Mpaka sasa nina hakika unajua hili, ya kwamba ili kuweza kufikia mafanikio makubwa, unahitaji kuweka juhudi kubwa sana, yaani sana. Kama wenzako wanafanya kwa kawaida, wewe unahitaji kwenda mbali zaidi. Na kama mpaka sasa hukubaliani na hilo, usiendelee kusoma.

Sasa kuna sababu mbili za kuweka juhudi kubwa sana.

Sababu ya kwanza ni kuwaonesha wengine kwamba wamekosea, au hawakujua. Labda kuna mtu alikuambia huwezi, na sasa unataka kumwonesha kwamba unaweza, na unajitoa kuweka juhudi kubwa sana. Na bila ya ubishi utafanikiwa kufikia chochote unachotaka, maana hasira hii inakuletea nguvu kubwa sana.

Sababu ya pili ni kuweka juhudi kwa sababu ndicho kitu umechagua kufanya, na unajua unaweza, bila ya kujali wengine wanasema nini. Hapa unajitoa kweli kuweka juhudi kwa sababu ndio umeamua na ndiyo kitu muhimu zaidi kwako. Hata watu waseme nini hawakusumbui. Kwa njia hii pia ni lazima utafanikiwa, maana hakuna wa kuzuia nguvu hiyo kubwa ya maamuzi yako.

Je wewe ni sababu ipi inayokusukuma?

Kwa haraka unaweza kusema kwa kuwa sababu zote zinaleta matokeo unayotaka, basi haijalishi sababu inayokusukuma ni ipi.

Lakini kuna tofauti kubwa sana, kama sababu yako ni ya kwanza, utayafikia mafanikio, lakini baada ya hapo bado utaona maisha yako hayajakamilika. Na kama sababu yako ni ya pili, utayafikia mafanikio na maisha yako yatakuwa yamekamilika.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Why Motivating People Doesn’t Work And What Does. (Sayansi Mpya Ya Hamasa Na Uongozi)

TAMKO LANGU;

Juhudi kubwa ninazoweka sasa ili kufikia mafanikio makubwa, zinaweza kuwa zinatokana na mimi kutaka kuwaonesha wengine kwamba wamekosea, au zinaweza kuwa zinatokana na mimi kuchagua hiki ndiyo kitu ninachotaka. Sitakubali kuendeshwa na sababu za kuwaonesha wengine wamekosea, badala yake nitachagua kile ambacho ndio ninataka na kuweka juhudi zangu zote.

NENO LA LEO.

The will to win, the desire to succeed, the urge to reach your full potential, these are the keys that will unlock the door to personal excellence – Confucius

Hitaji la kushinda, hamu ya kufanikiwa, haja ya kufikia uwezo wako mkubwa, hizi ni funguo zitakazofungua mlango wa ubora wa hali ya juu.

Hakikisha sababu ya wewe kuweka juhudi kubwa ili ufanikiwe inatoka ndani yako na siyo kutaka kuwaonesha wengine.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.