na hivyo ni lazima uwe umejitoa hasa kama kweli unataka kufikia kile ambacho umepanga kufikia kwenye maisha yako.

 
Yafuatayo ni mambo 10 muhimu ya kuzingatia kwenye safari yako ya maisha ya kujitegemea.
1. Hustahili chochote.
Tuanze na habari ambayo inaweza kuwa siyo nzuri sana kwako, ukweli ni kwamba hustahili chochote. Na nimeanza na hii kwa sababu najua umekuwa unadanganywa sana kwamba unastahili hiki au kile. Hasa kama umepata elimu ya juu basi utakuwa umedanganywa sana ya kwamba kwa kuwa umesoma basi unastahili kupata ajira. Hata kama ni kweli unastahili kupata ajira, lakini ajira hizo hazipo, sasa unafanya nini?
Unapoanza maisha yako ya kujitegemea, anza na mtazamo kwamba hustahili chochote, anza ukijua kwamba hakuna yeyote atakayekuletea kile ambacho unataka. Anza ukijua kwamba chochote unachotaka kwenye maisha yako utakipata kwa kukitafuta mwenyewe.
Kama wazazi wako wana uwezo mkubwa unaweza kuwa pia umedanganywa au umejidanganya kwamba unastahili kupata urithi mkubwa kutoka kwa wazazi wako. Pia nakuambia achana na mawazo hayo na weka juhudi kwenye kutengeneza kile ambacho ni chako. Sikuambii ukatae vile wazazi wanavyokupa, ila ninachokuambia ni usifikiri ni lazima wakupe.
SOMA; Sababu Kumi Na Moja(11) Kwa Nini Usiombe Ruhusa Na Uombe Msamaha.
2. Chukua kazi yoyote unayoweza kupata kwa sasa.
Kama ambavyo tumeona hapo juu, hata kama umesoma, ajira ni changamoto kubwa sana kwa zama hizi tunazoishi. Tumekuwa na wasomi wengi kuliko nafasi za ajira zinazopatikana. Na maendeleo ya teknolojia yanazidi kuvunja ajira nyingi sana. Hivyo kwa sasa, wewe kama kijana usichague sana kazi gani ufanye.
Kama pia tulivyoona hapo juu ya kwamba hustahili chochote, hata kazi pia uliyosomea bado hustahili kuipata. Unaweza kukataa hilo na kugoma nyumbani kwenu mpaka upate kazi uliyosomea, ila jua itakuchukua muda mrefu.
Chukua kazi yoyote ambayo unaweza kuipata sasa, ndio nimesema kazi yoyote hapo, ambayo unaweza kuipata sasa, na ni kazi halali ambayo unaweza kuingiza kipato. Na kwa upande wa kipato usiangalie sana kwa sasa, wewe anza na kuchukua kazi inayopatikana, hatua inayofuata iko hapo chini.
3. Weka juhudi kubwa sana.
Baada ya kupata kazi yoyote na kuamua kuifanya, ifanye kwa bidii sana. Weka juhudi kubwa sana kwenye kazi hiyo, hata kama ni kazi usiyoipenda, hata kama ni kazi ambayo hukusomea. Kwa kuwa umeshaamua kufanya kazi hiyo, weka juhudi kubwa na ifanye kwa ubora ambao hakuna mwingine anayeweza kufanya kama wewe.
Jitoe hasa katika kufanya kwa ubora, usiangalie wengine wanafanyaje na wewe kufanya kama wao, usiangalie unalipwa kiasi gani ndio ufanye kwa kiwango hiko. Fanya kama wewe ndiye mmiliki wa kazi husika au kama wewe ndiye unayelipwa kiwango cha juu sana kuliko wengine wote.
Kikubwa unachohitaji kwa sasa ni watu wa kukuamini kwamba unaweza kufanya kitu na kupata kipato kidogo cha kuendesha maisha yako. kumbuka wewe ni kijana na bado hustahili chochote, hivyo weka juhudi kubwa sana.
