Katika matatizo yote unayopitia kwenye maisha yako, naweza kusema asilimia 90 yanasababishwa na hisia. Hisia sio nzuri kabisa kwenye ufanyaji wa maamuzi.

Hisia na kufikiri haviwezi kwenda pamoja. Unapokuwa na hisia kali kufikiri kunakuwa chini sana. Na unapoweza kuzishusha hisia zako chini, ndio unaweza kufikiri sawasawa.

Hisia ndio zimekuwa zinatufanya tunaingia kwenye ugomvi na wengine, hisia ndio zimekuwa zinatufanya tunakata tamaa, hisia ndio zimekuwa zinasababisha tunatapeliwa.

Kwa mfano kama mtu amekutukana, kinachokuja haraka kwenye akili yako ni nini? Kuumizwa kwa hisia, kwa nini amenitukana, amenionaje, amenishushia heshima, lazima nitamwonesha na mengine mengi. Hatimaye na wewe unamtukana na dakika chache mpo kwenye vita kali. Lakini kama mtu huyu alipokutukana ulizizuia hisia zako na kuepuka kulikuza hilo, baadae unaweza kumfuata ukiwa umetulia na kumuuliza tatizo ni nini mpaka akutukane, na huenda mkayamaliza vizuri bila hata ya kudhalilishana zaidi.

Mfano mwingine unajua fika kabisa kwamba ili upate fedha ni lazima uweke juhudi kubwa. Kwamba hakuna fedha zinazopatikana kirahisi. Anakuja ndugu yako au mtu wako wa karibu, anakwambia kuna dili nzuri nimeipata, nipe milioni moja na nitakurudishia milioni moja na laki tano baada ya mwezi mmoja. Kwa kusikia hivi tu hisia zako zinapanda na unashindwa kabisa kufikiri. Yaani laki tano kwa mwezi mmoja, bila ya kufanya chochote? Chukua milioni hii hapa, akishaondoka na ukakaa chini na kufikiri, baada ya hisia kushuka, utaishia kuomba iwe tu sio uongo, maana utagundua umefanya makosa.

Jitahidi sana kuzidhibiti hisia zako katika hali yoyote unayoipitia. Najua siyo jambo rahisi lakini jifunze kila mara, unapoona unakimbilia kufanya jambo au maamuzi au chochote ndio wakati wa kusimama kwanza, kutokufanya chochote nakufikiri kwa kina.

Hisia zina msaada wake katika kuyafanya maisha yetu yawe bora, lakini zinapokutawala, maisha yanakuwa hovyo sana.

SOMA; Hisia mbili zinazowaongoza binadamu na jinsi ya kuzitumia kwenye biashara na ujasiriamali.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba hisia zangu ndio zimekuwa zinaniletea matatizo mengi hasa pale ninaposhindwa kuzidhibiti. Kuanzia sasa nimeamua kuwa nazidhibiti hisia zangu ili niweze kufikiri vyema na kufanya maamuzi ambayo ni sahihi kwangu.

NENO LA LEO.

Your emotions are very unstable and should never be the foundation for direction in your life.

Joyce Meyer

Hisia zako siyo imara hivyo kamwe usizifanye kuwa ndiyo msingi wa mwelekeo wa maisha yako.

Hakikisha unadhibiti hisia zako maana hizi ndiyo zinakuingiza kwenye matatizo makubwa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.