Kama kuna eneo muhimu kwenye maisha yetu, ambalo limesahaulika sana ni ukuaji wa kiroho. Tunajali kuhusu afya zetu za mwili, na kujali kiasi kuhusu afya za akili, lakini tunasahau kuhusu afya ya kiroho.
Kila mmoja wetu ana maisha yake ya kiroho, bila ya kujali dini aliyonayo, kabila analotokea au nafasi yake kwenye maisha anayoishi. Ni maisha haya ya kiroho ambayo ni muhimu sana katika kukamilisha maisha bora na yenye mafanikio makubwa.
Kwa nini ni muhimu sana kuwa na ukuaji wa kiroho?
Maana kubwa ya maisha yetu inaanzia kwenye maisha ya kiroho. Tukishatimiza yale ya msingi, yaani kuhakikisha tupo hai, kwa kupata chakula na malazi na mavazi, kinachofuatia sasa ni kwa nini tunaishi. Kama utakumbuka kuna wakati watu walikuwa wakijadiliana TUNAKULA ILI TUISHI AU TUNAISHI ILI TULE? Kwa jibu lolote, kuhusu kula bado hakuna muunganiko wa karibu na maana kubwa ya maisha yako.
Mahitaji ya msingi yakishatimizwa, hapa ndipo maisha yatakapoanza kukudai kile kikubwa zaidi ambacho mpaka sasa bado hujakitoa.
Inawezekana kwa sasa unasukumwa zaidi na fedha, kwa sababu fedha ndicho unachohitaji sana katika maisha yako kwa sasa. Kama huna uhakika wa kesho, au kama unaishi mwezi kwa mwezi kama ambavyo wengi wanaishi, kwakupata mshahara, kulipa madeni na hatimaye kuanza kukopa tena, kwa hakika utakuwa tayari kufanya chochote ili kupata fedha.
Kama unafanya biashara ambayo faida unayoipata ndiyo inayoendesha faida, na hivyo biashara hiyo inasua sua, utakuwa tayari kufanya biashara yoyote kama tu inakuingizia faidia.
Lakini kama umechagua kuishi maisha ya mafanikio, kama ambavyo tunajifunza kwenye KISIMA CHA MAARIFA na AMKA MTANZANIA, hutabaki hapo kwa muda mrefu, utafika wakati ambao sio mrefu sana, ambapo fedha itaacha kuwa ndio hitaji muhimu sana kwenye maisha yako. pale utakapofikia uhuru wa kifedha, ya kwamba hata usipofanya kazi bado una uhakika wa kuishi, ndipo utakapoanza kuona ombwe kubwa kwenye maisha yako kama utasahau ukuaji wa kiroho sasa.
Ukuaji wa kiroho ni muhimu sana kwenye maisha yetu kwa sababu ni kupitia maisha ya kiroho ndipo tunasukumwa kufanya kile ambacho ni muhimu sana kwetu na kwa wengine pia. Maisha haya yanatupa maadili ya kujua kipi ni bora kwetu kufanya na kipi sio bora. Maisha haya yanatuwezesha kuchagua kati ya mema na mabaya na kuweza kuyasimamia hata kama dunia nzima inakwenda kinyume na sisi. Na maisha haya ndiyo yataleta ukamilifu kwenye maisha yetu, kama tutayaelewa na kuyazingatia.
Pia ukuaji wa kiroho ni muhimu sana kwa sababu tunapozaliwa tunakuja duniani tukiwa watupu, hatuji na maelekezo yoyote kwamba tunatakiwa kufanya nini. Kwa miaka yetu yote ya ukuaji tunazungukwa na jamii ambayo inajaribu kutuambia ni nini tunatakiwa kufanya. Tumekutana na taratibu mbalimbali ambazo nyingine ni nzuri na nyingine sio nzuri. Na kuna taratibu nyingi kama ukizifuata huwezi kufikia yale maisha ambayo ni bora kwako. Ni kupitia maisha ya kiroho ambapo unaweza kujua ni kipi unaweza kufanya vizuri sana kwenye dunia hii na kisha kuweka juhudi zako kwenye kitu hiko. Katika maisha haya ya kiroho tunajijua vizuri sisi wenyewe tunajua nguvu zetu ziko wapi na madhaifu yetu yako wapi. Na kwa njia hii tunajua ni kipi bora kwetu kufanya.
Ukuaji wa kiroho pia unatuwezesha kufikiri zaidi ya sisi wenyewe. Katika maamuzi yoyote ambayo tunayafanya, tunafikiria wengine pia wanaathirika au kunufaika vipi na maamuzi hayo. Kama tulivyoona kwenye kupigania mahitaji ya msingi hapo juu, kama huna chakula, utasukumwa kufanya chochote ili ule, utaweza kuiba, kudhulumu au kufanya chochote ili ujipatie chakula. Kwa sababu hiyo ndiyo hatua ya mwisho ya wewe kuhakikisha unaendelea kuishi. Lakini kwa maisha ya kiroho, kabla hujafanya jambo lolote unafikiria wengine pia, unaacha ule ubinafsi wa mimi nipate kwanza, au mimi nipate zaidi na kuangalia wengine nao wanapata nini, au kuhakikisha hawaumii kwa kupata kwako.
Kitu kingine kikubwa sana ni kupambana na changamoto za kila siku za maisha. Umewahi kuona watu wawili wanapata tatizo moja, labda wote wamefukuzwa kazi, mmoja anaendelea na mambo yake mengine na mwingine anakata tamaa kabisa, anakuwa mlevi au hata anafikia kujiua? Jinsi tunavyokabiliana na changamoto za maisha ya kila siku, inategemea sana na ukuaji wetu wa kiroho. Wale ambao bado ni wachanga kiroho wanapokutana na changamoto wanaumizwa sana, wanaweza kukata tamaa au kuchukua hatua ambazo sio bora kwao. Wale ambao wamekomaa kiroho wana uwezo wa kuhimili changamoto yoyote wanayokutana nayo na kuendelea kuweka juhudi. Hawa wanakuwa wanajua ya kwamba chochote wanachokutana nacho, kama hawajafa basi sio mwisho wa dunia, na wana nafasi ya kuendelea kuweka juhudi na kupata chochote wanachotaka.
Ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuweka juhudi kwenye ukuaji wa kiroho, kwa sababu mwisho wa siku, baada ya kupata chochote tunachotaka, maisha yako ya kiroho ndiyo yatakayokuletea ukamilifu kwenye maisha yako. siku utakapokuwa unavuta pumzi yako ya mwisho, hutahesabu ni magari au nyumba nyingi kiasi gani umekuwa nazo, hutahesabu ni fedha kiasi gani ulikuwa nazo benki, na wala hutahesabu ni maeneo mengi kiasi gani uliwekeza. Bali utajiuliza kama maisha yako yalikuwa na msaada kwa wengine, na kama maisha yako yalikuwa na maana kubwa kwako.
Tusisahau eneo hili muhimu sana katika juhudi zetu za kuwa na maisha bora. Nakutakia kila la kheri katika kutafakari maisha yako ya kiroho.
Katika makala ijayo ya FALSAFA, tutaangalia hatua za kuhakikisha tunakuwa na ukuaji wa kiroho.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,