Mtu yeyote ambaye amewahi kupanda mlima mrefu, Kilimanjaro au mwingine wowote, atakuambia kitu kimoja muhimu, hakujikuta kileleni. Badala yake alianza kupiga hatua moja baada ya nyingine, na kidogo kidogo akapanda mpaka kufikia kileleni.

Huu ndio ukweli wa maisha, huwezi kuibukia kileleni, yaani ukajikuta tayari upo kileleni, hakujawahi kutokea muujiza wa aina hiyo. Unapiga hatua moja baada ya nyingine na hatimaye unafika kileleni, kama hutaacha.

Lakini tunapokuja kwenye maisha ya kawaida, hasa maisha ya zama hizi, watu wamekuwa wakifikiri wanaweza kuibukia kileleni. Kwamba umeanza kazi na baada ya muda mfupi umepanda cheo na kuwa nafasi za juu. Au umeanza biashara na baada ya miezi kadhaa unamiliki biashara kubwa sana na yenye mafanikio makubwa.

Hiki ni kitu ambacho wengi wamekuwa wakijidanganya na imepelekea kukata tamaa hasa pale wanapokutana na uhalisia wa maisha.

Kama ilivyo kwenye kupanda mlima, njia siyo rahisi. Kwanza ni kupanda mlima, KUPANDA, nafikiri unaelewa vizuri ilivyo vigumu kupanda. Pili njia inakuwa na mawe, tatu kuna kuchoka. Lakini unapoamua unafika kileleni.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha pia, chochote unachotaka hakitakuwa rahisi, utakutana na magumu, utakutana na changamoto na utakutana na hali nyingi za kukatisha tamaa. Lakini utakapojua kwamba hakuna njia nyingine ya uhakika ya kufika kileleni, utaendelea na safari yako.

Ndiyo tutakutana kileleni, kwenye kilele cha mafanikio. Ila hatutaibukia pale, badala yake tutapanda kidogo kidogo. Kwa kuwa tayari kuweka juhudi kubwa na kutokukata tamaa.

SOMA; Mambo Kumi(10) Muhimu Usiyojua Kuhusu Mafanikio, Na Jinsi Yanavyokurudisha Nyuma.

TAMKO LANGU;

Nimejikumbusha ya kwamba safari yangu ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio haitakuwa rahisi, lakini sitaiacha safari hii. Sitegemei kuibukia kwenye kilele cha mafanikio, nimejiandaa kupanda hatua kwa hatua mpaka kufika kileleni. Hakuna kitakachonitoa kwenye safari hii.

NENO LA LEO.

“Every mountain top is within reach if you just keep climbing.”

― Barry Finlay

Unaweza kufikia kilele cha mlima wowote kama utaendelea kupanda bila ya kukata tamaa.

Mafanikio hayatokei kama ajali, bali yanatokana na juhudi unazoweka kwa muda mrefu, kama ilivyo kwenye kupanda mlima, hatua kwa hatua.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.