Siyo vibaya kukasirika, kama unaweza kuzidhibiti hasira zako. Kama utaweza kujizuia usichukue hatua kutokana na hasira ulizonazo, kwa sababu hatua unazochukua wakati ukiwa na hasira, huwa siyo hatua nzuri. Hili ni jambo muhimu sana la kuzingatia pale unapokuwa umekasirika.

Leo tunakwenda kuchimba ndani na kuangalia ni upi hasa msingi wa hasira. Kwa kujua msingi huu utaweza kuzitawala zaidi hasira zako na hivyo kufanya maamuzi bora sana kwako na wanaokuzunguka.

Msingi wa hasira ni hofu. Kinachokufanya ukasirike siyo kitu ambacho kimetokea au hakijatokea, bali hofu uliyonayo wewe juu ya vitu hivyo. Kadiri unavyokuwa na hofu juu ya mambo fulani ndivyo unavyopata hasira pale yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea yaende. Unakuwa na hofu kwamba mambo yatakuwa mabaya zaidi mbeleni au utapoteza zaidi na hivyo kupata hasira.

Tukiweza kuzigundua hofu hizi tulizonazo tutaweza kupunguza sehemu kubwa ya hasira zetu, au hata kujua njia sahihi ya kuzitatua. Unapokuwa na hasira, kaa chini na jiulize ni nini nahofia kwenye jambo hili linalonipa hasira. Ukiweza kuangalia jambo hilo vizuri utaona hatua sahihi kwako kuchukua ambazo zitakuondolea hasira uliyonayo mara moja.

Hata kama una hasira na mtu kwa muda mrefu, kaa chini na jiulize ni kitu gani unahofia juu ya mtu huyo kinachokufanya uwe na hasira. Unapoangalia hofu hizi unakuja kugundua ya kwamba mambo mengi yanayokupa hasira hayastahili kabisa kukukasirisha.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Usiruhusu Vitu Vidogo Viharibu Siku Yako.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba msingi wa hasira ni hofu. Hasira zangu hazitokani na kile kinachotokea au kutokutokea, bali zinatokana na hofu nilizonazo juu ya kinachotokea au kushindwa kutokea. Kuanzia sasa nitakuwa nazichunguza hasira zangu kwa undani ili nione hofu nilizonazo.

NENO LA LEO.

Msingi wa hasira ni hofu. Kinachokukasirisha wewe siyo kile kinachotokea au kutokutokea, bali zile hofu ulizonazo juu ya kinachotokea au kutokutokea.

Kila unapokuwa na hasira, jiulize ni kitu gani unachohofia na utaweza kuondokana na hasira zako bila ya kujiingiza kwenye matatizo mengine.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.