Dunia inabadilika kwa kasi sana, kadiri siku zinavyokwenda vitu na watu wanabadilika sana. Na mabadiliko haya yanakuja na mambo mazuri na mambo mabaya pia.

Kuna vitu viwili muhimu sana ambavyo vimekuwa adimu sana kwenye dunia ya sasa. Vitu hivi vina thamani kubwa sana na ni mtaji wa kukuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako. na uzuri ni kwamba vitu hivi viwili vinaanzia ndani yako mwenyewe, na wala huhitaji kwenda kuvinunua.

Vitu hivi vimekuwa adimu kwa sababu tunaishi kwenye dunia ambayo kuna vitu vingi sana vya kufanya, na muda tulionao hautoshi kufanya vitu vyote tunavyotaka. Katika kukazana kufanya kila tunachotaka kufanya, ndipo tunapopoteza vitu hivi viwili muhimu sana.

Kitu cha kwanza ni UMAKINI. Umakini umekuwa adimu sana katika zama hizi. Hizi zama za facebook, wasap, instagram na mitandao mingine ya kijamii, ni vigumu sana kuweza kuituliza akili sehemu moja kwa umakini. Badala yake watu wamekuwa wakiruka ruka huku na huko kwenye mitandao ya kijamii na mambo mengine ambayo yanawapunguzia umakini.

Bila ya umakini kwenye kitu chochote unachofanya, huwezi kutoa matokeo bora. Na kama akili yako haijatulia sehemu moja, umakini unapotea. Kwa dunia ya sasa ambapo tumeunganishwa na dunia nzima kwa masaa 24 kwa siku, unahitaji kufanya juhudi za ziada kujijengea umakini.

Kitu cha pili ni UAMINIFU. Imani imekuwa ndogo sana katika nyakati hizi. Mtu anaweza kuongea chochote, kuahidi chochote ambacho hana uhakika kama anaweza kutekeleza. Na hili limepelekea watu wengi kushindwa kutimiza vile walivyoahidi. Ukosefu wa umakini unachangia sana kupungua kwa imani. Kwa sababu mtu anaweza kuahidi akijua mambo yatakwenda vizuri, ila ukosefu wa umakini ukamzuia kumaliza kwa wakati. Unahitaji kujijengea uaminifu mkubwa sana kwenye maisha yako na kupitia kile unachofanya, ukiahidi timiza.

Ukiwa na umakini, utaweza kufanya mambo yako na kumaliza kwa wakati. Ukiwa na uaminifu utapata watu wengi wanaotaka kufanya kazi na wewe. Na kwa sababu una umakini, utaongeza wengi zaidi. Huu ni mtaji tosha kwako, anza sasa kujijengea umakini na uaminifu.

SOMA; UAMINIFU; Uhusiano kati ya tabia ya uaminifu na mafanikio Makubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kwenye dunia ya sasa umakini na uaminifu vimekuwa adimu sana. Na kwa sababu kitu chochote adimu kina thamani kubwa, nitahakikisha nakuwa mwaminifu na makini kwenye kila jambo nitakalofanya, hii itaniletea matokeo bora na kuwavutia wengine kuwa karibu na mimi. Najua huu ni mtaji muhimu sana kwangu.

NENO LA LEO.

Trust in what you love, continue to do it, and it will take you where you need to go.

Natalie Goldberg

Uaminifu ndio kitu unachokipenda, endelea kuwa mwaminifu na utaweza kwenda popote unapotaka kwenda.

Uaminifu ni mtaji mkubwa sana kwako kuweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, ulinde mara zote.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.