Mambo 20 Niliyojifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha The Truth About Innovation (Ukweli Kuhusu Uvumbuzi)

Ni siku nyingine ya kujifunza mambo 20 kutoka kwenye kitabu cha wiki. Wiki hii tunajifunza kwenye kitabu kinachoitwa The Truth About Innovation (Ukweli kuhusiana na Uvumbuzi au Ubunifu). Mwandishi wa kitabu hichi anaitwa Max McKeown ambaye ni mbobevu au guru wa maswala ya usimamizi (management). Mwandishi anaelezea kweli 54 kuhusu uvumbuzi wa aina mbalimbali. Kitabu hiki ni cha muhimu kwa kila mtu anayetarajia kuwa mbunifu katika tasnia yoyote. Kitabu kinafundisha mambo mengi sana kuhusiana na uvumbuzi, kutoka kwenye mawazo hadi kuwa biashara. Chochote unachofanya usipo kuwa mbunifu au mvumbuzi lazima utapitwa na wakati, maana dunia inabadilika kila kukicha, mahitaji ya wateja ya leo sio mahitaji yao ya kesho. Soko la leo sio soko la kesho. Kwa mfano uvumbuzi wa simu, hebu piga picha kuanzia simu zilipoanza, tukianzia na simu za mezani, kisha ujio wa simu za mkononi kuanzia kwenye simu zile kubwa zenye antena kama redio, hadi leo ujio wa Smart Phone. Hakuna kinachodumu, bali UBUNIFU ndio unaodumu. Our century’s greatest innovation will be the method of innovation.

 
Karibu tujifunze
1. Baadhi ya ubunifu unategemea ubunifu mwingine au mazingira mengine. Mfano uvumbuzi wa taa ya umeme (bulb) usingekua na matumizi kama pangekua hakuna mfumo wa umeme pamoja na mifumo ya nyaya, genereta, vituo vya umeme (power stations) pamoja na makampuni ya kuendelea kutunza hivyo vitu. Pia upo ubunifu mwingine ambao sio tegemezi, aidha kwa sababu unaweza kusimama wenyewe kama wenyewe au mazingira ya kufanikiwa kwake tayari yalishakuwepo. Knowing what your idea relies on is vital to its success.
2. Shabaha (focus) za ubunifu zinatofautiana.
· Ubunifu wa bidhaa (product innovation). Huu unahusisha bidhaa mpya na sifa mpya za bidhaa za zamani. Bidhaa inaweza kua mpya, au bidhaa ile ya zamani ikawa na sifa mpya.
· Ubunifu wa mchakato (Process Innovation) – Huu unahusisha njia mpya za kufanya vitu. Bidhaa inaweza kua ni ileile, lakini njia ya uzalishaji ikawa mpya, nzuri na yenye ufanisi zaidi.
· Ubunifu wa kishirika (organizational innovation) – huu unahusisha kutafuta njia mpya za kupangilia na kusimamia watu. Hapa bidhaa na mchakato unaweza kuwa ni uleule lakini upangiliaji wa watu unabadilika.
3. Wazo zuri kamwe haliwezi kuwa kamilifu, na haliwezi kufanya vizuri kikamilifu kwenye masoko yote na misimu yote. Kwanza hakuna kitu kama wazo kamilifu la kibiashara (no perfect business idea). Kuna mawazo mazuri yenye kuhitaji kuwekewa juhudi, kuboreshwa au kuhuishwa mara kwa mara. Hivyo usidharau wazo ulilonalo kwa kigezo kwamba halijakamilika, hakunaga wazo lililokamilika. There is no such thing as the perfect business idea. Ideas need constant renewal.
4. Mawazo mazuri huvutia watu wa kukusaidia. Watu huwekeza matumaini, muda na fedha katika kujaribu kuyafanya mawazo mazuri kua uhalisia. Wapo watu wenye fedha lakini hawana mawazo, pia wapo watu wengi wenye mawazo lakini hawana fedha. Usiishie kuwa na wazo tu, bali hakikisha wazo lako ni zuri kiasi cha kuvutia wawekezaji, kama sio zuri mwanzoni endelea kubuni njia mbalimbali za kuliboresha wazo lako.
