Kujua thamani ya biashara yako na kipato unachoweza kuingiza kupitia biashara hiyo ni moja ya vitu muhimu unavyotakiwa kuzingatia. Na kama ukiweza kufanya hivi kabla hujaanza biashara yako unaweza kuianza ukiwa na mpango bora wa kutoa thamani kubwa na kutengeneza kipato kizuri. Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara na kufanya kwa mazoea, hivyo pale wanaposhindwa kutengeneza faida au kukuza biashara zao wanashindwa kujua ni hatua zipi sahihi kwao kuchukua. Leo kupitia makala hii ya KONA YA MJASIRIAMALI, tutakwenda kujifunza vitu vinne vinavyochangia thamani ya biashara yako na kuamua ni kipato gani unaweza kutengeneza kupitia biashara hiyo.
- Mahitaji.
Kiti cha kwanza kabisa ni mahitaji au uhitaji wa kile ambacho wewe unatoa au unataka kutoa. Je watu wana uhitaji kiasi gani kwa bidhaa au huduma ambayo unaitoa? Kadiri uhitaji unavyokuwa mkubwa, ndivyo ambavyo thamani inavyozidi kuwa kubwa. Hapa unahitaji kujua ni shida ipi ambayo watu wanayo na inawaumiza na wapo tayari kuitatua shida hiyo. Na hapo unaangalia kwa jicho la biashara yako, kujiuliza inawezaje kutatua changamoto ambazo watu wanazo kwa sasa.
Kama unataka kutengeneza faida nzuri kwenye biashara, basi angalia kitu ambacho watu wana uhitaji mkubwa nacho na wapatie. Unapogusa pale panapouma, watu lazima watafute kitu cha kutuliza yale maumivu yao. Hili ni zoezi ambalo unaweza kulifanya kwa urahisi kwa kuangalia biashara yako na matatizo ambayo watu wanayo na kuona inawasaidia vipi.
- Upatikanaji.
Kitu cha pili kinachochangia thamani ya biashara yako na kipato pia ni upatikanaji wa kile ambacho wewe unauza, au unataka kuuza. Kama kinapatikana kwa urahisi, basi thamani yake inakuwa siyo kubwa na hata faida utakayopata inakuwa ni kidogo. Kama kila mtu anaweza kufanya biashara unayoifanya wewe na kwa namna ile ile, basi huna kitu kikubwa cha kushindana. Mnaishia kugombea wateja wachache kwa ninyi wafanyabiashara ambao mmeshindwa kujitofautisha.
Kama unataka kufanya biashara ambayo ina thamani kubwa, unaweza kuanza na vitu hivi viwili muhimu, kuangalia mahitaji ambayo watu wanayo, na pia kuangalia yale ambayo hayapatikani kwa urahisi. Mara nyingi vitu ambavyo havipatikani kwa urahisi ni vigumu kufanya na hivyo wengi kutokuwa tayari kufanya, hii inapelekea thamani yake inakuwa kubwa. Lakini vitu vinavyopatikana kwa urahisi siyo vigumu kufanya, na kila mtu anakimbilia kufanya ndiyo maana thamani yake inakuwa ndogo.
Hata kama unafanya biashara ambayo inafanana na ya wengine, angalia ni jinsi gani unaweza kuwapatia wateja wako kitu ambacho hawakipati kutoka kwa wafanyabiashara wengine.
- Ubora.
Hiki ni kitu kingine muhimu sana ambacho wateja wanatumia kuweka thamani kwenye biashara yako. kama kile unachotoa ni bora, basi wengi watakithamini na unaweza kuuza kwa bei kubwa. Lakini kama unachotoa siyo bora, wengi watajua siyo bora na hawatakithamini. Utalazimika kuuza kwa bei ndogo ili ufanye biashara na hapo ndipo unazidi kukosa faida.
Mara zote jiwekee viwango vya ubora kwenye biashara yako ambavyo ni lazima ukazane kuvifikia mara zote. Kwa njia hii wateja wako watajijengea mtazamo huu kuhusu wewe na wataithamini biashara yako. Lakini kama utashindwa kujiwekea viwango vya ubora na kuvifuata, hakuna mteja atakayekuwa anakutegemea wewe. Watu wanapenda vitu vilivyo bora ili kuhakikisha fedha yao inatumika kwa ufasaha.
- Wingi.
Wingi wa kile unachotoa pia unahusika kwenye thamani na kipato cha biashara yako. Kama una vitu viwili vyote vya ubora sawa na bei sawa, lakini vina ujazo au wingi tofauti, wengi watanunua kile ambacho kina ujazo mkubwa, au wingi zaidi. Hivyo angalia ni kwa jinsi gani unaweza kuongeza wingi kwenye biashara yako.
Unahitaji kuwa makini kwenye wingi kwa sababu wengi wanapoongeza wingi huwa wanapunguza ubora. Hivyo hakikisha unaongeza wingi na ubora nao pia unaongezeka. Hata kama gharama itakuwa juu, wateja wengi wapo tayari kulipa gharama za ziada kupata kitu ambacho ni bora na kinamtosheleza kulingana na mahitaji yake.
Mara zote ifikirie biashara yako katika maeneo hayo manne muhimu, na jiulize ni eneo lipi unahitaji kufanyia kazi ili kuongeza thamani ya biashara yako na kipato chako pia. Nakutakia kila la kheri.