Wewe kama mfanyabiashara, mara kwa mara utajikuta kwenye mazungumzo na watu wengine, ambayo yanahusu biashara au mambo mengine.
Watu hawa wanaweza kuwa wafanyabiashara wenzako,  wateja wako au wawekezaji.
Na mnaweza kuwa mmekutana kwenye mkutano au kwenye eneo la biashara.
Katika kuzungumza, mada nyingi zinaweza kujitokeza na mkachangia. Hii ni vizuri kwani mnajenga uhusiano mzuri ambao mnaweza kuutumia zaidi kibiashara.
Lakini unahitaji kuwa makini sana na mada unazojadili katika mazungumzo ya kibiashara unayokuwepo.
Kuna baadhi ya mada zinaweza kukufanya ukose wateja au ukose fursa za kibiashara. Ni muhimu ujue mada hizi na uziepuke ili kuondoa nafasi ya wewe kukosa fursa.
Hizi hapa ni mada tatu unazotakiwa kuziepuka unapokuwa kwenye mazungumzo ya kibiashara.
1. Mada zinazohusu mapenzi.
2. Mada zinazohusu siasa.
3. Mada zinazohusu dini.
Hayo ni maeneo muhimu ya maisha yetu lakini usiyajadili kwenye biashara.
Hii ni kwa sababu watu wengi huchukulia mambo hayo kwa hisia, hivyo inapotokea mnatofautiana inaweza kupelekea kuumizana hisia.
Na mtu yeyote anayeumia hisia ataepuka sana kile ambacho kiliumiza hisia zake.
Hivyo kuwa makini, unachotaka ni kuendesha na kukuza biashara yako, na sio kujua dini ipi au chama kipi cha siasa ni bora kuliko vingine. Hayo ni maongezi unaweza kuchagua kufanya na watu wengine, ambao hawahusiki na biashara yako.
Nakutakia kila la kheri.