5. Uvumbuzi/ubunifu mkubwa unastahili jina kubwa. Aina ya jina ambalo ubunifu unapewa, hua linajalisha sana. Japo ubunifu mkubwa unaweza kuendelea kuwepo bila kua na jina kubwa lakini jina kubwa na zuri hua linasaidia sana hususani kama ubunifu huo ni wa bidhaa, huduma au kitu fulani utakachokua unajaribu kuuza chenye kuhitaji kua na brand nzuri.
6. Majina mazuri ya uvumbuzi, mara kadhaa huonekana ni mazuri baada ya kufanikiwa kufanya vizuri kwenye soko. Hakuna njia maalumu ya kuchagua jina zuri kwa ajili ya uvumbuzi. Mfano kampuni ya Apple, ilipata jina lake baada ya mwanzilishi wake (Steve Jobs) alidhani tunda la Apple ni tunda zuri na lililokamilika. Kampuni ya Ebay ilipata jina lake baada ya mwanzilishi wake kutaka iitwe “Echo Bay” ila ikashindikana, kisha akaamua kufupisha na kuiita Ebay, jina lililokuja kuonekana ni zuri sana. Hata hivyo kuweka juhudi katika kutafuta jina zuri na kuepuka jina baya ni vizuri na yafaa sana. A great name can allow an okay innovation to become a great brand.
7. Kila wazo jipya linajumuisha mawazo ya zamani. Uhalisia (originality) haupo katika kutengeneza kitu kutoka kwenye kitu kisichokuwepo kabisa (nothing). Tunaposikia kwamba hichi kitu ni Original (OG) haimanishi kwamba vimetengenezwa kutoka hewani. Uhalisia unategemea uwekaji pamoja wa mawazo na vifaa katika njia mpya. Kitu kinaweza kua original hata kwa kuunganisha mawazo yaliyokuwepo awali na kuyapangilia kwenye mtindo mpya, ili mradi tu huo mpangilio mpya uwe unakidhi mahitaji ya watumiaji.
8. Ni bora kuomba msamaha kuliko kuomba ruhusa. Ni mara chache sana unaweza kupata ruhusa ya kufanya kile unachodhani kinafaa. Kwa hofu ya kushindwa, tunaacha kufanya vile tunavyoamini na kusubiria mpaka tupewe ruhusa. Ukiona unapewa ruhusa kwenye kila unachotaka kufanya, basi ujue huna utofauti, au huna jipya, au hata kama ni mapya basi hayatishii kivilee. Ukitaka kufanya kitu cha tofauti usisubiri kuomba ruhusa Jiruhusu mwenyewe. Bora ukosee uje kuomba msamaha.
9. Uvumbuzi mwingi unahusisha uvunjaji au upindishaji wa kanuni. Sio uvunjaji kanuni ambao sio wa kimaadili au wenye nia ya udanganyifu, bali ni uvunjaji wa kanuni ambao ni muhimu kwa ajili ya kubuni mawazo, kuyajenga na kuyatoa nje. Kanuni zina msaada, maana zinatusaidia kufanya kazi pamoja. Japokuwa kanuni pia zinaweza kua kikwazo kwenye njia ya kufanya majaribio, uboreshaji na hata kupata mpenyo wa kiuvumbuzi. Kuna wakati inalazimika kuvunja kanuni ili kupata ubunifu. Doing something different is often only possible if you bend, break, and ignore rules.
10. Motisha yaweza kutoka nje au ndani. Unaweza kuwapa watu kazi wanayoipenda au waweza kuwalipa watu kufanya kazi wasiyoipenda. Wale wanaofanya kazi wanayoipenda ni kwamba wanapata motisha ya kutoka ndani, na wataifanya hiyo kazi kwa ubunifu zaidi. Wale wanaolipwa kufanya kazi wasiyopenda wao watakua wanajali zaidi kuhusu hiyo motisha kutoka nje (fedha) na hawatajisumbua kwenda mbele zaidi. Motisha ya ndani ni ya muhimu sana katika ubunifu. Kama unachofanya kinatatua tatizo fulani, na hamasa yako ikawa ni kuona watu wakinufaika na kile unachotoa, ni dhahiri kwamba utakua na motisha wa kutoka ndani. Motivation from inside is vital to creativity.
