Habari za wakati huu rafiki?
Karibu tena kwenye mazungumzo yetu haya kati yangu mimi na wewe rafiki yangu. Ni muda mrefu hatujapata nafasi ya kufanya mazungumzo haya, tangu mwaka huu uanze. Nimekuwa na mambo mengi kidogo tangu mwaka umeanza, tumefanya semina ya malengo kwa njia ya mtandao ambayo imekuwa na mafanikio makubwa sana. Kwani washiriki wote wameondoka na malengo makubwa na wanayokwenda kufanyia kazi.
Pia nimehariri na kutoa kitabu cha KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO ambacho ni kitabu kinachobeba kurasa 366 za siku zamwaka huu 2016 ambapo kila siku unakuwa na kitu cha kufanyia kazi. Kama bado hujapata kitabu hiki basi kipate mapema ili mwaka huu usipotee tena kama miaka mingine ya nyuma.
Pia tumeendelea kujifunza na kuhamasika kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo kwa sasa nafasi za kujiunga zimeongezeka zaidi. Awali ilikuwa nafasi 100 tu kutokana na sheria ya kundi la wasap ambapo mwisho ilikuwa watu 100. Kwa sasa wasap wameongeza idadi ya watu wanaoweza kuwa kwenye kundi na kufikia 256, hivyo kuna nafasi kama 150 za kuweza kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kujiunga na KISIMA unapata nafasi ya kusoma makala zilizopo kwenye mtandao wa KISIMA CHA MAARIFA na pia unapata nafasi ya kuwa kwenye kundi la wasap ambapo utajifunza mengi zaidi kutoka kwa watu wengine wenye mtizamo chanya wa kimaendeleo. Kila siku utapata tafakari nzuri ya kuianza siku yako ukiwa chanya na kwenda kuweka juhudi zaidi.
Ninachoweza kusema ni kwamba kama mpaka sasa haupo kwenye KISIMA unakosa mengi na huenda ukapoteza tena mwaka huu 2016. Jiunge sasa na KISIMA ili uwe karibu na watu ambao wanajua ni wapi wanakwenda. Tatizo la jamii zetu zimejaa watu ambao hawajui ni wapi wanakwenda.
Taarifa muhimu;
Kutakuwa na mabadiliko kidogo kwenye mazungumzo yetu haya, mwaka jana tulikuwa na mazungumzo haya mara mbili kwa wiki, yaani jumanne na alhamisi. Mwaka huu mazungumzo haya yatakuwa mara moja kwa wiki, yaani jumanne na siku ya alhamisi nitakuwa nakutumia ujumbe wowote mzuri, huenda wa kukupa hamasa zaidi au kukushirikisha taarifa za mafunzo, vitabu na kadhalika. Mwaka huu natarajia kuchapa vitabu viwili, hivyo naweka muda kwenye kuandika na kuhariri vitabu vitakavyochapwa. Jiandae kusoma vitabu hivi pia.
Kitu kingine muhimu, ili kuweka mazungumzo haya yaendelee kuwa hai na ya kuhamasisha, naomba uwe unafungua na kusoma kila jumanne na alhamisi. Na muhimu zaidi uwe unajibu email hizi. Ninasoma na kujibu kila email unayonitumia kwa sababu nathamini sana muda wako unaotumia kuniandikia. Naomba pia na wewe uwe unajibu kwenye kila mazungumzo unayopokea, chochote utakachojibu iwe ni kuongeza au kuuliza swali, kutanipa hamasa ya kujua tupo pamoja na hivyo kuendelea kuandaa mazungumzo mazuri zaidi.
Baada ya hayo machache naomba nikushirikishe mazungumzo yetu ya leo ambapo tunakwenda kuangalia kwa ndani tabia zetu sisi wanadamu.
Kuna tabia moja ambayo imekuwa inatuingiza kwenye matatizo, na kutunyima fursa. Kwa tabia hii ambayo kila mmoja wetu anayo, umekuwa unajipa msongo wa mawazo, kujijaza chuki na hata kushindwa kuchukua hatua ya kuboresha maisha yako.
