Kama kuna kitu ambacho unaamini ni kweli, na una uhakika kabisa ni kweli, lakini watu wengine hawakubali wala kuamini kwamba ni kweli, una njia mbili za kuwafanya wakubali na kuamini.

Njia ya kwanza ni kuwafanya wasikie, yaani kuwaambia. Na kwa sababu ukiwaambia watakubishia, basi utahitaji kubishana, na katika kubishana utahitaji kuwaeleza mengi, kuja na ushahidi w akutosha kwamba unachosema ni kweli na watu waamini. Hii ni njia rahisi kutetea ukweli, lakini tatizo ni kwamba haizai matunda, japo utabishana sana, lakini watu hawatakubali na kupokea ukweli huo. Hata kama watakuitikia kwamba wamekuelewa, lakini bado hujabadili mawazo yao, wataendelea kuamini kwamba haiwezekani.

Njia ya pili ni kuwafanya waone, hapa unafanya kile ambacho unaamini na kujua ni kweli, na unawaacha waone kwa macho yao wenyewe kwamba ni kweli kitu hiki kimefanyika na kimeleta matokeo mazuri. Hapa utafanikiwa kuwashawishi watu kwamba unachotetea ni ukweli na wao wataupokea na kuamini. Changamoto ya njia hii ni ndefu, ngumu na ina changamoto nyingi. Kwa sababu wakati unafanya, bado watakusonga kwamba haitawezekana.

Njia bora kabisa ya kubishana na kutetea ukweli wako ni kufanya, kuongea kila mtu anaweza, kutoa ushahidi kila mtu anaweza, ila kufanya na kuja na matokeo mazuri, ni wachache sana wanaoweza hivi. Na sio kwamba ni haiwezekani ndio maana wachache pekee ndio wanaweza, bali wengi hawana uvumilivu wa kuyasubiri matokeo.

Kama kuna kitu unachoamini ni kweli na ungependa wengine pia waamini ni kweli, usipigishane kelele na mtu, wewe FANYA. Na mwisho wa siku majibu yatasema yenyewe.

SOMA; Mambo Kumi(10) Muhimu Usiyojua Kuhusu Mafanikio, Na Jinsi Yanavyokurudisha Nyuma.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza ya kwamba njia bora kabisa ya kubishana na kutetea ukweli wangu ni kufanya. Kuongea kila mtu anaweza na ni vigumu kubadili misimamo ya watu. Ila kufanya na kutoa majibu mazuri ni rahisi kwa wengi kushawishika. Nitaendelea kuwa mtu wa vitendo kwa kuweka juhudi kwenye kufanya vile ambavyo ni muhimu sana kwangu.

NENO LA LEO.

People may doubt what you say, but they will believe what you do. ~Lewis Cass

Watu wanaweza kuwa na mashaka na kile unachosema, lakini wataamini kile utakachofanya.

Usikazane kupiga kelele ili watu wakuelewe, badala yake fanya, ukweli unaonekana vizuri kuliko unavyosikika. FANYA na wataona wenyewe.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.