Tangu tunakua, tumejengewa tabia ya kuzoea kile ambacho tunacho kila siku, na kutokukipa thamani kubwa. Lakini kile ambacho hatuna kila siku, kile ambacho tunakiona au kukipata mara chache sana, huwa tunakipa thamani kubwa.

Gharama ya madini yanayotumika kwenye urembo au mapambo, haitokani sana na utofauti wa madini hayo, bali upatikanaji wake. Madini ambayo ni rahisi kupatikana bei yake ni rahisi, na yale ambayo ni adimu kupatikana bei yake ni ghali.

Kwa mfano chuma ni madini, na dhahabu ni madini. Utaona watu wamevaa cheni za dhahabu na sio za chuma, hii ni kwa sababu dhahabu inapewa thamani kubwa kuliko chuma, na hii inatokana na kwamba ni vigumu kupata dhahabu kuliko kupata chuma.

Na hata kwenye familia hili lipo, watu wa familia ambao mnaonana kila siku mnaona ni kawaida na hata matumizi yanakuwa ya kawaida. Akija mgeni mambo yanabadilika haraka sana. Kuna matumizi mengine ya ziada yatafanywa kwa sababu tu ya mgeni.

Hivyo tumelibeba hili kwenye kila jambo, kama ni kitu ambacho kipo kila siku, hakuna tatizo, hatusumbuki sana. Kama ni kitu ambacho kinaonekana mara chache basi tunasumbuka.

Vibaya zaidi tumepeleka hili kwenye muda pia. Kwa kuwa muda tunao kila siku, basi tunaona ni kitu cha kawaida, hatuupi thamani kubwa kwa sababu tunajua kesho ipo na kesho yake pia.

Lakini tunasahau kwamba hakuna kitu adimu kama muda, muda ulionao leo hutakuja kuupata tena kwenye maisha yako. hivyo ni vyema kuutumia vizuri na kuupa thamani kubwa ili uweze kufanya makubwa.

Muda wako una thamani kubwa sana, hasa kwenye kufikia mafanikio yako. dakika moja unayopoteza leo, huwezi kuipata tena, hata ungekazana kiasi gani. Anza sasa kubadili jinsi ambavyo unauchukulia muda, acha kufikiri unao wa kutosha sana na badala yake ona uhalisia ambao ni muda unapotea kwa kasi sana.

SOMA; Jinsi ya kutengeneza bajeti ya matumizi mazuri ya muda wako kama mjasiriamali.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba nimekuwa sivipi thamani vitu ninavyokuwa navyo kila siku. Na hatari kubwa ninayofanya ni kutoupa muda thamani kubwa. Hii inapelekea mimi kuona muda bado upo wakati muda unamalizika. Kila dakika inayopita ndiyo imeshapotea, hairudi tena. Kuanzia sasa nitaweka thamani kubwa kwenye muda wangu, sitaupoteza tena.

NENO LA LEO.

“The bad news is time flies. The good news is you’re the pilot.” – Michael Altshuler

Taarifa mbaya ni kwamba muda unapaa. Na taarifa nzuri ni kwamba wewe ndiye rubani.

Utakuwa rubani mzuri wa muda wako kama utajua thamani ya muda huo na kujua vipaumbele vya maisha yako. vinginevyo utaishia kwenye maafa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.