Kile kitu unachotaka kuficha, ndicho ambacho dunia inataka kuona. Na hii ni kwenye kazi, biashara na hata maisha.

Kuna vitu vingi ambavyo unajua unataka kufanya, lakini kwa sababu vitu hivyo ni vipya na hujawahi kufanya tena, unakuwa na hofu kubwa. Kwa kuwa na hofu hii unalazimika kuficha kile ambacho ulitaka kufanya.

Kwa upande wa pili, vitu hivi unavyoficha, vitu hivi ambavyo hupo tayari kufanya, ndivyo vitu ambavyo dunia inavitaka sana, ndio vitu ambavyo dunia inasubiri mtu anayeweza kuvifanya. Na kama akitokea mtu huyo basi dunia itakuwa tayari kumpa kile anachotaka.

Mara kwa mara umekuwa na mawazo ya uboreshaji wa biashara yako, mawazo ambayo kama ukiyatekeleza biashara yako itakuwa bora sana. Lakini tatizo ni kwamba hakuna ambaye amewahi kufanya mawazo hayo, na hivyo unahofia na kuficha, unaiacha dunia ikiwa na kiu.

Umekuwa na mawazo ya kuboresha sana kazi unayofanya, mawazo ambayo yataleta kitu cha tofauti ambacho anayepokea kile unachofanya atakuwa bora sana. Lakini kwa hofu unaogopa kutekeleza mawazo hayo na kuyaficha.

Fikiri ni vitu vingapi ambavyo ulifikiri unahitaji kufanya, na ukaogopa, ukaficha. Baada ya muda ukaona mtu mwingine akifanya kitu hiko na watu wengi wakanufaika nacho. Au kitu uliacha kufanya na baadae ukaja kufanya na watu wakanufaika sana?

Kama kuna kitu unajua unataka kufanya na unajua kitawanufaisha wengi hata kama ni kipya na hata kama unapata hofu ya kukifanya, usikubali kukificha, wewe fanya, kwa sababu dunia inakisubiri sana kitu hiko.

SOMA; Usihofu Kama Watu Watachukia…

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba vitu ambavyo nataka kuvificha ndivyo vitu ambavyo dunia inavitaka sana. Nimekuwa nakubali hofu ya kufanya mambo mapya kunirudisha nyuma. Kuanzia sasa sitakubaliana tena na hofu hii kwa sababu nina uhakika watu wengi wanasubiri kile kipya ambacho nakwenda kufanya.

NENO LA LEO.

“Our job in this life is not to shape ourselves into some ideal we imagine we ought to be, but to find out who we already are and become it.” ― Steven Pressfield

Jukumu letu kwenye maisha sio kujibadili na kuwa kama vile tunavyofikiri tunatakiwa kuwa, bali kujua vile tulivyo na kisha kuwa hivyo.

Kuna vitu vingi vikubwa unavyoweza kufanya kwenye maisha yako, ila unavificha kwa sababu ya hofu. Anza kuvifanya sasa, dunia inavisubiri kwa hamu.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.