Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba ili waweze kubadili maisha yao basi wanahitaji kufanya mapinduzi makubwa sana ndani ya muda mfupi. Wanakuwa wanawaangalia wale ambao wameshapiga hatua na kuona kwamba wakiweza kupiga hatua moja pekee watakuwa mbali sana.

Lakini hivi sivyo mambo yanavyokwenda, hakuna mtu anayeweza kufanya mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi. Mabadiliko yoyote unayoyaona yanafanyika kidogo kidogo ndani ya muda mrefu. Baadaye ndiyo yanakuja kuonekana ni mabadiliko makubwa. watu wote unaoona wamefika mbali, hawakujikuta pale siku moja, bali walifanya mambo madogo madogo ambayo kwa pamoja yamewafikisha pale.

Unachohitaji ni kufanya kwa asilimia moja tu kila siku. Kila siku fanya kitu kidogo ambacho kinakuelekeza kwenye malengo yako. Uzuri wa vitu hivi vidogo unavyofanya (1%) ni kwamba havitakuchosha na wala avihitaji maandalizi makubwa au kubadili maisha yako sana. Pia unapofanya kwa muda mrefu vinakuwa tabia na hivyo unajikuta unafanya tu bila hata ya kufikiria sana.

Kwa mfano kama unataka kuwa msomaji mzuri wa vitabu, panga kusoma kurasa 10 tu kwa siku, ukifanya hivi kila siku kwa mwaka utasoma kurasa 3650, hii ni sawa na vitabu 15 mpaka 20 kwa mwaka mmoja. Sasa mtu akikuambia nimesoma vitabu 20 kwa mwaka unaweza kumshangaa sana, labda ana muda mwingi, lakini ukweli ni kwamba amesoma kurasa kumi tu kila siku, kitu ambacho hata wewe unaweza kufanya, bila haya kuharibu ratiba zako nyingine.

Kama unahitaji afya bora, ni kuchagua kupanda ngazi badala ya lifti, kuchagua kusimama na kutembea badala ya kuzunguka kwenye kiti. Kuchagua kula mbogamboga na matunda badala ya vyakula vya haraka.

Kama unahitaji kuwa na mahusiano bora na wengine ni kuchagua kuwa na mazungumzo chanya na watu hao. Kuchagua kuwajali kwa mambo madogo madogo.

Siku moja mtu aliniandikia, natamani siku moja niweze kuandika kama wewe, niwe na wasomaji wengi kama wewe. Nikamwambia siku hiyo haitatokea yenyewe, bali unaitengeneza wewe mwenyewe, kwa kuanza kuandika sasa. Na wala haihitaji uandike vitu vingi kwa siku, unaweza kuandika ukurasa mmoja tu, lakini unapofanya kila siku, zinakusanyika na kuwa nyingi, au hata kuwa kitabu kabisa. Fanya kidogo kila siku, na mafanikio hayawezi kukukimbia.

SOMA; KITABU; Kurasa Za Maisha Ya Mafanikio, Nidhamu Uadilifu Na Kujituma.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba mafanikio hayatokani na tukio moja kubwa, bali matukio mengi madogo madogo yanayotokea kwa muda mrefu. Kuanzia sasa, kila siku nitafanya kwa angalau asilimia moja kuelekea kwenye malengo yangu. Kila siku nitachagua kitu kidogo cha kufanya ambacho kitanisogeza kwenye malengo yangu.

NENO LA LEO.

Ili kufikia mafanikio huhitaji kufanya mabadiliko makubwa sana ndani ya muda mfupi, badala yake unahitaji kufanya mabadiliko madogo madogo kwa muda mrefu.

Kila siku unahitaji kufanya kwa asilimia moja kile ambacho unataka kufikia kwenye maisha yako. Soma kurasa 10 za kitabu kila siku na kwa mwaka utakuwa umesoma vitabu visivyopungua 15.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.