11. Viongozi wakubwa kwenye kampuni hawapati manufaa au tuzo kutokana na ubunifu wa wazo jipya. Hata hivyo ubunifu wa vitu vipya haupo kwenye maelekezo ya kazi zao (job descriptions). Mawazo mengi sana ya ubunifu hua yanazimwa na viongozi wa shirika au kampuni. Wao hawapo pale ili kuzalisha mawazo mapya, bali wapo pale kutunza kazi zao kwa kuendelea kutengeneza fedha zaidi. Wao wanafurahishwa kutengeneza fedha zaidi na kufanya kazi zao vizuri. Kama ukipeleka ubunifu kwa bosi wako ukashindwa kumuonyesha jinsi gani ubunifu huo unaweza kumsaidia na yeye kunufaika, basi uwezekano wa kupiga chini hilo wazo lako ni mkubwa.
12. Kutarajia mawazo yote kuwa na tija ni kukosa uhalisia. Ubunifu unaoleta ufumbuzi hua mara nyingi unapatikana baada ya majaribio mengi sana. Mfano Thomas Edson ambaye ni mvumbuzi wa taa ya kutumia umeme (bulb) alifanya majaribio kama 9,999 na yote hayo hakupata ufumbuzi, ila alipojaribu mara nyingine ndipo bulb ikagunduliwa. Hivyo unapaswa kujaribu tena na tena kutoka kila upande mpaka kuwe kuna kitu kimekua bora. Hii inatufundisha kwamba hata yale mawazo yanayoonekana hayana matumizi (useless) yanaweza kua na kazi maana katika kujaribu yapo mafunzo mengi unayoyapata ambayo yanakua msaada kwenye majaribio ya mbeleni katika kutengeneza mawazo yenye kufaa kutumika. Expecting all ideas to be useful is unrealistic
13. Anza na majaribio madogo madogo kabla ya kwenda kwenye majaribio makubwa. Majaribio mengi sana kwenye uvumbuzi hua hayafanikiwi kwa sababu unakuta rasilimali zote zimetumika kabla ya suluhisho sahihi kupatikana. Unapokua unafanya majaribio makubwa makubwa ina maana utahitaji rasilimali nyingi sana, hata ukifanikiwa kupata huo ubunifu, unakua huna tena rasilimali za kutekeleza maana zote zimeishia kwenye majaribio. Hebu fikiria Thomas Edson alivyojaribu mara 9,999, kama majaribio hayo yangekua ni makubwa yenye kuhitaji rasilimali nyingi, ni wazi kwamba asingefanikiwa kufikia majaribio hayo yote, maana angeishiwa rasilimali mapema kabla ya kupata suluhisho. Making as many small bets as possible increases the number of attempts possible and keeps options open
14. Ubunifu sio lazima kuanza na kitu kipya, unaweza kutumia vile vitu ambavyo tayari vipo. Pia unaweza kutumia hata yale majaribio ambayo wengine wamefanya wakashindwa au ambayo yameonekana hayana matumizi. Improve on the useless attempts of others.
15. Mawazo hua yana muda wake kuisha (expire date). Kama watu hawataweza kutumia mawazo haraka iwezekanavyo hua yanasahaulika. Kama hua hautunzi (hauhifadhi ) mawazo hua yanapotea. Pia kama hua hushirikishi mtu mawazo yako hua yanapotea. Unapopata wazo hakikisha unaliandika mahali, andika kila kitu unachofikiri kuhusu wazo hilo. Usipoandika kadri muda unavyokwenda ndivyo unavyosahau vitu vingi, lakini kikubwa ni kwamba unakosa ile hamasa ya utekelezaji wa lile wazo. Ukishaandika wazo lako, waweza kuwashirikisha watu unaowaamini, ambao unajua wana mchango mzuri kwako, usiogope kukosolewa, maana katika kukosolewa ndipo unajifunza na kupata maboresho ya wazo lako.