4. Ondoka nyumbani.
Nafikiri hili liko wazi, kama kweli umeamua kuanza maisha ya kujitegemea, basi nyumbani unakoishi sio sehemu sahihi kwa wewe kufanya hivyo. Kukaa nyumbani bado utaendelea kupata zile hisia ya kwamba unastahili vitu fulani, utaendelea kujidanganya.
Kama wewe siye unayetoa msaada mkubwa wa kuendesha familia yenu, basi ondoka haraka sana. Kama wewe ndiye unayetegemewa kwenye kuiendesha familia basi endelea kuweka mipango mizuri ya maisha yatakwendaje bila hata ya uwepo wako, kwa sababu kuna wakati utahitaji kutokuwepo.
Soma hapa pia kuhusu kuondoka nyumbani; ONDOKA NYUMBANI
5. Weka gharama zako za maisha kuwa chini.
Hili ndilo jambo la msingi sana sana. Weka gharama zako za maisha chini sana, yaani chini. Ishi yale maisha ambayo ni ya msingi tu. Kumbuka nimekwambia hustahili chochote, hivyo achana kabisa na ule ujinga wa kutaka kuonekana na vijana wenzako, kwamba na wewe una simu ya kisasa, unabadili mavazi kila siku na unakwenda viwanja.
Weka gharama zako za maisha chini, kama una simu zaidi ya moja kwa sasa uza moja na baki na moja, kama una jozi(pair) zaidi ya tano za nguo zinakutosha sana, mwaka huu usinunue tena nguo nyingine. Na epuka gharama zote ambazo sio za msingi. Ila usiepuke kula, kula ni muhimu na kula vyakula vya afya, siyo chipsi. Kama ulikuwa unakunywa pombe acha, ni gharama kubwa sana unayoingia na hakuna kikubwa unachopata.
6. Kuwa na ndoto, ifanyie kazi kila siku, usiridhike haraka.
Unakumbuka nimekwambia chukua kazi yoyote ambayo unaweza kuipata kwa sasa, iwe ipo kwenye malengo yako au la. Kikubwa ni kuchukua kazi ambayo itakupa majukumu mbele ya wengine na utaanza kutengeneza jina lako. Lakini wakati unafanya kazi hiyo ni lazima wewe binafsi uwe na ndoto yako kubwa. Ni lazima ujue unataka kwenda wapi na maisha yako, ni yapi makubwa unataka kufanya kwenye maisha yako.
Na fanyia kazi ndoto hii kila siku. Usiridhike haraka kwa chochote unachopata, hitaji zaidi na nenda hatua ya ziada kwenye kila jambo. Utakapoweka juhudi kubwa kwenye kazi yoyote uliyoipata, utaona watu wanakushawishi ukae kwenye kazi fulani milele, usikubali, kazi yoyote unayokwenda kuanza siyo ya kufa nayo, pale unapata tu uzoefu wa dunia na pia unaionesha dunia ni kipi ulichonacho ndani yako.
7. Nidhamu.
Nidhamu ni muhimu sana katika safari hii unayokwenda kuanza. Maisha ya kujitegemea wewe mwenyewe siyo maisha ya kufanya chochote unachotaka, maana hii ndio picha ya kwanza utakayokuwa unapata kwenye akili yako. kwamba sasa naondoka nyumbani ambapo nabanwa na nakwenda kufanya chochote ninachotaka, utapotea.
Ni lazima uwe na nidhamu ya hali ya juu sana, uwe na nidhamu binafsi, ya kuheshimu mipango yako na ratiba zao. Ni lazima uwe na nidhamu ya fedha, kuhakikisha matumizi hayakui kuzidi kipato chako. Na pia ni lazima uwe na nidhamu ya muda, maana hii ndio rasilimali muhimu sana kwako.
