Kuna vitu vingi sana unavyotakiwa kujali kwenye maisha haya, vitu ambavyo vinatakiwa kukuumiza kichwa kuhusu shughuli unazofanya na maisha kwa ujumla.
Lakini kuna kitu kimoja unatakiwa kujali zaidi, kuna kitu kimoja ambacho kinatakiwa kukuumiza zaidi kuliko vitu vingine. Kitu hiko ni wanaokuamini.
Anza na swali ni nani anayekuamini? Ni watu gani ambao wanakuamini?
Tunaishi kwenye dunia ambayo uaminifu ndiyo msingi pekee wa kujenga mahusiano bora. Na ni kutoka kwenye mahusiano bora ambapo unaweza kutengeneza maisha bora na ya mafanikio. Mahusiano bora na mwajiri wako, mahusiano bora na wateja wako na mahusiano bora na familia yako.
Unahitaji kujali sana ni nani anayekuamini kwa sababu wale wanaokuamini ndio wanaowezesha maisha yako kusonga mbele. Wale wanaokuamini ndio wanaokulisha, wanaolipia gharama za maisha yako, wanaolipia watoto wako ada ya shule. Ni wale wanaokuamini tu ndio wanafanya hivi na sio vinginevyo.
Na hii ni kwa kila mtu, iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara. Iwe ni msanii, mwandishi, mkulima, daktari au mfagia barabara. Watu wanaokuamini ndio wanaokupa wewe fursa za kusonga mbele zaidi kwenye kile unachofanya.
Hivyo acha kuhofu unawezaje kusonga mbele, na badala yake jali ni watu gani wanakuamini na wewe unawaamini pia. Maana hapa ndipo penye hazina yako. tengeneza mahusiano ya uaminifu na mtu yeyote unayekutana naye au unayofanya naye kitu chochote. Mahusiano hayo yatakulipa vyema hapo baadaye.
SOMA; SIRI YA 30 YA MAFANIKIO; Uaminifu Unalipa Gawio Kubwa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba wale wanaoniamini ndio watu muhimu sana kwenye maisha yangu. Kwa sababu watu hawa ndiyo watanipa fursa za kuweza kufanya kile ninachofanya na kufaidika nacho. Nitahakikisha najenga mahusiano ya uaminifu na watu wote wanaonizunguka ili nijiweke kwenye nafasi ya kupata fursa nyingi na nzuri zaidi.
NENO LA LEO.
Watu wanaokuamini ndio wanaokupa wewe fursa za kuishi maisha ya mafanikio. Watu hawa ndio wanaokuajiri, au wanaonunua kwako au wanaokupa ushirikiano kwenye jambo lolote unalofanya.
Jenga mahusiano ya uaminifu na mtu yeyote unayekutana naye au kufanya naye kitu chochote. Mahusiano haya yatakulipa vizuri sana baadaye.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.