16. Uvumbuzi wenye thamani ni matokeo ya kutokukubaliana (disagreement). Pale panapokua na mawazo kinzani uwezekano wa kuzaliwa uvumbuzi ni mkubwa sana. Panapotokea kutokukubaliana usilaumu sana wengine kwa kuwaona wanakosea, mnapotofautiana ndio mnapata mawazo mapya. Kama watu wakiwa na umoja sana, na wakakubaliana sana kwenye kila kitu, hua mara nyingi hakuna mawazo mapya. Watu wanahitaji umoja wa kutosha ila sio uliozidi kiasi pia wanahitaji kukinzana ila sio sana hadi kushindwa kufanya kazi pamoja. Patience Is Needed With Disagreement.
17. Viongozi ni wa muhimu sana katika ubunifu. Kama viongozi watakua na mtazamo wa mbele, watu wanaowaongoza watatumia muda mwingi kujiandaa kwa ajili ya wakati ujao. Kufikiri kuhusu wakati ujao (future) kunarahisisha kuamini kwamba yale yasiyowekana yatawezekana. Kama kiongozi atakua anatizama wakati wa sasa tu, watu anaowaongoza katika kufanya ubunifu watatumia muda mwingi kufanya vile wanavyoviweza kwa wakati huu wa sasa tu na hivyo kukosa muda wa kufikiri vitu vinavyoweza kufanyika wakati ujao. Kufikiri kwa ajili ya wakati uliopo tu, kunawafanya watu kuingia kwenye mtego wa kufuata kanuni na shinikizo za wakati uliopo. Mfano wanaweza kua wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha malengo ya mwezi huu yanafikiwa, lakini wakashindwa kutizama ni nini mahitaji ya wateja kwa mwaka ujao. Kiongozi ndio anapaswa kuongoza timu yake, maana watu wanamtizama sana kiongozi, wanaangalia jinsi anavyofikiri, jinsi anavyowasiliana, pia wanaangalia ishara. Leaders matter to innovation. The way you think. The way you talk.
18. Fanya kile ambacho mshindani wako hataweza kukifanya. Kuna shida katika ushindani, maana mnajikuta mnaishia kupigania eneo moja, kwenye mipaka ile ile. Ni kama vile mbwa wanaogombania mfupa mmoja. Kwanini usitafute eneo lako? Kwanini usitafute mfupa wako? Tafuta eneo ambalo halina mvuto kwa huyo mpinzani wako lakini unaweza kufanya kitu kizuri kwa ajili ya watu ambao wanahitaji kukinunua. DO WHAT YOUR COMPETITION WON’T
19. Kujifunza vitu vipya ndio moyo wa ubunifu. Kuna ushahidi unaoonyesha kwamba ubunifu ni ujuzi ambao kila mtu anaweza kujifunza. Kama wewe ni mwajiri, katika kuajiri usiishie kuajiri mtu kwa kile anachokijua tu bali angalia huyo mtu anajifunzaje vitu vipya. Ni kweli unahitaji mtu mwenye ujuzi tayari ambaye anafahamu vitu tayari, lakini hiyo haitoshi, maana vile anavyofahamu leo haina maana na kesho vitahitajika. Kama mtu hana hamasa ya kujifunza vitu vipya anaweza kukufaa kwa sasa, lakini kwa baadaye hata kufaa, maana ataendelea kubaki na kile anachokijua tu. Don’t just hire for what they can do now or for what you need doing now. Things will change. Consumer tastes will change. The market will change.
20. Mafanikio ya jana sio dhamana ya mafanikio ya kesho. Watu hupenda kukusifia kwa matokeo mazuri ya sasa, ambayo yametokana na maamuzi mazuri uliyofanya wakati uliopita. Kwa bahati mbaya ukiamini sifa unazopewa na kulowea kwenye sifa hizo uwezekano ni mkubwa ukafanya maamuzi yasiyo mazuri ambayo yataleta matokeo mabaya wakati ujao Warning – Past success does not guarantee future success.
Asante sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

2 thoughts on “Mambo 20 Niliyojifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha The Truth About Innovation (Ukweli Kuhusu Uvumbuzi)

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: