Akili yako na mawazo yako yote yanapaswa kuwa kwenye kile kitu ambacho unakitaka au unakitafuta, na siyo mahali pengine popote. Kuiondoa akili yako kwenye kile unachotaka na kuanza kufikiria kingine ni kujipoteza.
Kama unataka kufanikiwa kwenye jambo lolote, ni lazima ufikirie jambo hilo, ni lazima uangalie kule unakotaka kwenda. Na siyo kuangalia kule ulikotoka au kwingine ambapo siyo muhimu kwako.
Kwa mfano kama unakimbia mbio za mita 100, na tayari umeshakimbia mita 60 na zimebaki mita 40, una njia mbili za kuliangalia hili;
Moja unaweza kuangalia kwamba tayari nimekimbia mita 60, pamoja na urefu wote huu bado hata sijamaliza. Kwa kufikiri hivi unaweza kukata tamaa.
Pili unaweza kuangalia ya kwamba umebakisha mita 40 pekee ili ukamilishe mbio zako. Kwa kufikiri hivi utapata hamasa zaidi ya kumalizia sehemu iliyobaki.
Hivi ndivyo unavyopaswa kufikiri kwenye safari yako ya mafanikio, usiangalie ni umbali kiasi gani umekwenda mpaka sasa, bali angalia ni umbali kiasi gani umebaki ili ukamilishe lengo. Kwa kuangalia hivi utapata hamasa kubwa ya kuendelea kuweka juhudi ili kufikia malengo yako.
Ni mbele kwa mbele, usirudi nyuma, nyuma ni mwiko. Na fikra zako pia ziwe mbele kwa mbele.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba safari yangu ya mafanikio nahitaji kufikiria zaidi kule ninakokwenda kuliko kule nilikotoka. Najua kwa kuangalia kule ninakokwenda nitapata hamasa zaidi na nikiangalia kule nilikotoka naweza kukata tamaa. Nitaangalia nilipotoka kwa kujifunza tu, lakini mawazo yangu yote yatakuwa mbele kwa mbele.
NENO LA LEO.
Una njia mbili za kuiangalia safari yako ya mafanikio; unaweza kuangalia kule ambapo umetoka mpaka kufikia sasa, lakini hii inaweza kukukatisha tamaa, hasa kama umepitia changamoto nyingi. Pia unaweza kuangalia kule unakoelekea na kiasi gani kimebaki ufikie malengo yako, hii itakuhamasisha zaidi. Mara zote fikiria mbele, angalia ni kiasi gani umebakiza ili kufikia lengo lako, hii itakupa msukumo wa kulifikia.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.