Tabia tunayokwenda kuzungumzia leo ni tabia ya KUTAFUTA SABABU. Sisi binadamu ni viumbe wa kutafuta sababu. Kwa jambo lolote linalotokea, huwa hatuliachi hivi hivi, ni lazima tutafute sababu. Na mara nyingi huwa sababu hizi hatuzipati kwa jambo husika, bali tunazitengeneza sisi wenyewe kwa fikra zetu na hisia zetu. Na hapa ndipo matatizo mengi sana yanapoanzia.
Kwa mfano, umepishana na mtu ambaye mnafahamiana, ukamsalimia na hakuitika. Ni mawazo gani yanayokuja kwenye akili yako? haraka sana utaanza kutengeneza sababu. Nimemsalimia hajaitika, labda ni kwa sababu hanipendi, labda kwa sababu ananionea wivu, labda kwa sababu nilifanya kitu fulani, utaendelea kujijaza sababu nyingi sana. Cha kushangaza sababu zote zitakuwa hasi na hutapata kabisa nafasi ya kufikiria sababu moja ambayo inaweza kuwa sahihi kuliko zote. Labda hajakusikia, au ana mawazo mengi, au ana matatizo yake binafsi. pamoja na yote, huhitaji kutafuta sababu. Wewe umemsalimia mtu hakuitika, basi endelea na ulichokuwa unafanya, wakati mwingine msalimie tena, na utaona sababu zote ulizokuwa unatengeneza mwanzo hazikuwa sahihi. Huu ni mfano unaotengeneza matatizo kwa wengi, na kuna hali tofauti tofauti za mfano wa aina hii.
Mfano mwingine ni pale ambapo mtu anakuwa amefanikiwa, kukushinda wewe, japokuwa mtu huyo alikuwa na hali ngumu au mlikuwa na hali sawa. Labda mnafanya biashara moja, au mnafanya kazi pamoja. Unashangaa mwenzako mambo yake yanakwenda vizuri lakini wewe kila siku una changamoto. Haraka sana unakimbilia kwenye sababu. Yeye ana maisha mazuri kwa sababu alitokea familia nzuri, au hana majukumu kama niliyonayo mimi, au ana bahati kwenye mambo fulani, au anapendelewa au anatumia nguvu za giza. Utajipa sababu nyingi sana, zote za kuiridhisha nafsi yako. lakini hakuna sababu hata moja itakayokuwa ya kweli au itakayokusaidia wewe kutoka hapo ulipo. Na cha kushangaza una nafasi ya kuwa karibu na mtu huyo na akakushirikisha ni jinsi gani unaweza na wewe kuwa na maisha bora. Lakini hutaki kwa sababu utavuruga sababu zako. Huu ni mfano wa jinsi sababu zinavyokunyima fursa, na kuna aina nyingi za hali kama hiyo.
Ufanye nini sasa?
Kama umefuatilia hiyo mifano vizuri, utaona ya kwamba huwa tunatafuta sababu ambazo zinaendana na sisi, ambazo zinaturidhisha sisi, na kutufanya tuone tupo sahihi zaidi ya wengine. Kote huku ni kujidanganya, na kujirudisha nyuma.
Kitu kikubwa cha kufanya ni kuacha kutafuta sababu, hasa zile zinazotoka ndani yako mwenyewe, zinazokufurahisha. Badala yake tafuta ukweli wa mambo. Kwa mifano yetu hiyo hapo juu, umemsalimia mtu hakuitika, unaweza kumfuata baadaye akiwa ametulia na kumwuliza ulimsalimia lakini hakuitika, kuna tatizo lolote? Na atakuambia ukweli, labda hakukusikia, au mawazo yake yalikuwa mbali, au atakuonesha kwamba ana tatizo na wewe. Kama kuna mtu ulikuwa unamwona wa kawaida ila sasa mambo yake yananyooka sana, mtafute na fanya naye mazungumzo, mwulize ni ipi siri ya mambo yake kwenda vizuri, watu hawa watakueleza kila kitu.
LAKINI…..
Lakini hutafanya hivyo kwa sababu utaona kufanya hivyo ni kujishusha, utaona ni kujipendekeza na mengine mengi utakayoendelea kujidanganya. Na hivyo utaendelea kujikusanyia sababu zako zisizo za msingi, na utaendelea kutengeneza matatizo na kuzikosa fursa.
