Watu wote ambao ni waongo sana leo, hawakuanza kuwa waongo wakubwa siku moja, walianza kidogo kidogo na hatimaye wakajikuta katikati ya uongo mkubwa.

Watu wote ambao ni wezi na matapeli wakubwa leo, hawakuanza wakiwa wezi na matapeli, walianza kidogo na kwa nia njema sana.

Watu wote ambao ni walevi wakubwa leo, hawakuanza wakiwa walevi, walianza kwa kutumia kilevi kwa kiasi kidogo sana, na kwa nia njema.

Kuna mtego ambao upo kwenye kuanza kutumia kitu, hasa hivi vitu ambavyo sio bora kwetu kwa baadaye. Mtego huo ni ile fikra kwamba nafanya mara moja tu, na sitarudia tena. Na kweli mtu anafanya mara moja, lakini kwa matokeo mazuri ambayo anayapata, anashawishika kurudia tena.

Unaanza na uongo kidogo, na watu wanauamini, na wewe unaona hah kumbe watu wanaamini uongo huo? Siku nyingine unadanganya tena, na watu wanaamini. Sasa unapodanganya hivi ili uongo wa mwanzo usijulikane, unaendelea kudanganya tena, na hapa unatumbukia kwenye shimo la udanganyifu, na siku moja watu wanajua kila kitu.

Unaanza kwa kuiba kidogo, na kweli unafanikiwa, na unaona kumbe inawezekana kupata kirahisi hivi? Wengine wanakazana na kuumia lakini mimi ni mjanja, nimeweza kupata kirahisi. Unarudia kuiba tena na ukija kustuka umeshakuwa mwizi uliyebobea.

Unaanza kwa kutumia kilevi kimoja, kutaka kuondokana na mawazo au kujipumzisha, na unapata utamu wake. Siku nyingine unajaribu tena na unazoea kabisa, baadaye unaishia kuwa mlevi.

Tunachojifunza hapa leo, kabla hujaanza kufanya jambo lolote, jiulize je baadae linaweza kukujengea tabia gani? Kama tabia hiyo siyo nzuri kwa mafanikio zaidi ya baadaye basi achana kabisa na kufanya kitu hiko. Usijidanganye kwamba ni mara moja tu, utajitumbukiza kwenye shimo ambalo sio zuri kwako.

Na kama tayari umeshaingia kwenye shimo, acha kuendelea kuchimba. Amua sasa ya kwamba unaachana na hayo unayofanya na unaanza kunyoosha maisha yako. kwa maamuzi haya utaweza kuzivuka changamoto utakazokutana nazo.

NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

SOMA; SIKU YA 21; Sheria Za Asili Zitakazokuletea Utajiri Na Mafanikio.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba wote ambao wameishia kwenye mambo mabaya, hawakuanza wakiwa na mambo hayo mabaya. Bali walianza wakiwa watu wema na wakajaribu kukunja kona kidogo. Lakini baada ya kukunya kona hiyo hawakuweza kurudi tena. Mimi nimeamua kutokukunja kona kwenye jambo lolote lile. Na katika yale mambo ambayo nimeshakunja kona nitaondoka na kurudi kwenye mstari.

NENO LA LEO.

We are all born as empty vessels which can be shaped by moral values.

Jerry Springer

Tunazaliwa tumiwa watupu na tunatengenezwa kwa maadili.

Chagua maadili ambayo yatakufikisha kwenye mafanikio makubwa, usijaribu kukata kona, utapotea kabisa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.