Unapoanza kufanya kitu chochote kipya, na ukajitoa kukifanya kwa ubora wa tofauti kabisa, watu wataanza kwa kukusifia, lakini baada ya muda mfupi wataanza kukupuuza, yaani kutojali sana kile unachofanya.

Na pengine watakuambia una wazo zuri lakini kwa hapa haliwezekani, au kuna wengine walianza kama wewe lakini walishindwa. Au unachojaribu kufanya hakitawezekana kwa mazingira haya na wakati huu.

Hivyo hawatojali, na watakachokuwa wanasubiri ni pale utakapoanguka ili wakamilishe utabiri wao, kwamba tulimwambia hakusikia, asingeweza na mengine mengi.

Sasa dawa ya hali hii ni moja tu, ni wewe kupuuza yale yote wanayosema, na kutojali kutokujali kwao na badala yake kuendelea kuweka juhudi kubwa sana. Kuendelea kufanya kwa ule ubora uliotazamia kufanya, kuendelea kuwa na ndoto yako kubwa.

Na kama utaenda na hilo, bila ya kukubali kurudishwa nyuma na kitu chochote, itafika mahali hawataweza tena kukupuuza, wataanza kujali kwa sababu utabiri wao haujaweza kufanya kazi. Na pia wanapitwa na vitu vizuri ambavyo wewe unavitoa.

Jukumu lako wewe ni kuendelea kuweka juhudi, kuendelea kuweka ubora wa hali ya juu mpaka wale wenye wasiwasi na wewe waache kuwa na wasi wasi na wale ambao hawajali waanze kujali. Wakati unaendelea kuweka juhudi sio kwa sababu unataka wajali, bali kwa sababu ndiyo kitu ambacho umechagua kufanya.

Usisubiri mpaka kila mtu akupigie makofi ndio uanze kuweka ubora, anza na ubora na makofi yatakuja baadaye, na hata yasipokuja, hiyo siyo biashara yako, biashara yako ni kuzalisha kilicho bora.

SOMA; Sababu 5 Kwa Nini Ni Marufuku Wewe Kukata Tamaa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba nitakapoanza kufanya jambo lolote kubwa na bora watu wengi wataanza kunipuuza na kutokujali. Lakini kama nitaendelea kufanya bila ya kutetereka, wote wanaonipuuza wataanza kujali. Nachagua kuweka ubora kila siku sio kwa sababu nataka watu wajali, bali kwa sababu nimechagua maisha hayo. Na kutojali kwa watu sitokubali kunirudishe nyuma kwa sababu najua baadaye watajali, kama sitoacha.

NENO LA LEO.

First they ignore you, then they laugh at you, then they fight you, then you win.

Mahatma Gandhi

Kwanza wanakupuuza, kisha wanakucheka, halafu wanapambana na wewe, mwishowe unaibuka mshindi.

Usikate tamaa pale watu wanapokupuuza au kukucheka au kupambana na wewe, jua kwamba mwishoni utaibuka mshindi, kama hutaacha kufanya.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.