Maisha ni yako, chaguo ni lako.
Je ni namna gani umekuwa unatengeneza sababu? Nishirikishe kwa kuweka maoni yako hapo chini, nipe pia mfano kama unao wa mahali umewahi kujipa sababu halafu ukaja kugundua haikuwa kweli. Tushirikishane ili kujifunza zaidi.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
asante kocha kwa kupata nafasi ya kuongea nawe,ulichozungumza kocha kimenigusa sana hasa kipengele cha kumsalimia mtu na hakuitikia ilikuwa inanipa maswali mengi ambayo nilikuwa nakosa majibu,
mwisho niliamua nilie msalimu na hakuitikia tukikutana tunapishana tu simsalimu,mpaka atakapo anza yeye kunisalimu nami nikimkuta nitamsalimu.
Nashukuru sana kocha kwakunifungua katika kifungo sikuwa najua sababu,nimejua nilikuwa nikijipa sababu za uwongo tena zenye mtazamo hasi, nitazingatia kwa umakini yote niliyojifunza kupitia mazungumzo yako nami.
Asante kocha.
LikeLike
Karibu Erick,
Vizuri sana kwa kujifunza na kupanga kuchukua hatua.
Kila la kheri.
LikeLike
Hahahahahahaha kweli kabisa kocha!
Hilo swala la kujipa sababu lipo sana.
Kumekuwa na tabia ya watu kutochukua hatua muhimu katika maisha kwa sababu tu ya kujipa sababu. Na hilo linaweza kutokea kwa kusikiliza maneno ya watu pia.
Mfano: Utamsikia mtu akisema siwezi kumpeleka mtoto wangu shule fulani kwa sababu nasikia wanatumia nguvu za giza. Hapo tayari amejipa sababu ya kutompeleka mtoto wake shule nzuri kwa kujipa sababu za kusikia kwa watu na si kwamba amefanya uchunguzi.
Mfano: 2
Mtu anashindwa kufanya biashara fulani(hasa hizi za mitandao) kwa kuamini kwamba ni za kifreemason,anakupa na sababu kabisa,mtu hawezi kukulipa hivi hivi lazima kuna jambo hapo!
Hivyo ametafuta sababu ya kutojikwamua kiuchumi kwa sababu ya imani zake,badala ya kufanya uchunguzi ajue hzo hela zinapatikana vipi!
Mimi binafsi nilikuwa napenda sana kujipa sababu za kutoamka mapema asubuhi! Kama,kwanza mvua inanyesha siwezi kuamka,sasa je walioamka si watu/binadamu!?!
Au mtu akiniuliza nitasema sijisikii vizuri ndo maana bado nimelala,kihalisia sio kweli ila ni sababu tu ya kutoamka,na ikiwezekana wanionee huruma niendelee kulala.
Sababu zipo nyingi sana! Ila nimeshea hzo chache!
Ahsante.
Sekela K M
LikeLike
Asante sana Sekela kwa mifano hii hai uliyotushirikisha hapa.
Ni kweli kabisa hasa kwenye biashara ya mtandao, wengi wamekuwa wakijipa sababu, lakini kwa undani hawajui.
Kikubwa ni tuweke sababu hizi pembeni na tutafute ukweli wenyewe.
TUPO PAMOJA.
LikeLike
hapo kwenye sababu kweli huwa na mimo nakosea ola nimejirekebisha
LikeLike
Vizuri sana Geofrey kwa kujifunza na kuamua kujirekebisha.
Kila la kheri.
LikeLike
Ahsante kocha umenifungua zamani niliujua kupata maisha mazuri ni mpaka uwe na kiwango fulani cha ngazi za elimu
Nilijijzuia kubeba majukumu fulan ya maisha yangu mapema nikiamin bado kwa umri wangu na wapo wanaohusika na kujali hatamu ya maisha yangu
Nikimin huwez kusoma ukiwa na mke ni vigumu kufanya masomo wakati una ndoa malijza masomo uoe
Hzo ni baadh ya sababu nilikuwa njhkijiambia
LikeLike
Vizuri Hendry kwa kujifunza,
Sasa chukua hatua sahihi.
Kila la kheri.
LikeLike