Hadithi inakwenda kwamba mama mmoja alikuwa anakata samaki mkia kabla ya kumkaanga. Binti yake alikuwa akiona hilo kila siku ila hakuelewa kwa nini. Basi akaamua siku moja amuulize mama yake. “mama kwa nini unamkata samaki mkia kabla ya kumkaanga?” mama akamjibu bibi yako alikuwa anafanya hivyo. Basi ikabidi mama amigie simu bibi kumuuliza, bibi yule naye akamwambia mama mtu, bibi yako alikuwa anafanya hivyo. Basi kumaliza mzizi wa fitna ikabidi wampigie yule bibi kizee, kwa bahati nzuri alikuwa bado hai, wakamuuliza kwa nini ulikuwa unakata mkia wa samaki kabla ya kumkaanga? Bibi akajibu, “nilikuwa nakata mkia wa samaki kwa sababu kikaangia changu kilikuwa kidogo na samaki asingeweza kuenea”
Vizazi viwili vimekuwa vikifanya jambo lile lile kila siku, kwa kushindwa kujiuliza swali rahisi sana ambalo wewe utapata nafasi ya kulijua hapa.
Ni rahisi sana kwenda na maisha kama yanavyokwenda, yaani pale ambapo tunakuwa tumeanza kufanya kitu, na tabia ikajijenga kwenye kufanya kitu hiko, basi baada ya hapo huwa tunaendelea kufanya kwa sababu tumezoea kufanya.
Mambo mengi tunayoyafanya kwenye maisha yetu ya kila siku tunafanya kwa mazoea, labda tumeona wengine wakifanya hivyo au tuliwahi kufanya hivyo awali tukapata matokeo mazuri. Kunaweza kuwa na njia bora zaidi za kufanya kile tunachofanya lakini hatuzijui kwa sababu kuna swali tunasahau kujiuliza.
Mambo mengi tunayofanya kwenye maeneo yetu ya kazi ni kwa sababu tumekuwa wengine wanafanya hivyo, au tulielekezwa kufanya hivyo. Kunaweza kuwa na njia bora zaidi za kufanya kazi, lakini hatuzitumii kwa sababu hatujawahi kujiuliza swali moja muhimu sana.
Inawezekana pia imani ya kidini uliyonayo sasa, upi nayo kwa sababu ndiyo wazazi wako walikulea kwa imani hiyo, hujawahi kukaa chini na kujiuliza swali muhimu ambalo litaboresha zaidi imani yako.
Swali muhimu sana unalopaswa kujiuliza leo na kila siku ni KWA NINI?
Chochote unachofanya, na kwa njia yoyote unayofanya, jiulize kwa nini?
Kwa nini unafanya kazi unayofanya, kwa nini unapita njia unayopita, kwa nini unaamini unachoamini?
Jiulize kwa nini kwenye kila jambo ambalo unafanya na kwa swali hili utahitaji kufikiri zaidi, na unapofikiri ni lazima utakuja na majibu bora sana.
KWA NINI ni swali ambalo litachokoza fikra zako na fikra zako zimejaa busara kubwa sana itakayokuwezesha kutatua changamoto yoyote na kuboresha maisha yako?
Kwa nini? Jiulize swali hili kila siku, kila mara na kila wakati. Litakulazimisha ufikiri zaidi.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mambo mengi ninayafanya kwa mazoea, na chochote kinachofanyika kwa mazoea hakiwezi kuwa bora. Nimejifunza pia swali la KWA NINI ni swali ambalo linachokoza fikra zangu na kunifanya nijue kwa undani juu ya kile ninachofanya. Kuanzia sasa nitakuwa najiuliza swali KWA NINI kwenye jambo lolote ninalofanya au kupitia, kila siku, kila mara na kila wakati.
NENO LA LEO.
Thinking is the hardest work there is, which is probably the reason why so few engage in it.
Kufikiri ndio kazi ngumu kuliko zote duniani, ndio maana watu wachache sana wanaifanya.
Mara zote jiulize swali KWA NINI kwenye chochote unachofanya, swali hili litakusukuma ufikiri zaidi. Na unapofikiri unapata mengi zaidi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.