Hii dunia haina huruma kama unavyofikiri, ukishindwa kwenda kwa nidhamu, itakupoteza kabisa. Nidhamu ni msingi muhimu sana kwako
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kujijengea Nidhamu Ya Fedha Na Kuifanya Ikuzalishie Zaidi.
8. Uadilifu.
Tekeleza kile ambacho umeahidi kutekeleza, kuwa na tabia njema, mbele za watu na hata kwako binafsi pia.
Sasa hivi wewe kama kijana kuna vitu viwili ambavyo unamiliki, tabia yako na juhudi zako. Ukicheza na chochote hapo umekwenda na maji. Tabia yako inapokuwa nzuri, utavutia fursa nyingi sana upande wako.
Halafu huu ni wakati mzuri sana wakuwa na tabia nzuri, maana watu wenye tabia nzuri wamekuwa adimu sana. Usiwe mwongeaji tu, kuwa mtu wa vitendo. Na usiibe, wala kudhulumu, hata kama kila mtu anafanya hivyo.
9. Marafiki.
Hawa sasa unaweza kuhitaji kuwabadili, hasa kama hawaendani na maisha uliyochagua. Kama marafiki ulionao sasa ni wa kuitana kwenye bata, kuambiana ni viwanja gani vikali, kushawishiana kufanya mambo ya kuonekana, hawa hawakufai. Kuendelea kuwa nao, watakukatisha tamaa na kukurudisha nyuma. Utakapoanza kutekeleza hayo hapo juu watakuambia umebadilika, watakuambia unapotea, watakuambia unakimbilia wapi.
Usiwasikilize, hawajui wanaloongea, bado wapo kwenye giza, wewe umeshaiona nuru, usiipoteze. Ni wakati sasa wa kutengeneza marafiki wapya ambao watakuwa chachu kwako kufanyia kazi ndoto yako. marafiki ambao wana mtizamo sawa na huo ulionao wewe na hivyo mkaweza kwenda pamoja.
Kama unaona huwezi kupata marafiki wa aina hiyo, au hujui pa kuwapata, nimekupa njia rahisi ya kuwapata hapo chini.
10. Kujifunza.
Jifunze kila siku, angalau hiki ndio kitu ambacho utatakiwa kukifanya kila siku kwa siku zote za maisha yako. jifunze kuhusu kile ambacho unafanya kwa sasa, jifunze kuhusu ndoto zako unazotaka kufikia kwenye maisha yako.
Pia jifunze kuwa chanya na kuzitumia fursa zinazokuzunguka. Na njia bora ya kujifunza kila siku ni kupitia AMKA MTANZANIA  na KISIMA CHA MAARIFA. Kila siku unapoamka tembelea mitandao hiyo miwili, kuna kitu kipya utajifunza, na kama utakiweka kwenye maisha yako, basi mambo yatabadilika.
Pia kupitia KISIMA CHA MAARIFA unaweza kupata marafiki wanaoendana na ndoto zako. Unapata marafiki hawa kama ukijiunga na kuwa mwanachama, ambapo unapata nafasi ya kuingia kwenye kundi la wasap ambalo lina watu wengi wenye mtizamo chanya wa kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha. Karibu sana. Kama ungependa kuwa sehemu ya kundi hili na kuzungukwa na watu chanya, nitumie ujumbe kwa wasap kwenye namba 0717396253.
Hayo ni mambo kumi muhimu sana kati ya mengi ambayo unatakiwa kuyajua unapokwenda kuanza safari hiyo ya kujitegemea. Yote niliyokushirikisha hapo juu nilianza kuyafanya na mpaka sasa bado ninayafanya, na maisha yangu yanazidi kubadilika na kuwa bora zaidi kila siku. Nakusihi sana wewe kama kijana mwenzangu uchukue hatua sasa, hakuna linaloshindikana kama kweli umeamua.
Nakutakia kila la kheri katika safari hii ya kipekee unayokwenda kuianza kwenye maisha yako.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
+255 717 396 253