Kuna mbinu nyingi sana za kushinda vita, lakini kuna moja ambayo ni muhimu zaidi.

Mbinu hiyo muhimu sana ni kujua wakati gani wa kushambulia na wakati gani sio wa kushambulia.

Wakati mzuri wa kushambulia ni pale ambapo unaona adui ni dhaifu au kuna madhaifu ya adui ambayo umeshayajua.

Wakati ambao sio mzuri wa kushambulia ni pale ambapo hujamjua adui yako vizuri, au adui ana nguvu kuliko wewe, yaani amekuzidi kwa kila kitu. Hauachi kabisa kushambulia, bali unajipanga vyema pamoja na kutafuta eneo ambalo adui ni dhaifu.

Najua huendi kupigana vita, sasa kwa nini nakwambia haya?

Kwa sababu kuna vita nyingi zinaendelea kwenye maisha yako.

Wewe kuweza kufikia malengo yako ni vita. Ni vita kwa sababu kuna maadui wengi ambao wanakuzuia na kukurudisha nyuma.

Wewe kuweza kubadili tabia mbaya ambazo hazikupeleki kwenye mafanikio ni vita. Ni vita kwa sababu tabia ambazo tayari umejijengea ni ngumu sana kuzing’oa.

Hapa ndipo unahitaji mbinu za kivita ili kuweza kufikia malengo, au kuondokana na tabia na uweze kufikia mafanikio makubwa.

Kwenye kufikia malengo yako, anza kufanyia kazi yale maeneo ambayo umeshayajua vizuri, yale ambayo ni rahisi kwako kuanza na endelea kukua kwa kuanzia hapo. Usitake kuanza na makubwa sana, ndiyo unahitaji kuwa na malengo makubwa, ila unapoanza, anza kidogo.

Kwenye kuondokana na tabia mbaya, jua udhaifu na uimara wa tabia hiyo mbaya uko wapi. Kama ni ulevi basi jua uimara wa tabia hiyo labda upo kwa marafiki zako, unapokutana nao ni lazima ulewe. Na udhaifu wa tabia hiyo upo kwenye kuchagua kufanya kitu ambacho kitakuweka bize sana. Kwa njia hii unaweza kuepuka yale maeneo ambapo tabia hiyo ipo imara, na kwenda kwenye yale maeneo ambapo tabia hiyo ina udhaifu.

SOMA; Kama Maisha Ni Vita, Basi Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kujua.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba ili niweze kufikia malengo yangu nahitaji kuanza na yale maeneo ambayo ni madogo na yanawezekana kwangu, na niendelee kukua kuanzia hapo. Najua pia kuondokana na tabia mbaya nahitaji kuepuka yale maeneo yanayochochea tabia hiyo na kuenda maeneo ambayo tabia hiyo inakosa kichocheo. Nitazingatia haya ili niweze kuondokana na tabia zisizo bora na kufikia malengo yangu.

NENO LA LEO.

Do the difficult things while they are easy and do the great things while they are small. A journey of a thousand miles must begin with a single step.

Lao Tzu

Fanya vitu vigumu wakati bado ni virahisi na fanya vitu vikubwa vikiwa bado ni vidogo. Safari ya maili elfu moja inaanza na hatua moja.

Fanyia kazi malengo yako kwa kuanza na vile ambavyo ni rahisi kufanya, na kuanza kufanya vidogo vidogo ambavyo baadae vitakuwa vikubwa sana.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.